Friends of Simba wamchangia kocha Kisaka
Wanachama wa Friends of Simba wakiwa Hospitali ya Burhani na aliyekuwa kocha wa makipa wa Simba, James Kisaka ambaye amelazwa katika hospitali hiyo. Anayesalimiana na Kisaka ni kiongozi wa kundi hilo, Evance Aveva. Wanachama hao walimpa Kisaka Sh 2.5 kwa ajili ya matibabu.
Muktasari:
Mwili wa kocha huyo ambaye ni kipenzi cha wengi hauna nguvu,anainuka kwa msaada wa kaka yake anayeitwa, Michael Kisaka ambaye ndiye anayemuuguza.
KUNDI la Friends of Simba juzi Jumamosi walikwenda Hospitali ya Burhan kumjulia hali aliyekuwa kipa na kocha wa makipa wa Simba, James Kisaka na kumpa Sh 2.5 Milioni.
Friends of Simba walimpa, Kisaka pesa hizo kwa ajili ya kumsaidia gharama za matibabu.
Kisaka ambaye alianza kupata matatizo kabla ya mzunguko wa kwanza kumalizika, jicho moja lilifumba na mwili kukosa nguvu na miguu kuwa kama imepooza.
Mwanaspoti ilifika kwenye hospitali hiyo iliyopo Mtaa wa India, Dar es Salaam na kuonana na Kisaka ambaye hata kumtambua mwandishi wa habari hizi ambaye ni rafiki yake wa siku nyingi ilikuwa tabu kwani anaona kwa shida.
Kiongozi wa Friends, Evance Aveva aliyemkabidhi pesa hizo, aliulizwa mara mbilimbili wewe nani na alipojitambulisha ndipo akapata kumbukumbu kwa mbali akaomba msaada wa kunyanyuliwa na kuzungumza kwa taabu.
Mwili wa kocha huyo ambaye ni kipenzi cha wengi hauna nguvu, anainuka kwa msaada wa kaka yake anayeitwa, Michael Kisaka ambaye ndiye anayemuuguza.
Akizungumza kwa tabu, Kisaka alisema: “Nashukuru viongozi kwa msaada wenu, ninapoona hivi nafarijika na kuona kuwa nyuma yangu kuna watu wanaonijali. Hali yangu kiafya ndiyo kama hivi mnavyoona, lakini nashukuru naendelea vizuri na naamini Mungu atanijalia afya yangu itarudia.”
Aveva ambaye aliongozana na viongozi wengine wa Friends of Simba ambao ni Miki Magarinzo, Mlamu Ngambi na David. Kwa niaba yao, Aveva alisema: “Tumeona kumjulia hali, Kisaka kama unavyojua ni mwenzetu tumekuwa naye kipindi kirefu, na tumempa kiasi hiki kidogo kwa ajili ya kumsaidia gharama za matibabu.”