Fei Toto awapiku Dube na Allan Okello Ligi Kuu Bara
Muktasari:
- Katika mechi hiyo Azam iliyoshinda 3-0, Fei Toto alichangia mabao matatu baada ya kufunga mawili dakika ya 9 na 58 na kuasisti pia lingine moja, lililofungwa na mshambuliaji nyota wa timu hiyo, Mkongomani Jephte Kitambala, dakika ya 20.
MABAO mawili ya Ligi Kuu Bara aliyofunga kiungo mshambuliaji nyota wa Azam FC, Feisal Salum 'Fei Toto' juzi dhidi Mtibwa Sugar, kwenye Uwanja wa KMC Complex, Mwenge, Dar es Salaam, yamemfanya kufikia rekodi yake aliyoweka msimu wa 2024-2025.
Katika mechi hiyo Azam iliyoshinda 3-0, Fei Toto alichangia mabao matatu baada ya kufunga mawili dakika ya 9 na 58 na kuasisti pia lingine moja, lililofungwa na mshambuliaji nyota wa timu hiyo, Mkongomani Jephte Kitambala, dakika ya 20.
Mabao hayo mawili aliyofunga kiungo huyo, yamemfanya kufikisha tisa hadi sasa msimu huu akiongoza na kuwapiku, Prince Dube wa Yanga na Mkongomani Fabrice Ngoy wa Namungo FC 'Wauaji wa Kusini', ambao kila mmoja wao amefunga mabao manane.
Mbali na kuongoza kwa kufunga, ila kiungo huyo mshambuliaji anaongoza pia kutengeneza nafasi nyingi za mabao kwa maana ya kuasisti, akiwa na nane akiwapiku, Allan Okello wa Yanga mwenye sita na Elie Mpanzu kutoka Simba aliyeasisti matano.
Kwa maana hiyo, Fei Toto amehusika katika mabao 17 ya Ligi Kuu Bara na kikosi hicho cha Azam FC, sawa na aliyoweka msimu wa 2024-2025, alipofunga manne na kuasisti 13, akiwa ndiye aliyeongoza, akihitaji kwa sasa bao moja kuweka rekodi mpya.
Fei Toto ndiye mchezaji aliyefanya vizuri zaidi kwa mwaka 2024 na alichangia mabao 27 ya Ligi Kuu Bara, baada ya kufunga 15 na kuasisti 12, akimzidi, Stephane Aziz KI, aliyekuwa Yanga, ambaye alichangia 21, akifunga 12 na kuasisti pia tisa.
Mwaka 2024, Fei Toto aliongoza kwa nyota waliochangia mabao mengi, akifuatiwa na Stephane Aziz KI aliyekuwa Yanga ambaye kwa sasa anaichezea Al-Ittihad SC ya Libya, ambapo hadi anaondoka alichangia 21, baada ya kufunga 12 na kuasisti tisa.
Kiwango bora cha Fei Toto, kilimfanya kumaliza na mabao 19 ya Ligi Kuu Bara kwa msimu wa 2023-2024, akiwa ndiye mchezaji mzawa aliyeshika nafasi ya kwanza kwa kufunga mabao mengi zaidi, nyuma ya Aziz KI, aliyekuwa Yanga, aliyefunga mabao 21.
Pia, alikuwa mchezaji bora wa Kombe la Shirikisho (FA), msimu wa 2023-2024, kwa kuifikisha Azam fainali na kuchapwa na Yanga kwa penalti 6-5, baada ya suluhu (0-0) ya dakika 120, kwenye Uwanja wa New Amaan Complex, Zanzibar, Juni 2, 2024.
Kiwango hicho kizuri anachokionyesha kiungo huyo mshambuliaji, ndicho kilichowafanya mabwenyenye wa Al Ahli Tripoli ya Libya kumwekea Sh4.5 bilioni, ili kumsajili tangu msimu wa 2025-2026, umeanza, japo Azam FC ilimuwekea ngumu kumwachia.