Anjelina, Giniki washinda mbio za Ngorongoro race

Anjelina, Giniki washinda mbio za Ngorongoro race

Muktasari:

  • Wanariadha Anjelina John na Shing'ade Giniki wameshinda mbio hizo  za Ngorongoro race zilizoshirikisha zaidi ya wanariadha 1000 kutoka mikoa mbali mbali nchini.

KARATU. Wanariadha Shing'ade Giniki na Anjelina John wamefanikiwa kuibuka washindi wa mbio za Ngorongoro race zilizofanyika leo Septemba 25, 2022 katika viwanja vya mazingira Bora ulioko Karatu mkoani Arusha.
Giniki ameibuka mshindi baada ya kumaliza mbio za kilomita 21 akitumia saa 1:04:01 na kujinyakulia kiasi cha Sh1 milioni huku nafasi ya pili akimaliza Mathayo Sombi aliyetumia saa 1:04:46 na kuzawadiwa Sh500,000 na Fabian Joseph akimaliza nafasi ya tatu kwa saa 1:06:32 na kuzawadiwa Sh250,000.

Kwa Upande wa wasichana Anjelina John alikata utepe wa kilomita 21 Kwa kutumia saa 1:17:01 na kuondoka na Sh1 milioni, nafasi ya pili amemaliza Fatuma Malenga  aliyetumia saa 1:33:31na kuzawadiwa Sh500,000 huku nafasi ya tatu akifika Debora Benedicto akimaliza kwa saa 1:35:58 na kuvuna Sh250,000.

"Nimefurahi kushinda leo katika mbio hizi, natumai nitazidisha juhudi za kushiriki mbio nyingi za ndani ili kujitangaza na kuboresha mda wangu kwa ajili ya kushiriki mbio za kimataifa." alisema Giniki.

Anjelina, Giniki washinda mbio za Ngorongoro race

Mbio hizo pia zilikuwa na kipengele cha kilomita 10 zilizoongozwa na wakuu wa wilaya ya Karatu Dadi Kolimba, mkuu wa wilaya ya Same, Edward Mpogoro na Mkuu wa wilaya ya Mwanga Abdallah Mwaipaya na viongozi mbalimbali wa serikali na riadha.

Katika kilomita 10 kwa upande wa wanaume, Fabian Joseph amekata utepe akitumia dakika 32:04 na kujinyakulia Sh300,000 huku nafasi ya pili akimaliza Daudi Ng'imba aliyetumia dakika 32:43 na kuzawadiwa Sh200,000 huku nafasi ya tatu akichukua Kaposhi Laizer aliyetumia dakika 33:12 na kuzawadiwa Sh100,000.

Kwa Upande wa wanawake mwanariadha Anastazia Dolomongo alishinda akitumia dakika 39:23 na nafasi ya pili akimaliza Valentine Maiko aliyetumia dakika 39:40 na Nuru Benedicto aliyemaliza nafasi ya tatu kwa dakika 43:22.

Kwa kilomita tano wanaume alishinda Bernado Geay, akifuatiwa na Francis Damian na Benjamin Bernad, huku Kwa wasichana alishinda Elizabeth Ilanda wakifuata Olive Francis na Lucia Ezekiel.

Muandaaji wa mbio hizo Kutoka Kampuni ya Meta promotion, Meta Petro alisema kuwa lengo kubwa la mbio hizo ni kukuza utalii Kwa kumsapoti Rais Samia kupitia filamu ya Royal tour.

"Malengo yetu mwaka huu yametimia na tunashukuru washiriki kutoka maeneo mbali mbali kuja kushiriki na tunaahidi kuchukua mapungufu yote ya msimu huu kama changamoto ya kuboresha mbio zetu Kwa msimu ujao." alisema Petro.