Gono na athari zake kwa wachezaji

Muktasari:
Imeelezwa kuwa kukosekana kwake uwanjani katika mechi za karibuni ikiwamo ile Jumanne ya UEFA dhidi ya Inter Milan ni kutokana na kiungo huyo toka nchini Brazil kuwa katika matibabu ya ugonjwa huo.
Kiungo wa klabu ya Barcelona ya nchini Hispania, Arthur Melo amekosa mechi kadhaa za wiki iliyopita na huku akijiandaa kukosa mechi ya El Clasico dhidi ya Real Madrid kutokana na kuugua ugonjwa wa gono.
Taarifa iliyotolewa na Andrea Ginola, mmoja wa viongozi wa klabu hiyo imeeleza sababu ya kukosekana kwa kiungo huyo mwenye miaka 23 katika mechi dhidi ya Mallorca ni kwa sababu ya ugonjwa huo unaonea kwa njia ya kujamiana na kitabibu ukijulikana kama sexual transmitted diseases (STD).
Ugonjwa huu wa zinaa ujulikanao kwa Kiswahili fasaha kama kisonono unaelezwa kumshabulia Melo na kumsababishia mitoki hali iliyosababisha kushindwa kushiriki mazoezi na mechi kadhaa.
Bacteria wajulikanao kitabibu kama Neisseria gonorrhoeae ndio husababisha kisonono (gonorrhea).
Imeelezwa kuwa kukosekana kwake uwanjani katika mechi za karibuni ikiwamo ile Jumanne ya UEFA dhidi ya Inter Milan ni kutokana na kiungo huyo toka nchini Brazil kuwa katika matibabu ya ugonjwa huo.
Kiungo huyo bado hajaonekana kuelewana vyema na kiungo mpya Frankie De Jong, inaelezwa hali yake hiyo imeleta gumzo sana mitandaoni watu wakishangaa staa kama yeye kapataje tatizo hilo.
Basi leo tutalitupia macho tatizo hilo ambalo wengi wanalijua maarufu kama “Gono” ili kuweza kupata ufahamu wake.
Gono ni nini?
Gono ni kifupisho cha Gonorrhea kwa kitabibu ambayo kwa Kiswahili ni kisonono. Ni ugonjwa unaonea kwa kujamiana na mtu mwenye maambukizi na huwapata wanawake na wanaume.
Kwa mwanaume kama Melo ni kutokana na kujamiiana na mwanamke bila kinga ambaye ana maambukizi ya gono.
Ugonjwa huu kwa mwanaume huambatana na hali ya maumivu katika maeneo ya uzazi na endapo hatua za matibabu zisipochukuliwa mwanaume anaweza kuwa mgumba.
Habari njema ni kuwa tatizo hili linaweza kutibika bila tatizo lolote na mgonjwa hupona na kuendelea na majukumu yake kama kawaida.
Ugonjwa huu unaenea kutoka mtu mmoja kwenda mwingine kwa kujamiana kwa njia ya uke/uume, haja kubwa na njia ya mdomo.
Unawezaje kupunguza hatari ya kupata gono?
Njia ya kuepukana na tatizo hilo pamoja na magonjwa mengine yanayoenea kwa njia ya kujamiana (STD) ni kuepukana kujaamiana bila kinga.
Kuwa na mpenzi mmoja mwaminifu ambaye amepima na kuonekana kutokuwa na magonjwa haya ya STD. Ikumbukwe kuwa watu wenye wapenzi wengi ndio wako katika hatari ya kupata tatizo hili.
Vilevile ni vizuri kumpeleka mwenza wako au wenza wako ambao ulijamiiana nao bila kinga katika huduma za afya ili waweze kutibiwa tatizo hilo.
Dalili za gono zikoje?
Wapo baadhi ya watu wanaweza kuwa na maambukizi ya gono lakini wasiwe na dalili zozote hasa wanawake kwani wana uwezo wa kutoa hifadhi ya maambukizi kwa miezi hata sita bila kuonyesha dalili.
Lakini mara tu mwanamke huyo mwenye maambukizi anapojamiiana bila kinga na mwanaume huchukua saa 24-72 kuonyesha dalili hizo.
Mwanaume anaweza kupata dalili hizo kesho yake tu anapoamka kwa kuhisi hisia za kuungua au kukereketa katika njia ya mkojo, kuona uchafu mweupe au njano au kijani ukitoka katika tundu ka uume.
Dalili hii hii hufanana na maziwamaziwa ambayo hunasana na nguo ya ndani. Dalili hii imepata msemo maarufu kwa kuisema kuwa “leo nimemka nakamua dawa ya mswaki” hii ni kutokana na mfanano wa uchafu huo.
Dalili nyingine ni kupata maumivu katika kende na wakati wa kukojoa, pia kuvimba mitoki ambayo huambatana na maumivu.
Dalili nyingine anazoweza kupata mwanaume ni pamoja na kupata hali ya uchovu na homa.
Uchunguzi na matibabu
Kwa kawaida tatizo hili linaweza kubainika kwa daktari kupata historia nzima ya dalili na uchunguzi wa kimwili.
Sampuli ya mkojo inaweza kuchukuliwa na kufanyiwa uchunguzi wa kina wa kimaabara.
Pale mgonjwa anapobainika kuwa na maambukizi dawa za matibabu za ‘antibaotiki’ ambazo zina mwongozo wake maalumu huweza kutumika kutibu.
Ni kawaida pia sampuli ya uchafu kufanyiwa kupimo cha upandikizaji ili kubaini aina ya vimelea wa gono na ‘antibaotiki’ sahihi inayowaua wadudu.
Dawa hiyo itahitajika kuwatibu wenza wote wawili ili kuzuia kuenea kwa maambukizi haya.
Ni kawaida kutokea kwa vidudu vya gono kuwa sugu na kutoa upinzani kwa dawa za matibabu, ndiyo maana inashauriwa kutumia dawa hizo kama daktari alivyoelekeza.
Inashauriwa kuepuka kujamiiana kabla ya kupona na ni angalau baada ya wiki mbili ndipo mtu anaweza kuanza maisha ya kujamiiana kama kawaida.
Wenza wanatakiwa kutumia dawa kwanza na kuepuka kujamiiana katika kipindi cha matibabu.
Ikumbukwe kama mwenza wa kike hatapata matibabu maambukizi hayo yanaweza kumsababishia ugumba kutokana na mashambulizi ya vimelea hivyo katika nyumba ya uzazi na mirija ya uzazi.
Endapo mwanaume asipotibiwa anaweza kupata shambulizi katika mirija ya mbegu za uzazi hali inayoweza kumletea ugumba, hivyo kushindwa kupata mtoto.
Hivyo ni muhimu sana kwa wenza wote kufika mapema katika huduma za afya kupata matibabu na kushikamana na matibabu na ushauri wa watoa huduma za afya.
Hapa nchini zipo huduma maalumu kwa ajili magonjwa ya STD na ngozi na dawa zake za matibabu hutolewa bure katika vituo vya afya vya serikali.
Matumizi ya kinga, yaani mipira ya kiume (condoms) yanahimizwa kwani siyo tu yanasaidia kinga dhidi ya STD, bali pia hupunguza hatari ya kupata maambukizi ya VVU.
Pamoja na wadau mbalimbali kushangaa Melo kupata ugonjwa huo, lakini kwa upande mwingine kuwa maarufu na kipato kikubwa kwa wanasoka kunawafanya kuwa katika hatari ya kujiingiza katika mahusiano yasiyo rasmi na wapenzi tofauti.
Hatua mbalimbali za matibabu zimechukuliwa kwa Melo ikiwamo kumfanyia ushauri nasaha na kuelimishwa juu ya STD.
Kwa sasa Melo anaendelea vizuri na matibabu chini ya jopo la madaktari wa Barcelona na anatarajiwa kuwa fiti baada ya wiki ijayo.