
Muktasari:
Timu ambazo zilikuwa zikibadilishana usukani wa ligi hiyo kwa mbwembwe ni Mtibwa na JKT Ruvu ingawa Azam na Coastal Union nazo zilishaongoza kwa kipindi kifupi.
KIONGOZI wa wachezaji wa Yanga, Nadir Haroub ‘Cannavaro’ na Kocha wake, Hans Pluijm hawakuvutiwa na kiwango cha timu hiyo jana Jumatano ingawa walishinda bao 1-0 dhidi ya Coastal Union mjini Tanga kwenye mechi ya Ligi Kuu Bara katika Uwanja wa Mkwakwani mjini hapa.
Hata hivyo, nje ya uwanja mashabiki wa Yanga walikuwa wakishangilia kwa mbwembwe wakiimba:” Wapigwe tu...Coast Wapigwe tu.” Ushindi huo wa Yanga ndiyo umeifanya timu hiyo iliyofanya usajili wa zaidi ya Sh500 milioni kuongoza ligi kwa mara ya kwanza tangu msimu huu uanze kwa kufikisha pointi 22.
Timu ambazo zilikuwa zikibadilishana usukani wa ligi hiyo kwa mbwembwe ni Mtibwa na JKT Ruvu ingawa Azam na Coastal Union nazo zilishaongoza kwa kipindi kifupi.
Katika mchezo wa jana ambao ulikuwa kiporo, Yanga ilifunga dakika ya 11 kupitia kwa Cannavaro aliyefunga kwa kichwa akiunganisha mpira wa kurushwa wa kiraka mwenye nguvu za mikono, Mbuyu Twite.
Kiraka wa Coastal, Mkenya Rama Salim aliisumbua ngome ya Yanga mara nyingi na dakika ya tano alikosa bao la wazi baada ya kushindwa kumsoma kipa Ally Mustapha ‘Barthez’, hata kipa wa Coastal Union alikumbana na kashikashi kadhaa za Andrey Coutinho na Amissi Tambwe.
Mchezo huo ulitawaliwa na butuabutua nyingi zilizotokana na ubovu wa uwanja jambo ambalo lilisabaisha majeraha kwa baadhi ya wachezaji wakiwamo Amissi Tambwe na Twite.
Kipindi cha pili hakuna shambulizi lolote la maana lililofanywa na timu hizo huku ubabe na kupoteza muda vikitawala.
Kocha Pluijm alisema: “Hatujacheza soka letu, uwanja ulikuwa mgumu sana na haukuwa na mazingira rafiki kwa wachezaji, lakini nilichofurahia ni kwamba tumeshinda.”
Cannavaro alikiri hawakucheza katika kiwango chao, lakini akawasihi mashabiki wawavumilie akisema ligi ina vikwazo vingi.
Kocha Mkenya anayeinoa Coastal, James Nandwa alisema ni aibu kupoteza mchezo nyumbani, lakini wamefanya uzembe kuiruhusu Yanga kutumia nafasi moja waliyoipata. “Wamepata nafasi moja tu na wameitumia ipasavyo, ni uzembe wetu.”
Kwa mujibu wa msimamo ulivyo, Yanga inaongoza kwa pointi 22, ikifuatiwa na Azam 21, huku Mtibwa, Polisi Morogoro, Ruvu Shooting na JKT Ruvu kila moja ikiwa na pointi 18. Yanga; Barthez, Twite, Oscar Joshua, Rajab Zahir, Cannavaro, Said Makapu, Simon Msuva, Salum Telela, Tambwe/Danny Mrwanda, Kpah Sherman, Coutinho/Hussein Javu
Coastal; Kado, Hamis Mbwana, Sabri Rashid/Othman Tamim, Abdalla Mfuko, Tumba Said, Abdulhalim Humoud, Joseph Mahundi/Mohammed Mtindi, Godfrey Wambura, Hussein Sued, Rama Salim, Hub Imben/Kenneth Masumbuko.