FIFA yamfungia maisha bosi wa soka Ghana
Muktasari:
Shirikisho la soka la kimataifa (Fifa), limemfungia maisha aliyekuwa bosi wa Chama cha soka nchini Ghana ambaye pia alikuwa makamu wa Rais wa Shirikisho la soka barani Afrika (Caf) Kwesi Nyantakyi, aliyekumbwa na kashfa ya kuomba na kupokea rushwa pamoja na mambo ya ufisadi.
Zurich, Uswisi. Shirikisho la soka la kimataifa (Fifa), limemfungia maisha kujihusisha na masuala yote yanayohusiana na soka Rais wa zamani wa Chama cha Soka nchini Ghana (GFA), Kwesi Nyantakyi.
Uamuzi huo umefanywa na Bodi ya soka ya Fifa, iliyoketi juzi baada ya kupitia ripoti iliyomtia hatiani kwa makosa ya rushwa an ufisadi.
Nyantakyi ambaye pia alikuwa makamu wa Rais wa Shirikisho la soka Afrika (Caf) alijiuzulu uongozi ndani ya nchi yake, Urais wa Umoja wa soka kwa nchi za Afrika Magharibi na ule wa Caf baada ya kukumbwa na kashfa hiyo.
Katika taarifa hiyo ya Fifa, Nyantakyi, anadaiwa kukiuka sheria za maadili ya uongozi kwa kuangalia maslahi binafsi badala ya yale ya soka kinyume na kanuni za maadili ya uongozi.
"Tunapenda kuwataarifu wadau wa soka duniani kote kuwa,Nyantakyi, amefungiwa kujihusisha na masuala ya soka kwa maisha yake yote, katika nyanja za kitaifa na kimataifa,” ilisema taarifa hiyo.
Pamoja na kufungiwa pia shirikisho hilo limemtoza faini ya faranga za Uswisi 500,000 ambazo anatakiwa kuzilipa mara moja kinyume cha hivyo atafikishwa mahakamani.
Nyatakyi alipokea rushwa kutoka kwa mwandishi wa habari Anas Aremeyaw Anas, ambaye alijadiliana naye kuhusu mambo kadhaa ikiwemo upangaji wa matokeo na kuhamisha fedha za udhamini za Chama cha soka Ghana.
Nyantakyi aliiongoza GFA kuanzia mwaka 2005 hadi Juni mwaka huu alipolazimika kujiuzulu baada ya uchunguzi wa kashfa hiyo kuanza kufanyiwa kazi.