Emery awachunia mastaa wake
Muktasari:
Kipigo hicho kimemuuma sana Emery na kubwa zaidi ni kwamba amepoteza fursa ya kucheza Ligi ya Mabingwa Ulaya msimu ujao, ikiwa ni msimu wa tatu mfululizo.
BAKU, AZERBAIJAN.ASIKWAMBIE mtu, kufungwa kunauma. Tena kufungwa kwenye fainali? Muulize Unai Emery atakwambia.
Unajua kwa nini? Kocha huyo Mhispaniola amewanunia wachezaji wake wote wa Arsenal baada ya kuchapwa kwenye fainali ya Europa League na Chelsea juzi Jumatano.
Emery ameamua kuchagua jambo moja tu, kuwanunia wachezaji wake, hakuzungumza na yeyote kwenye vyumba vya kubadilishia nguo huko mjini Baku, Azerbaijan baada ya fainali hiyo iliyomalizika kwa kikosi chake kuchapwa 4-1.
Kipigo hicho kimemuuma sana Emery na kubwa zaidi ni kwamba amepoteza fursa ya kucheza Ligi ya Mabingwa Ulaya msimu ujao, ikiwa ni msimu wa tatu mfululizo.
Kiungo Granit Xhaka ndiyo mchezaji pekee wa Arsenal aliyezungumza na waandishi wa bahari baada ya mechi hiyo. Wengine wote kila mmoja alikuwa akiuguza maumivu ikiwamo kocha wao ambaye aliamua kuwachunia kabisa wachezaji wake.
Xhaka aliulizwa kama kocha amesema kitu baada ya fainali hiyo, alijibu: “Hakuna kitu.”
Alipoulizwa kwanini, Xhaka alijibu: “Sifahamu. Bila shaka atakuwa amehuzunika. Kocha, wachezaji hakuna aliyezungumza na mwenzake kwenye vyumba vya kubadilishia.”
Xhaka mwenyewe alichukia baada ya mwandishi kumuuliza kama wameamua kuwaangusha kwa makusudi wachezaji Petr Cech na Aaron Ramsey, ambao wanaoondoka kwenye timu hiyo.
Kwa dharau, kiungo huyo wa kimataifa wa Uswisi alijibu: “Umeuliza swali zuri sana. Ni swali zuri. Hivi unadhani tunaweza kufanya hivyo?”
Mwandishi alijibu: “Nimekuuliza swali.”
Kitu ambacho Xhaka alijibu kwa hasira: “Nimekuuliza wewe pia. Swali lako ni la kijinga, samahani sana. Tafadhali, siwezi kujibu upuuzi kama huo.”
Kiungo huyo mwenye mashuti makali akaulizwa kuhusu mipango yake ya baadaye kama ataachana na Arsenal na kujibu: “Mimi? Nina mkataba hapa.”
Kwa sababu Emery amekacha, Xhaka alikumbana na maswali magumu ikiwamo uwezo wa Arsenal kusajili wachezaji bora wakati hawapo kwenye mikikimikiki ya Ligi ya Mabingwa Ulaya. Kiungo huyo alijibu: “Sifahamu, sio uamuzi wangu kusajili wachezaji wakubwa au wachezaji wadogo.”
Arsenal ilikuwa na mpango kabambe kabisa katika kukifuma kikosi chake, lakini kutokana na kushindwa kuwamo kwenye Ligi ya Mabingwa Ulaya msimu ujao jambo hilo linaweka ugumu kwenye jitihada za kuwapata wachezaji inaowataka.
Hata hivyo, wenyewe wamepanga kupambana kuhakikisha wanasajili wale mastaa wanaowataka kwenye kikosi. Mmoja wa mastaa wanaotajwa kwamba huenda wakatua Emirates ni kiungo wa Barcelona, Andre Gomes.
Kiungo huyo alikuwa na msimu mzuri huko Everton alikocheza kwa mkopo akitokea Nou Camp.
Kukosa tiketi ya Ligi ya Mabingwa Ulaya jambo hilo linamfanya Kocha Emery kuwa na Pauni 40 milioni tu za kufanya usajili katika dirisha hili la majira ya kiangazi huko Ulaya. Arsenal ingepokea mkwanja wa Pauni 90 milioni kama ingefanikiwa kuichapa Chelsea, pesa ambayo ingeweka sawa bajeti yake ya usajili.
Kwenye dirisha hili la majira ya kiangazi, Arsenal imekuwa ikihusishwa na wachezaji wenye majina makubwa kama Gianluigi Donnarumma, Samuel Umtiti, Harry Maguire, Wilfried Zaha na Nicolas Pepe.
Lakini, sasa kocha huyo itabidi ahamie tu kwa wachezaji wa bei nafuu, kama vile beki wa Espanyol, Mario Hermoso, ambaye anaweza kumsajili kwa Pauni 18 milioni tu na winga wa Ajax, Hakim Ziyech, ambaye anaweza kupatikana kwa ada ya Pauni 25 milioni.
Ziyech amekuwa na kiwango bora msimu huu akifunga mabao 16 na kuasisti 13 kwenye ligi ya Eredivisie na kuipa Ajax ubingwa wa Uholanzi. Wachezaji hao wawili ndio ambao Arsenal inaweza kuwamudu kwa bajeti yao ya usajili, la kama itaongezeka kwa kuuza baadhi mastaa wao isiyowataka.