Atletico yavunja rekodi

Sunday November 22 2020
atletico pic

MADRID, HISPANIA. JANA Jumamosi, imevunjwa rekodi ya muda mrefu ya Atletico Madrid kutopata ushindi katika dimba la Wanda MetroPolitano kwa miaka kumi dhidi ya Barcelona baada ya kuibuka na ushindi wa bao 1-0 kwenye mchezo wa LaLiga.

Baada ya mchezo huo Atletico imefikisha alama 20 baada ya kucheza mechi nane na ikapanda hadi nafasi ya pili ya msimamo wa ligi ikimshusha Villarreal inayoshika nafasi ya pili kwa alama 19 baada ya kucheza mechi nane.

Atletico ilijipatia bao katika dakika za nyongeza za kipindi cha kwanza baada ya golikipa wa Barca kufanya makosa ya kutoka kwenye eneo lake jambo lililompa faida Yannick Carrasco kuifungia timu yake bao ambalo lilidumu hadi dakika ya mwisho ya mchezo.

Katika mchezo huo Barca ilionekana kucheza bila ya muunganiko kuanzia eneo la ulinzi hadi ushambuliaji hususani kwa Lionel Messi ambaye muda mwingi alikuwa anatembea kiwanjani.

kipigo hicho kimesababisha Barca ishuke hadi nafasi ya 10 ikiwa na pointi 11 baada ya kucheza mechi nane huku mchezo ujao ikitarajiwa kuumana na Dynamo Kyiv kwenye michuano ya Ligi ya Mabingwa.

Ligi hiyo itaendelea leo kwa michezo minne ambapo Eibar itakuwa inaumana na Getafe saa 10:00 jioni huku Cadiz itakuwa inaialika Real Sociedad saa 12:15 na Granada itakuwa na shughuli pevu mbele ya Real Valladolid saa 2:30 kabla ya Deportivo Alaves kupepetana na Valencia saa 5:00 usiku.

Advertisement

..........................................

Na Mwandishi wetu

Advertisement