Azam FC waenda likizo na manoti mfukoni
Basi la Azam wanalotumia kusafiria
Muktasari:
Anzia hapa; kwanza uongozi wa klabu hiyo chini ya Mwenyekiti, Said Mohamed, umewaruhusu nyota wote waliopambana kupata ubingwa wa Ligi Kuu Bara msimu uliomalizika wiki iliyopita, kumpumzika kwa miezi miwili na watatakiwa kurejea kambini Juni 16
AZAM FC hawataki usumbufu, unajua nini? Imewapa likizo ya miezi miwili wachezaji wake wote na imewalipa mishahara ya miezi hiyo ili kuondoa longolongo katika kipindi hicho cha mapumziko yao.
Anzia hapa; kwanza uongozi wa klabu hiyo chini ya Mwenyekiti, Said Mohamed, umewaruhusu nyota wote waliopambana kupata ubingwa wa Ligi Kuu Bara msimu uliomalizika wiki iliyopita, kumpumzika kwa miezi miwili na watatakiwa kurejea kambini Juni 16.
Jambo la pili ni kwamba, tofauti na timu nyingine, Azam imewapatia nyota wake wote pamoja na benchi lao la ufundi mishahara ya miezi miwili katika kipindi chote cha likizo yao huku nyota hao wakisubiri bodi ya wakurugenzi ya timu hiyo ikifikiria ni kiasi gani iwapatie wachezaji hao baada ya kunyakua ubingwa.
Kwa kutwaa ubingwa wa ligi hiyo inayodhaminiwa na Vodacom, Azam itapewa Sh75 milioni.
“Tumeruhusiwa kwenda kupumzika, tumeambiwa tunatakiwa kuwa hapa Juni 16, lakini tulichofurahia kama wachezaji ni kitendo cha uongozi kutupatia mishahara yetu yote ya miezi miwili, ni wazi hata ungekuwa wewe ungefurahishwa na hilo,” alisema mmoja wa nyota wa kikosi hicho.
Mohamed aliithibitishia Mwanaspoti kwa kusema: “Kweli tunawalipa mshahara wa miezi miwili kisha watapumzika hadi Juni 16, lazima wapumzike kwa maana wamefanya kazi kubwa.”
Wakati hali ikiwa hivyo kwa kikosi kizima cha Azam, mchezaji Mohamed Konne, ambaye ni raia wa Ivory Coast yupo katika nafasi kubwa ya kutemwa na timu hiyo kutokana na kuwa majeruhi kwa muda mrefu.
Taarifa iliyopatikana kutoka katika ripoti iliyowasilishwa kwa uongozi wa Azam na kocha, Joseph Omog, imesema Konne yupo katika nafasi kubwa ya kutokuvaa jezi za timu hiyo msimu ujao ambapo nafasi yake anasakwa kiungo mchezeshaji mahiri.