Arusha City, Nyota FC wafuata nyayo za Yanga

Wakati mabingwa wa soka Tanzania bara Yanga, jana wakifanya makamuzi ya kuinyuka timu ya Zalan FC ya Sudan jumla ya mabao 4-0, wadogo zao Arusha City wamefuata nyayo hizo Kwa kuifunga Timu ya Meserani sawa na Nyota fc nao walivyowafunga Olasiti FC.
Yanga wamepata ushindi huo katika michuano ya kuwania kutinga hatua ya makundi ya ligi ya mabingwa, huku Arusha city na Nyota FC wakiwania nafasi ya kutwaa ubingwa wa mkoa wa Arusha.
Arusha City ilifanikiwa kuichapa timu ya Meserani jumla ya mabao 4-0 katika uwanja wa Ilboru na kuwafanya kuimarika zaidi kileleni katika kundi B' wakiwa na alama sita baada ya mchezo wa awali wa kufungua ligi kuichapa timu ya Olasiti mabao 3-0.
Mchezaji Baraka Mwaikimba ndiye aliyefungua karamu ya mabao kwenye timu ya Arusha City baada ya dakika ya 25 kumtuma kipa wa Meserani kuokota mpira nyavuni, huku Neophat Jerome akifunga la pili dakika ya 43 na kipindi Cha pili nae Mathew mfamalao akifunga lake dakika ya 60 kabla Mickydady Phalis kuhitimisha bao la nne dakika 80.
Kocha wa Arusha city Mahsen Bawaziri alisema kuwa ushindi huo unatembea juu ya malengo yao ya kuutaka ubingwa wa mkoa ambao umechagizwa na mazoezi ya mda mrefu waliyoyafanya mara baada ya kupanda ligi msimu huu.
Kwa Upande wa Nyota FC waliizabua timu ya Olasiti jumla ya mabao 4-0 katika uwanja wa Edmund Rise ulioko jijini Arusha, matokeo yaliyowabakiza katika nafasi ya pili wakiwa na Alama nne baada ya mechi ya awali kuvuna alama moja katika suluhu ya bao 1-1 dhidi ya Royal.
Katika mchezo huo, Ibrahim Bakari alijipatia mabao mawili dakika ya 23 na 41 huku Godfrey Magesa akifunga dakika ya 67 na Peter mshomba kumalizia bao la nne dakika ya 83 na kuhitimisha ushindi huo mnono.
Kocha wa Nyota FC, Thobias Majira alisema wamesota sana katika ligi ya mkoa hivyo wamejiwekea malengo ya kuhakikisha hawapotezi mchezo hata mmoja Ili kufanikisha kutwaa ubingwa wa mkoa.
Nae kocha wa Olasiti Laurence Gasa alisema kuwa wameanza ligi vibaya Kwa kufungwa mechi zote mbili za awali kutokana na sababu mbali mbali zilizoko nje ya uwezo wao ambao wanaamini watayafanyia maboresho kuhakikisha wanabakiza timu mkoani Ili mwakani kuweka upya malengo makubwa zaidi.
Katika matokeo mengine timu ya Ascona FC walitoka tasa ya bila kufungana na timu ya Beach boys, sawa na Kakakuona aliyecheza na Kilinga katika uwanja wa FFU Kwa mrombo matokeo yaliyojitokeza tena Kwa USA Star waliotoka 0-0 dhidi ya CSC FC waliochezea Kangasero.