CAF yaifuata Simba Dar

BAADA ya tetesi za muda mrefu, Simba imepiga bao la kisigino kwa kuteuliwa kuwa timu pekee ya Tanzania itakayoshiriki michuano mipya ya Afrika Super League itkayoanza Agosti mwaka huu, sasa imethibitisha kweli baada ya Shirikisho la Soka Afrika(CAF) kuifuata timu hiyo Dar es Salaam.
Michuano hiyo ambayo klabu shiriki itavuna Dola 2.5 milioni (Sh 5.8 bilioni) kwa maandalizi tu, achilia mbali zile itakazobeba bingwa wa michuano hiyo na CAF sasa wanaifuata Simba kwa ajili ya kuikagua ili kuangalia kukidhi vigezo na kuwekwa kwenye ushiriki wa msimu huu.
Habari za uhakika ambazo Mwanaspoti linazo ni kuwa Caf tayari imeshaziteua timu nane ambazo zitashiriki michuano hiyo itakayofanyika kwa mara ya kwanza Afrika, huku Simba ikiwa mojawapo na tayari imeshajulishwa kuhusu hilo kwa uthibitisho na uongozi wa klabu hiyo chini ya Bodi ya Wakurugenzi inayoongozwa na Salim Abdallah 'Try Again' umeshawasha taa ya kijani.
Katika kudhihirisha mambo yameiva, vigogo wa Kamati za Mashindano na ile ya Leseni za Klabu kutoka CAFm watatua nchini, Februari 14 ili kukutana na Simba kuwapa muongozo wa namna watakavyoshiriki mashindano hayo pamoja na ukaguzi wa kuona utayari wa wawakilishi hao.
Katika ujio huo, vigogo hao wa Caf watafanya ukaguzi wa viwanja ambavyo Simba inatumia kwa mazoezi, uwanja ambao utatumika kwa mechi za mashindano hayo, ubora wa miundombinu kama hoteli na barabara za kutumiwa na timu na wageni watakaokuja kushiriki mashindano hayo.
Kana kwamba haitoshi, maofisa hao wa Caf watakagua vitabu vya mapato na matumizi vya Simba, pia namna inavyoendesha shughuli za kiutawala ili kujiridhisha kama Simba imetimiza vigezo na masharti ya kushiriki mashindano hayo.
Mwenyekiti wa Simba, Murtaza Mangungu alikiri wameshapewa taarifa juu ya ujio wa vigogo hao wa Caf ingawa alisema watatoa taarifa kamili baada ya muda mfupi.
"Ni kweli ujumbe wa Caf utakuja kututembelea kwa ajili ya masuala ya African Super League na taarifa zaidi zitatolewa watu wasiwe na shaka," alisema Mangungu.
Miongoni mwa faida za mashindano hayo, ni mgawanyo wa fedha kiasi cha Dola 1 milioni (Sh 2.3 bilioni ) kwa kila nchi mwanachama wa shirikisho hilo ambalo lina jumla ya wanachama 54.
Gharama za jumla za uendeshaji mashindano hayo ni kiasi cha Dola 100 milioni (Sh 233 bilioni) na bingwa atavuna kitita cha Dola 11.5 milioni (Sh 35 bilioni).
Mashindano hayo yataendeshwa kwa muda wa miezi 10, kuanzia Agosti hadi Mei, kwa kuanzia yatashirikisha jumla ya timu nane (8) lakini mpango wa muda mrefu ni kuwa na jumla ya timu 24 kutoka kanda tatu za soka ambazo ni Kanda ya Kaskazini, Kanda ya Kati/Magharibi na Kanda ya Kusini/Mashariki ambapo kila kanda itatoa jumla ya timu nane.
Idadi ya juu ya timu kutoka nchi moja kushiriki mashindano hayo ni timu tatu na zitatokea katika nchi 16 tofauti na yatakuwa na jumla ya michezo 197 kwa mujibu wa makadirio yaliyofanywa na Caf.
Ikumbukwe mashindano hayo yalizinduliwa rasmi hapa nchini, Agosti mwaka jana katika mkutano mkuu wa Caf uliofanyika Arusha ambao uliongozwa na Rais wa Shirikisho hilo, Dk. Patrice Motsepe na Rais wa Shirikisho la Mpira wa Miguu Duniani (Fifa), Gianni Infantino ambaye alikuwa mgexni mwalikwa.
Mbali na Simba, timu nyingine zinazotajwa kuwa zitashiriki mashindano hayo ni Al Ahly na Zamalek za Misri, Wydad Casablanca na Raja Casablanca (Morocco), Mamelodi Sundowns (Afrika Kusini), Esperance (Tunisia) na TP Mazembe (DR Congo).