Gets Program yaungana na Mlandizi

Muktasari:
- Imesalia mechi moja ya kumaliza msimu wa 2024/25 na Gets imeshuka rasmi baada ya kushinda mechi mbili.
HATIMAYE Gets Program imeungana na Mlandizi Queens kushuka daraja Ligi Kuu ya Wanawake baada ya kukusanya pointi 10 kwenye mechi 17.
Imesalia mechi moja ya kumaliza msimu wa 2024/25 na Gets imeshuka rasmi baada ya kushinda mechi mbili.
Kwenye mechi 17 imetoa sare nne na kupoteza 11 ikifunga mabao 11 na kuruhusu 46.
Timu zote mbili zilipanda daraja msimu huu na sasa zote zimerudi zilipotoka na sasa zitashiriki Ligi daraja la kwanza.
Akizungumza na Mwanaspoti, Kocha wa timu hiyo, Aristides Ngowi alisema changamoto kubwa iliyowaangusha msimu huu ni pamoja na kukosa muda wa maandalizi pamoja na usajili.
"Tumekuwa na changamoto nyingi, ishu ya usajili wachezaji wengi hawakuwa na vibali hilo limetuvuruga sana kwa sababu kuna wachezaji wengine hatukuwatumia kabisa," alisema na kuongeza
"Lakini pia changamoto ya kifedha iliyosababisha baadhi ya wachezaji kukimbia na kutafuta pesa za kujikimu kama kocha unapanga programu zako lakini kama huwatumii wachezaji inachanganya kwa kiasi fulani."