Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

EXCLUSIVE 2: Nabi afunguka dili la Bangala, Diarra

Baada ya kuona sehemu ya kwanza aliyekuwa kocha wa Yanga, Nabi Mohammed leo anaanza kuelezea hatua yake ya kuondoka klabuni; 

"Niweke wazi hapa watu wajue nimeona wapo ambao wanadhani mimi uamuzi wangu wa kuondoka Yanga sasa umetokana na tamaa ya fedha na wapo wengine wamekuwa wanamshambulia mwanangu Hedi wakidhani ujio wake hapa ndio amekuja kushinikiza kuondoka haya sio kweli.

"Nakumbuka wakati tunakwenda kucheza na TP Mazembe, Ofisa Mtendaji wa Yanga, Andre Mtine alinifuata na kunipa habari njema za kamati ya utendaji imeridhia niongezwe mkataba mpya palepale nilimwambia bosi wangu kuwa wasubiri kwa kuwa tayari nilishakuwa na hesabu tofauti juu ya hilo na nilimueleza."

"Baadaye hata mfadhili wa klabu Ghalib (Said Mohamed) alipa taarifa kwamba nimekuwa na mawazo tofauti, wakati narudi nyumbani kwenda kufuatilia hati yangu mpya ya kusafiria, aliniomba niende kuzungumza na familia juu ya kubadili mtazamo wangu.

"Lakini bado niliona ni wakati muafaka sasa hata kama sina timu ni vyema kwenda kupumzika. Ukweli ni kwamba baada ya hii miaka miwili akili yangu ilikuwa inaniambia kwamba timu inahitaji kupitia mabadiliko makubwa ya kuingiza damu mpya ambayo itakuja kuendeleza safari ya hapa tulipofikia.

"Tulipofika fainali ya Shirikisho hili liliongezeka unajua kila unapofikia mafanikio fulani lazima watu watahitaji kuona tunafika mbali zaidi, mimi sio kocha ninayetanguliza fedha mbele, kama ningekuwa hivyo nisingekuja hapa Yanga kwani kuna ofa nyingi nilizipata kabla lakini bado nikaja kufanya kazi hapa kwa miaka miwili na nusu.

"Hata wakati nikiwa hapa bado zilikuja ofa nyingi kubwa kutoka DR Congo, Afrika Kaskazini, Afrika Kusini  lakini sikutanguliza tamaa ya fedha kwangu mimi kitu muhimu kwa timu nitakayofanya nayo kazi ni kuona projekti nzuri kutoka kwa uongozi na sio fedha, hii ni mara ya pili mwanangu anakuja hapa nchini hasa ligi inapokaribia kumalizika, Hedi anaipenda sana Yanga ni mwanafunzi kule Ubelgiji lakini anapopata muda wa likizo kama hivi huwa anakuja huku Tanzania aone mechi za Yanga kwa macho yake.

"Ana upeo mkubwa wa kuchambua soka lakini hajahusika kunishawishi kuachana na Yanga na aliumia sana siku ambayo nilimwambia naondoka hapa, huu mkataba ambao umemalizika ni mimi nilizungumza na uongozi kuanzia mwanzo mpaka nikasaini hakuna sehemu ambayo alihusika Hedi  nawaomba watu wa Yanga wasimshambulie kwenye mitandao ni sawa kama wananikosea mimi kupitia mwanangu  haya ni maamuzi yangu binafsi ambayo nayafanya baada ya kuhakikisha kila kizuri kilipatikana kwa klabu hii ninayoipenda, nakiri klabu ilitaka kunibakisha hapa ila aya ni maamuzi yangu asilaumiwe mtu mwingine."


MADILI YA KINA BANGALA

"Baada ya kuiona timu kwenye miezi sita ya kwanza nilijua kipi kinahitajika na kiukweli niwapongeze viongozi kunisikiliza kwa kiasi kikubwa ulipokuwa unafika wakati wa usajili.

"Ukiniuliza usajili gani bora ni wengi tulifanya vizuri lakini wale ambao walikuwa bora zaidi katika kuchagua kwangu ni tulipowaleta Fiston Mayele, Bangala (Yannick), Djigui Diarra, Mudathir ambaye wakati nawaambia viongozi tumchukue ilikuwa ni hatari kwa kuwa changamoto kubwa alikuwa amekaa nje kwa miezi sita lakini alipoingia Mungu alimsaidia akaanza vizuri na kiukweli alionyesha kuwa ni mchezaji bora.

"Hawa wachezaji kutoka Congo wengi nilikuwa nawafahamu kabla tangu nilipokuwa nafanya kazi Motema Pembe na walipounganika na wengine tulipata timu imara ambayo ilichanganyika na wengine kama kina Aucho (Khalid), Mwamnyeto (Bakari), Job (Dickson), Feisal (Salum), Kibwana (Shomari), Djuma (Shaban) na wengine wote.


USAJILI WA DIARRA

"Ngoja leo nisimulie kitu ambacho wengi hawajui, wakati tulipokuwa tunatafuta kipa mpya tulipata kipa mmoja kutoka Ivory Coast, ambaye sasa yupo TP Mazembe, Hersi alishakamilisha karibu kila kitu.

"Ghafla baadaye Mshindo Msolla(Mwenyekiti wa Yanga wakati huo)alikuja na video za Diara kwangu nikaangalia na kuona kweli ni kipa bora, nilifanya mawasiliano na rafiki zangu waliopo Mali wakaniambia nikweli ubora ambao nauona kwenye video ndio ubora halisi wa kipa huyo mpaka sasa hapohapo nilikimbia haraka kwa Hersi nikamuuliza wamefikia wapi kwenye usajili wa yule kipa wa kwanza bahati nzuri walikuwa bado hawajamalizana.

"Nikamuomba sana wamchukue Diara na yeye alipoangalia akakubaliana nasi, ndio tukampata Diara unajua Diara nilimtaka sana kutokana ni kipa ambaye ubora wake unaendana na falsafa zangu, nilikuwa nataka kipa ambaye anajua kumiliki mpira vizuri na kuanzisha mashambulizi, makipa bora wengi sasa duniani ni wale ambao miguuni wanajua kuuchezea mpira."


WACHEZAJI KUKAA KAMBINI

"Wakati nafika hapa nilikuta utaratibu wa wachezaji kukaa muda mrefu kambini,uamuzi huo uliwafanya wachezaji kukosa muda mrefu wa kukaa na familia zao, ratiba hii ilitupa changamoto nyingi za utovu wa matukio ya utovu wa nidhamu kwa wachezaji, kulikuwa na mambo ya kutoroka kambini, au kuchelewa kuja kambini na mengine mengi kama ambavyo mnawajua wachezaji.

"Nikakutana na uongozi wa klabu nikawapa mtazamo wangu wa namna ambavyo tunaweza kufanya mabadiliko ya timu kukaa kambini ili kusudi kupunguza makosa ya kinidhamu lakini pia kuongeza ufanisi wa wachezaji na timu kwa ujumla, unajua maisha sio tu mpira peke yake, ili wachezaji wawe bora tunahitaji kuweka mizania sawa kati ya kujituma kazini na kuwa karibu na familia zao, uongozi walielewa ushauri wangu na wakakubaliana na mimi.

"Tukasema muda wa wachezaji kukaa kambini iwe siku tatu kabla ya kucheza mechi, uamuzi huu ulileta faida kubwa kwa timu yetu, wachezaji walifurahi na waliheshimu, walipokuja kambini walijituma sana ili kuhakikisha hawaharibu nafasi ambayo tumewapa.

"Unajua haikuwa rahisi sana kueleweka kwenye hili nafahamu pia hata viongozi kwao walinielewa lakini unajua kunja wakati presha kubwa kwao inatoka kwa mashabiki na wanachama nje hasa wanapowaona wachezaji muda mwingi wako mitaani, maamuzi haya yaliongeza ari ya ushindi kwenye timu, nafahamu bado kuna changamoto kwa wachezaji wa Afrika katika kujiheshimu lakini ulaya wachezaji wanaingia kambini siku moja kabla ya mechi.

"Tulichofanya ni kwamba kila siku wanakuja mazoezini na kurudi makwao lakini siku tatu kabla ya mechi hapo tunaingia kambini kujiandaa kikamilifu, ilikuwa ngumu kueleweka na kukubalika lakini niwashukuru viongozi lakini kwa nafasi kubwa tuliondoa changamoto za kutatua makosa ya kinidhamu kwa wachezaji."


UBORA YANGA ULIANZIA MAZOEZINI

"Tulikuwa tunafanya kazi kubwa kwenye uwanja wa mazoezi, najua kuna wakati mashabiki walikuwa wanasumbuka wanapoona mchezaji wanayemtaka hachezi lakini kwetu tulikuwa tunajua kwanini hachezi, mazoezini tulitaka kuona kila mchezaji anakuwa bora.

"Sijawahi kupanga timu kutokana na jina la mchezaji, ilikuwa tunaongea ubora wao lakini tukiona hana juhudi hakukuwa na chaguo lingine zaidi ya kukaa benchi, kila walipokuwa wanaona wachezaji wanaoanza kwenye mechi basi watambue kwamba hao ndio waliokuwa bora mazoezini na ndio maana hakukuwa na kelele kwa wachezaji wenyewe kwamba labda kuna upendeleo.

"Changamoto moja ambayo ilikuwa tunakabiliana nayo ni kutokuwa na uwiano bora wa baadhi ya nafasi hili ndio manaa mliona tunaweza kumchukua Kibwana kutoka beki wa kulia tunampeleka kushoto msingi wa mabadiliko haya ulikuwa ni kuona kama tunacheza na timu yenye watu bora wa kushambulia kutokea pembeni na tutamweka Kibwana labda tukiona Lomalisa (Joyce) hawezi kutusaidia kukaba vizuri.

"Hivyo hivyo tukiona kama tunahitaji beki anayeshambulia kwa nguvu basi tutamtumia Lomalisa kuja kutufanyia kazi, hata hili nalo halikuwa rahisi kukubalika kwa wachezaji lakini mwisho wa siku mimi ndiye kocha na nina wasaidizi wangu tukikubaliana hivyo basi hilo litafanyika bila kuangalia nani amefurahi au nani anachukia tulichotaka ni kufikia malengo kwa kushinda.