Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Dube atoa kauli tata, Dabo aingilia

STAA wa Azam FC, Prince Dube ametoa kauli tata kuhusiana na sakata lake la kutaka kuvunja mkataba na Azam FC
 
Raia huyo wa Zimbabwe aliandika barua juzi kwa Azam FC akiomba kusitishiwa mkataba huku akihusishwa na klabu za Yanga, Ihefu pamoja na Yadah na Highlanders za Zimbabwe.
 
Lakini Dube mwenyewe kwa mara ya kwanza amezungumza na Mwanaspoti kuhusiana na sakata hilo na kutoa kauli fupi yenye maswali tata, alipoulizwa juu ya sakata hilo na kwa kifupi alijibu: "Kuna mambo mengi hamuyajui, wakati ukifika mtayajua kwa sasa niacheni kwanza nitafakari."

Pamoja na kauli hiyo ya Dube inaonekana ameamua kurudisha majeshi nyuma akajipange upya baada ya kufanya kikao kirefu na kocha wake, Yousouph Dabo.

Sasa ni rasmi atarudi kundini kuelekea mechi za mwisho wa msimu. Dube anataka kusitishiwa mkataba wake na Azam, lakini akapewa masharti ya kulipa Dola 300,000 (takriban Sh700 milioni) ambazo zipo kwenye makubaliano ya mkataba  unaomalizika 2026.

Habari za uhakika ambazo Mwanaspoti inazo ni kwamba Dabo baada ya kusikia sekeseke hilo amemuita Dube mezani kutaka kujua kuna nini kinaendelea na baada ya majadiliano marefu kwenye ofisi ya kocha huyo katika Uwanja wa Azam Complex akakubali kurejea mzigoni na kuachana na ishu yake.

Dabo alipoulizwa na Mwanaspoti alijibu, "Dube bado ni mchezaji halali wa klabu (ya Azam) na ndio maana nikazungumza naye. Hayo mengine ni mambo ya ndani."

Katika barua yake, Dube ameomba avunjiwe mkataba, lakini asilipe kiasi kilichotajwa kwenye mkataba, bali arudishe pesa aliyopewa wakati anasaini mwaka jana ambayo ni Dola 200,000 (takriban Sh510 milioni).

Lakini, jibu alilokutana nalo mchezaji huyo ni kwamba hakuna mazungumzo mengine yoyote zaidi ya kufuata mkataba unavyotaka. Awali inadaiwa alitaka kutoa Dola 150,000 (takriban Sh382 milioni) kutoka kwa klabu inayomuwinda kimyakimya.

Habari zinasema kwamba Wakurugenzi walishakubaliana aondoke kutokana na kukerwa na 'kitrendi' chake cha kuandika barua ghafla bila kusema chochote.

Wakurugenzi hao walitoka na kauli moja kwamba Dube kaonyesha dharau na hakuna kingine zaidi ya kumruhusu aondoke ila kwa makubaliano ya kimkataba ambayo ni kulipa Dola 300,000.

Baada ya mazungumzo na Dabo, Dube atarudi kwenye timu na kuendelea kuitumikia, lakini kwa kifupi ni kwamba harakati zake zimekwama kwa sasa kutokana na mahitaji ya mkataba.

Lakini, kutoka vyanzo vya ndani ya klabu inayotajwa kuwa nyuma ya harakati hizo ni kwamba wao wako tayari kutoa nusu ya fedha zilizotajwa, lakini wanaogopa kujitokeza hadharani kwa sababu wataonekana walishafanya ushawishi.

Na kwa hilo, ndiyo maana walimtanguliza Dube mwenyewe mbele ili wamsaidie chinichini. Lakini harakati hizo zinaonekana kuwa ngumu ingawa lolote linaweza kutokea kuelekea mwisho wa msimu, huku Azam wakisisitiza kutokuwa na wasiwasi wowote.

Kuna sababu kubwa tatu mpaka nne zinatajwa za kuomba kuondoka ikiwemo Yanga, Ihefu na timu za Zimbabwe, lakini vyanzo vya kuaminika vinasema kuna kitu kinaendelea kimyakimya njiapanda ya Jangwani.


YANGA
Wanaamini Prince Dube anaweza kuwa mtu sahihi wa kuziba nafasi ya Fiston Mayele. Inaaminika Yanga wamekuwa wakihangaika kumshawishi mchezaji huyo kwa muda mrefu kutua katika kikosi hicho kutokana na uwezo wake.

Hivi karibuni wakati Azam FC ikiwa mikoani kwa mechi za Ligi Kuu, Dube alionekana kwenye Uwanja wa Benjamin Mkapa akishuhudia mechi ya Yanga ambapo ilishinda mabao 4-0 dhidi ya CR Belouizdad.
Dube hakusafiri na Azam kwa sababu ni majeruhi ambapo amekosa michezo kadhaa. Nyota huyo hajaichezea Azam tangu Februari 19 alipoingia kipindi cha pili dhidi ya Tabora United.
Hakusafiri na timu katika mechi mbili za mikoani - Mbeya dhidi ya Tanzania Prisons na Mwanza dhidi ya Singida Fountain Gate.

Lakini Mwanaspoti inajua kwa kawaida Azam FC husafiri na wachezaji wake hata kama ni majeruhi ikiwa ni sehemu ya kujenga umoja.

Hata hivyo, Dube hakusafiri ikisemekana alikataa kama sehemu ya shinikizo ili aachwe huru.
Habari za ndani ni kwamba inasemekana kuna mfanyakazi mmoja wa Yanga ambaye hapo kabla alikuwa Azam ndiye anayechora ramani ya kuhamia Jangwani na klabu hiyo ina uhakika kwamba ishu itakwenda kirahisi kwani ameshaanza ‘kuingia kwenye mfumo’.


IHEFU
Inaweza kuwa ajabu lakini bado ni kwa asilimia ndogo. Wamiliki wapya wa Ihefu wanataka kumnasa mchezaji huyo kwa gharama yoyote wakiamini atawasaidia kurahisisha safari ya mafanikio.
Kwa mujibu wa habari za ndani kutoka kwa watu wa karibu na Dube, mabosi wa Ihefu ambao zamani walikuwa wakiimiliki Klabu ya Singida United iliyopanda daraja mwaka 2017 walitaka kumsajili wakati ule sambamba na Tafadzwa Kutinyu.

Lakini Dube alichagua kwenda Afrika Kusini ambako hata hivyo hakufanikiwa na kuamua kurudi Zimbabwe.
Kinachoelezwa ni kwamba, kwa sasa wakiwa na timu mpya, mabosi wale wamerejea tena kwake na kuivuruga akili yake kwa ‘mzigo mrefu’ waliomuwekea mezani. Hata hivyo, Yanga bado imemuingia akilini zaidi.


NYUMBANI ZIMBABWE
Habari kutoka Zimbabwe zinasema timu mbili nchini humo zinapigana vikumbo kumrudisha kijana wao.
Mwanaspoti inaijua Highlanders FC, timu aliyokulia Dube ambayo kwa sasa ina wamiliki wapya wenye ‘mpunga mrefu’ wangependa kumrudisha nyota wao huyo kipenzi cha mashabiki.

Pia klabu ya Yadah FC ambayo hivi karibuni ilinasa saini ya nyota Khama Billiat iko katika harakati za kumnasa. Timu hizo mbili zinaitesa akili ya Dube, lakini Yanga wanazicheki tu.

Lakini, taarifa nyingine zinasema Dube anaamini majeraha yanayomuandama pale Chamazi yanatokana na mambo ya nje ya uwanja hivyo anataka kuondoka ili kujiepusha nayo.
Mchezaji huyo alijiunga na Azam FC 2020 akitokea Highlanders ya Zimbabwe - timu yake ya utotoni.
Aliyaanza maisha ya Chamazi kwa furaha kubwa kabla hajaumia kwenye mchezo dhidi ya Yanga, Novemba 25, 2020 na tangu hapo hakurudi kuwa Dube wa kabla ya kuumia.

Msimu huu pekee ameshakosa mechi zaidi ya tano kutokana na majeraha ambayo hadi sasa yanamuweka nje.
Hata hivyo, Mtendaji Mkuu wa Azam FC, Abdulkarim Amin ‘Popat’ amesema Dube ana mkataba nao hadi mwaka 2026 na unapaswa kuheshimiwa.
Hadi sasa nyota huyo amecheza dakika 734 katika dakika 1710 za mechi 19 ilizocheza Azam FC msimu huu. Dakika hizo ni katika mechi 12, huku akikosa mechi saba katika mechi 19 za msimu.

Kwa kifupi ni kwamba Dube amecheza chini ya nusu dakika za jumla kama angecheza mechi zote msimu huu na hii ni kutokana na pancha za hapa na pale ambazo zimekuwa zikimuandama katika misimu yote.

Katika dakika 734 za mechi 12 ambazo amecheza amefunga mabao saba na kutoa pasi mbili za mabao. Mkataba wa Dube na Azam FC unatarajiwa kumalizika ifikapo Juni 2026, ikiwa na maana kwamba bado ana misimu miwili na nusu mbele.