Aisha kuanza na Everton

Muktasari:
- Ratiba ya Ligi Kuu Soka Wanawake England kwa msimu ujao ambayo bingwa mtetezi ni Chelsea inaonyesha timu zitaanza kuumana Septemba 21 na itamalizika Mei 11, 2025.
BAADA ya kukamilisha uhamisho wa kujiunga na Brighton ya Wanawake akitokea BK Hacken ya Sweden, staa wa Twiga Stars, Aisha Masaka timu yake itacheza mechi ya kwanza ya Ligi Kuu dhidi ya Everton Septemba 22.
Ratiba ya Ligi Kuu Soka Wanawake England kwa msimu ujao ambayo bingwa mtetezi ni Chelsea inaonyesha timu zitaanza kuumana Septemba 21 na itamalizika Mei 11, 2025.
Brighton inatarajiwa kuanza msimu na kocha mpya Dario Vidosic aliyejiunga nao Julai mwaka huu akichukua nafasi ya Mikey Harris aliyekuwa akikaimu baada ya kufukuzwa kwa Melissa Phillips, Februari mwaka huu.
Baada ya mchezo huo utakaopigwa katika uwanja wao wa nyumbani wa Broadfield, Brighton itakuwa na mechi nyingine mbili za nyumbani ya kwanza ni Septemba 29 dhidi ya Manchester City kisha Oktoba 6 dhidi ya Aston Villa.
Mabingwa watetezi wa ligi hiyo, Chelsea wataanza kampeni ya kulitetea taji lao katika mchezo wa nyumbani dhidi ya Aston Villa.