Guardiola anaweza kufeli Manchester City
Pep Guardiola
Muktasari:
PEP Guardiola amepewa nafasi ya kukalia kitimoto cha Manchester City. Wengi wanasubiri kwa hamu kuona kama kocha huyu kijana ataipa makali timu hii na kuiweka katika anga za juu kama alivyo kwa Barcelona ya enzi zake. Hata hivyo, kuna sababu za kwa nini Guardiola anaweza kufeli Man City.
PEP Guardiola amepewa nafasi ya kukalia kitimoto cha Manchester City. Wengi wanasubiri kwa hamu kuona kama kocha huyu kijana ataipa makali timu hii na kuiweka katika anga za juu kama alivyo kwa Barcelona ya enzi zake. Hata hivyo, kuna sababu za kwa nini Guardiola anaweza kufeli Man City.
Mtihani wake wa kwanza
Huu unaweza kusema kwa urahisi tu kwamba utakuwa mtihani wa kwanza kwa kocha huyu Mshipaniola. Alipokuwa na Barcelona Ligi ya Hispania ilikuwa inatawaliwa na timu mbili tu, Barcelona na Real Madrid. Kama ukifanikiwa kumpiku Real Madrid basi daima unakuwa juu. Alipokwenda Bayern Munich, Guardiola aliikuta Bayern Munich ikiwa ndiyo timu tawala kama ilivyo kwa miaka yote hiyo. Hata hivyo, kwa kuja katika Ligi Kuu England, huo utakuwa mtihani wa kwanza halisi wa maisha ya ukocha ya Guardiola. Katika soka la Kiingereza, Guardiola atakutana na timu nyingi zinazowania ubingwa na si kusubiri kufungwa na Guardiola. Timu hizi ni kama vile, Manchester United, Chelsea, Arsenal, Liverpool, Tottenham na sasa mabingwa wapya, Leicester City. Vile vile Guardiola atakutana na makocha wenye mbinu na uzoefu wa Ligi Kuu England kama Arsene Wenger, Jose Mourinho, Rafael Benitez, Claudio Ranieri na wengineo. Haitakuwa kazi rahisi.
Ligi ngumu/pesa
Ligi za Hispania na Ujerumani ni tofauti sana. wakati nchini Hispania timu za Barcelona na Real Madrid zina mgawo mkubwa katika pesa za haki ya mauzo ya televisheni, nchini Ujerumani, Bayern Munich ndiyo klabu yenye nguvu kubwa kiuchumi kiasi cha kuwanunua wachezaji mahiri wa wapinzani wao mara kwa mara. Hata hivyo, hali hiyo haipo England. Klabu nyingi zimejikwamua kiuchumi na zina uwezo wa kuvutia wachezaji wazuri. Kitu kibaya zaidi kwa Guardiola ni kwamba kuanzia msimu ujao klabu za Ligi Kuu England zitakuwa tajiri zaidi kutokana na ongezeko la mgawo wa mauzo ya haki za Televisheni. Klabu kama Leicester City ina ubavu wa kumnunua mchezaji mzuri kutoka AC Milan, Bayern Munich na hata Real Madrid. Hii inasababisha hata timu za maeneo ya kati kutoa upinzani wa kweli na si wa kubabaisha.
Staili moja ya soka
Siku zote Guardiola ana staili moja tu ya soka. Staili ya soka la pasi nyingi na kumpa presha adui. Staili hii ilifanya kazi Barcelona kwa sababu ni staili ambayo imekuwepo klabuni hapo kwa miaka 20 nyuma. Staili hii haikufanya kazi sana Bayern Munich kwa sababu kwa Wajerumani siyo staili yao. Ni ngumu kwa staili hii kufanya kazi kwa Manchester City. Kwanza klabu za Uingereza hazichezi mpira wa kufunguka lakini vile vile zina ubavu mkubwa wa kujihami na kufanya mashambulizi ya haraka haraka. Pili waamuzi wengi wa Uingereza wanaruhusu soka la rafu na hivyo kuharibu mara kwa mara soka la kumiliki mpira. Kuna wachezaji wengi majeruhi katika soka la Kiingereza na kama Guardiola anadhani akiwa Bayern Munich alipata majeruhi wengi, basi asubiri Uingereza.
City inahitaji timu mpya
Guardiola anakwenda katika timu mpya huku akihitajika kuunda kikosi kipya kabisa. Wachezaji wengi wa Manchester City ni wazee na wastani wa umri wao ni miaka 29.2. Ukimtazama Yaya Toure ana miaka 32, David Silva ana miaka 30, Vincent Kompany ana miaka 29 na wengineo miaka imepanda. Guardiola anakabiliwa na kazi mbili. Kwanza ni kuunda timu mpya, lakini hapo hapo akishinda mataji. Ingawa Guardiola atakuwa na pesa nyingi lakini wakati mwingine pesa si kila kitu. Atahitaji muda kuwaunganisha wachezaji wake wapya, hasa kwa staili yake anayoipenda ya soka la pasi nyingi.
Hatapewa muda
Bahati mbaya kwa Guardiola ni kwamba ana jina kubwa katika kazi yake ya ukocha. Amechukuliwa kwa ajili ya mataji achilia mbali soka lake la kuvutia. Kuna makocha ambao wanapewa muda wa kufanya kazi zao lakini makocha kama Guardiola wanakuwa katika presha zaidi kwa sababu ya rekodi zao za nyuma. Makocha wengi wa timu zinazotumia sana huwa wanafukuzwa mapema. Kwa mfano, Manuel Pellegrini hakufukuzwa msimu uliopita kwa sababu matajiri wa Man City walikuwa wanasubiri Guardiola amalize mkataba wake Allianz Arena. Vinginevyo angekuwa ameshafukuzwa kwa kushindwa kuipa taji lolote Manchester City msimu uliopita. Matajiri wa City watatazamiwa kuwa kwa ukubwa wa jina la Guardiola ni lazima watachukua taji moja msimu ujao kati ya Ligi Kuu, FA au ubingwa wa Ulaya. Kama yakishindikana hayo bado kutaanza uvumi wa kufukuzwa kwake.