Beki Yanga mambo moto

Inaelezwa huko kambini Yanga imezidi kunoga kutokana na kimo cha beki mpya Mamadou Doumbia kuwafunika wenzake na kudaiwa itazidi kuufanya ukuta huo uwe imara zaidi kuzuia mipira ya juu.
Doumbia ana urefu wa Mita 1.88  akiwaacha mastaa aliowakuta ndani ya timu hiyo ambao ni nahodha Bakari, Mwamnyeto mwenye mita 1.82 , Yanick Bangala mita 1.79, Ibrahim Bacca mita 1.77 na Dickson Job mita 1.71.
Yanga inaongoza ligi ikikusanya pointi 59 katika mechi 22 ikishinda michezo 19, ikitoka sare mbili na kupoteza mara moja huku wakiruhusu mabao 10 kwenye michezo hiyo.
Wakizungumza kwa nyakati tofauti wadau wa soka walisema Yanga imekamilika kwenye safu yake ya ulinzi na ndio maana imeruhusu mabao machache shida ilikuwa ni kukosa umakini kwenye mipira ya juu ambayo ndio imeighalimu na kuruhusu mabao hayo.
Beki wa zamani wa Simba, Amri Said 'Stam' alisema Yanga imefanya usajili kulingana na mahitaji usajili wa beki huyo mpya umezingatia mahitaji kwa sababu timu yao haikuwa na uhitaji wa wachezaji wengi wameongeza nguvu muhimu.
"Mabeki waliopo ni wazuri na wamethibitisha hilo kutokana na idadi ndogo ya mabao waliyofungwa shida yao kubwa ilikuwa ni aina ya mabao wamekuwa wakikosa beki ambaye anaweza kuruka ujio wa huyu kama ataingia kwenye mfumo vizuri utasaidia;
"Ana kimo sahihi kama atafanya vizuri kazi yake kikosini atapunguza makosa madogo madogo ambayo yameonekana ndani ya timu hiyo."
Straika wa zamani wa Simba, aliyewahi pia kukipiga Jangwani, Zamoyoni Mogella 'Golden Boy' alisema kimo na uchezaji ni vitu viwili tofauti anaweza akawa mrefu lakini akakosa msaada kikubwa ni kumpa muda nimemuona kwenye mechi na Rhino Rangers alipewa dakika chache siwezi kuzungumzia ubora wake.
"Yanga ilikuwa ina uhitaji wa kusajili beki lakini suala la urefu ni ziada tu ubora ndio unatakiwa kuzungumzwa zaidi japo kimop pia kinachangia kwa kiasi kikubwa kupunguza makosa benchi la ufundi ndio linatakiwa kuwa na nafasi kubwa ya kuzungumzia usajili huu."
Kocha wa Yanga, Nasreddine Nabi alisema beki huyo anaitaji muda zaidi ili aweze kuthibitisha ubora wake alifunguka hayo baada ya kumpa dakika 45 za kwanza tangu asajiliwe na timu hiyo.
"Ni mapema sana kumzungumzia Doumbia kwa sababu amepata dakika chache za kucheza na timu ambayo haikuwa kipimo sahihi kwetu hivyo ninampa mechi tano zaidi ili aweze kuthibitisha ubora wake japo ujio wake ndani ya timu umeongeza changamoto ya namba ambayo itaongeza ubora wa kila mchezaji akitaka namba ya kucheza kikosi cha kwanza."
Kocha huyo mazoezini amekuwa akimteshi Doumbia dhidi ya mabeki wengine kama anatafuta kombinesheni nyingine ambayo atakuwa akiitumia kwenye mechi zao za ligi, ASFC na zile za CAF.