Dodoma Jiji yamkazia Medo kimtindo

Muktasari:

  • Medo anatajwa kwenda kuchukua nafasi ya Patrick Aussems 'Uchebe' baada ya mabosi wa Leopards kutofurahishwa na mwenendo wake.

TETESI za kocha mkuu wa Dodoma Jiji, Melis Medo kuhusishwa na klabu ya AFC Leopards ya Kenya zimezidi baada ya timu hiyo kutokuwa na matokeo mazuri.

Medo anatajwa kwenda kuchukua nafasi ya Patrick Aussems 'Uchebe' baada ya mabosi wa Leopards kutofurahishwa na mwenendo wake.

Mwanaspoti linafahamu kocha huyo yupo kwenye mazungumzo ya karibu na mabosi wa Leopards kwani sio mara ya kwanza kuhitaji huduma yake kwani ilishawahi kutokea wakati akifundisha nchini humo na klabu ya Wazito.

Leopards kwa sasa ipo nafasi ya saba kwenye msimamo wa Ligi kuu ikicheza mechi 31 huku ikijikusanyia pointi 48.
Mtu mmoja wa karibu na kocha huyo aliporafutwa na gazeti hili alisema;"Kweli kuna hizo taarifa baada ya mitandao mingi ya Kenya kuandika lakini kwa sasa kocha anaangalia zaidi kumaliza mechi za hapa."

Alipotafutwa Katibu Mkuu wa Dodoma Jiji, Fortunatus Johnson alisema ni habari ngeni kwake kwa sababu wasingeweza kutafutwa wao bali ni mhusika lakini watahakikisha kocha wao haondoki.

"Hizi taarifa ndio naziona hapa lakini sisi makocha wetu wanamaliza mikataba na tupo kwenye mazungumzo nao, tukielewana tutaendelea nao lakini tukishindwana hakuna namna," alisema Fortunatus.

Dodoma Jiji kwa sasa inashika nafasi ya 11 ikiwa na pointi 31 kwenye mechi 28, ilizocheza.