City haipoi, Nonga kishua zaidi

Muktasari:

  • Nonga anatarajia kutangaza kustaafu soka Juni 6 mwaka huu ikiwa ni miaka 13 tangu aanze soka la ushindani akianza kuichezea JKT Oljoro mwaka 2011.

Wakati zikibaki siku nne kuendelea na ligi kuu, Mbeya City imeendelea na mazoezi kwa ajili ya mchezo ujao dhidi ya Yanga huku ilishuhudiwa timu hiyo ikitumia saa matatu kujifua katika uwanja wa Sokoine.

City inatarajia kuwa uwanjani Juni 6 kuwakaribisha Yanga ikiwa ni mchezo wa raundi ya 29 kabla ya kuwapokea tena KMC katika mechi ya kufunga msimu wa 2022/23 utakaopigwa uwanja wa Majimaji mjini Songea Juni 9.

Leo ikisimimamiwa na Kocha wake Mkuu raia ya Uganda, Abdalah Mubiru, pia alisaidiwa na nyota wa zamani wa timu hiyo, Ally Lundenga sambamba na Straika Paul Nonga.

Hata hivyo Mwanaspoti inafahamu kuwa Nonga huenda akaagwa rasmi kucheza soka uwanjani katika mchezo dhidi ya Yanga na kupewa majukumu kikosini ikiwa ni heshima kwa nyota huyo mkongwe ambaye msimu huu amecheza mechi moja akitokea benchi dhidi ya Singida Big Stars.

Pia nyota huyo ambaye amecheza timu kadhaa ikiwamo Yanga, Mwadui, Gwambina na City tayari ameweka kabatini cheti cha ukocha leseni C inayitambuliwa na shirikisho la soka Afrika (CAF) huku Mbeya City ikihusika katika masomo yake na sasa anasubiri kupangiwa majukumu kikosini humo.

Mbeya City haijawa na matokeo mazuri msimu huu ikiwa imekusanya pointi 30 na kukaa nafasi ya 12 ikihitaji ushindi katika michezo yake miwili iliyobaki ili kubaki salama ligi kuu msimu ujao.

Katika mazoezi hayo Mubiru alitaka mastaa wake kumiliki mpira, pasi za haraka, pumzi na kufunga mabao na namna ya kuzuia hatari langoni.