Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Giovani Lo Celso fundi wa kiargentina aliyetua Spurs kumpa raha Pochettinho

Muktasari:

Wakati tayari Ndombele akiwa ameanza makali yake kwa kufunga bao, macho na masikio yamehamia kwa LO Celso ambaye aliingia katika pambano dhidi ya Newcastle wikiendi iliyopita. Ni nani huyu Lo Celsco?

LONDON, ENGLAND.KOCHA wa Tottenham, Mauricio Pochettino ameongeza mafundi wawili katika benki ya eneo la kiungo.

Baada ya kukaa madirisha mawili bila ya kununua mastaa, hatimaye amewanunua viungo Tanguy Ndombele kutoka Lyon na Giovani Lo Celso.

Wakati tayari Ndombele akiwa ameanza makali yake kwa kufunga bao, macho na masikio yamehamia kwa LO Celso ambaye aliingia katika pambano dhidi ya Newcastle wikiendi iliyopita. Ni nani huyu Lo Celsco?

Azaliwa mji mmoja na Messi

Jina lake kamili ni Giovani Lo Celso na alizaliwa April 9, 1996 katika mji wa Rosario nchini Argentina. Rosario ni mji waliozaliwa mastaa wawili wa soka la Argentina, Lionel Messi wa Barcelona na Angel Di Maria wa PSG.

Lo Celso alianza kucheza soka katika klabu ya vijana ya Roasio Central ambayo pia Di Maria alichezea udogoni. Baadaye akapanda hadi kikosi cha wakubwa ambapo alicheza pambano lake la kwanza mnamo Julai 19, 2015 dhidi ya Vélez Sarsfield pambano lililomalizika kwa suluhu ya bila kufungana.

Aliifungia Rosario Central bao la kwanza katika pambano dhidi ya Colon wakishinda mabao 3-0 mnamo Februari 28, 2016. Alifunga bao hilo katika dakika ya sita tu. Alifunga bao lake la pili katika kichapo cha mabao 3-2 dhidi ya Vélez Sarsfield mnamo April 10,l 2016.

Atua PSG

Julai 26, 2016 Lo Celso alijiunga na mabingwa wa Ufaransa, PSG kwa dau la Pauni 8.5 milioni huku klabu hiyo ikimpatia Lo Celso mkataba wa miaka mitano mpaka mwaka 2021. Hata hivyo kipengele cha mkataba kilimruhusu abakie klabuni Rosario kwa mkopo hapo mpaka Desemba 31, 2016.

Aliichezea PSG mechi ya kwanza mnamo April 5, 2017 katika pambano la robo fainali kombe la Ufaransa dhidi ya US Avranches. Katika pambano hilo aliingia uwanjani kuchukua nafasi ya kiungo wa Ufaransa, Adrien Rabiot dakika ya 63 wakishinda mabao 4–0 ugenini.

Lo Celso pia aliingia uwanjani katika pambano la Ligi ya mabingwa wa Ulaya dhidi ya Celtic na kupika bao la mlinzi wa kimataifa wa Brazil, Dani Alves katika ushindi wa mabao 7-1. Alifunga bao lake la kwanza kwa PSG katika ushindi wa mabao 3-2 dhidi ya Rennes mnamo Januari 30, 2018 ikiwa ni katika kombe la Ligi.

Mei 8, 2018 alifunga bao jingine kwa PSG katika ushindi wa mabao 2-0 dhidi ya Les Herbiers VF na hivyo kutwaa ubingwa wa kombe la Ufaransa msimu wa 2017–18.

Atinga Real Betis, atamba

Kutokana na kusheheni kwa mastaa wa eneo la kiungo PSG, Lo Celso alitimkia klabu ya Real Betis ya Hispania Agosti 31, 2018 kwa mkopo wa msimu mzima huku klabu hiyo ikipewa nafasi ya kumnunua jumla kama ingeridhika na kiwango chake kufikia mwishoni mwa msimu.

April 16, 2019 Betis waliamua kumchukua jumla Lo Celso na hadi kufikia mwishoni mwa msimu uliopita alikuwa mmoja kati ya mastaa wa timu hiyo ambapo alifunga mabao 17 baada ya kucheza mechi 46 za michuano mbalimbali..

Tottenham Hotspur yamnasa kwa mkopo

Agosti 8, 2019, Lo Celso alisaini Tottenham kwa mkataba wa mkopo wa msimu mzima huku wakipewa nafasi ya kumchukua jumla mwishoni mwa msimu. Hii ilitokana na uvumi mwingi uliozunguka hatima yake katika dirisha hili.

Alicheza mechi yake ya kwanza kwa Tottenham wikiendi ya pili ya Ligi Kuu ya England akiingia kipindi cha pili katika pambano dhidi ya Manchester City ambalo linakumbukwa kwa utata wa matumizi ya VAR. akaingia tena katka pambano dhidi ya Newcastle United.

Atingia jezi ya Argentina

Kutokana na kiwango chake kizuri akiwa na Rosario Central, Lo Celso alifanikiwa kuitwa katika kikosi cha Argentina chini ya umri wa miaka 23 ambacho kilishiriki katika michuano ya Olimpiki mwaka 2016. Agosti 4, 2016, Lo Celso aliichezea Argentina chini ya umri wa miaka 23 katika kichapo cha mabao 2-0 dhidi ya Ureno akichukua nafasi ya Cristian Espinoza dakika ya 72.

Novemba 11, 2017, Lo Celso aliichezea Argentina ya wakubwa mechi ya kwanza katika pambano dhidi ya Russia ambalo walishinda 1-0. Katika mechi hiyo alianza na kucheza dakika 59 kabla ya nafasi yake kuchukuliwa na Alejandro Gómez.

Mei 2018, Lo Celso ambaye ana pasipoti ya Italia pia kutokana na kuwa na asili ya nchi hiyo alitwa katika kikosi cha awali cha Argentina cha mastaa 35 ambao wangechukuliwa baadhi na kuwaikilisha nchi hiyo katika kombe la dunia Russia 2018. Baadaye akabakia katika orodha ya wachezaji 23.

Mei 2019, Lo Celso alijumuishwa katika kikosi cha wachezaji 23 wa kocha, Lionel Scaloni ambalo wangeshiriki michuano ya Copa Amerika nchini Brazil.

Juni 28 katika pambano la robo fainali dhidi ya Venezuela alifunga bao la pili katika ushindi wa mabao 2-0. Kwa ushindi huo Argentina walikwenda nusu fainali na kutolewa na wenyeji Brazil.