Yanga yanasa beki wa Henry

Tuesday May 10 2022
Yanga PIC
By Charity James

KIKOSI cha Yanga jana kilishuka uwanjani kuvaana na Tanzania Prisons, lakini mashabiki wa klabu hiyo wana kila sababu ya kufurahi zaidi kwa sasa baada ya mabosi wa timu hiyo kumnasa beki wa kushoto fundi wa kumwaga maji.

Yanga kwa misimu miwili mfululizo sasa imekuwa na tatizo la beki wa kushoto tangu, Gadiel Michael kuikacha timu hiyo na kutua Simba, jambo lililomfanya Kocha Nasreddine Nabi kumtumia beki wa kulia, Kibwana Shomary au winga Farid Mussa nafasi hiyo.

Sio kama Yanga haina mabeki wa kushoto hadi Nabi kuamua kuwatumia nyota hao la, kikosini kuna David Bryson na Yassin Mustafa ambao walikuwa wakisumbuliwa na majeraha ya muda kiasi cha kutokuwa fiti kwenda na kasi ya Yanga ya sasa.

Hata hivyo, katika kuhakikisha kikosi cha msimu ujao kinakuwa moto kwenye mbavu zote mbili, mabosi wa Yanga wamemnasa beki wa kushoto aliyewahi kunolewa na nyota wa zamani wa Monaco, Arsenal, Barcelona na timu ya taifa ya Ufaransa, Thierry Henry.

Beki huyo aliyenaswa na Yanga huku kiungo was sasa wa timu hiyo, Khalid Aucho akitajwa kuhusika kwa kiasi kikubwa kumvutia nyota huyo mpya ni Mustafa Kizza anayeichezea pia timu ya taifa ya Uganda, The Cranes.

Habari za uhakika kutoka ndani ya Yanga na chanzo chetu kutoka Uganda ni kwamba, Kizza aliyenolewa na Henry akiwa Montreal ya Canada ameshamalizana na Yanga kwa kila kitu akiwa kama mchezaji huru.

Advertisement

Beki huyo mwenye miaka 22, aliyeibuliwa na KCCA ya Uganda ni mchezaji huru baada ya kumaliza mkataba wake na Montreal na kilichobaki sasa ni kusubiri kuja Dar es Salaam mara ligi itakapoisha Juni kuungana na wenzake kwa maandalizi ya msimu mpya baadae.

“Kizza anakuja Tanzania, anakuja Yanga baada ya kumalizana na mabosi, ni beki mwenye uwezo mkubwa na amewahi kufanya kazi na Henry kabla ya kocha huyo kuteuliwa kama kocha msaidizi wa Ubelgiji mapema mwaka jana,” kilisema chanzo chetu kilichodokeza kuwa Kizza kavutiwa na uwepo wa Aucho Jangwani.

“Ni mchezaji mzuri na yupo huru kwa sasa baada ya kumaliza mkataba, kwa kiwango alichonacho hasa kuichezea timu ya taifa ya Uganda inampa nafasi ya kuja kuingia moja kwa moja katika mipango ya kocha kwani msimu ujao mashindano makubwa na tunahitaji kuwa na kikosi chenye wachezaji bora,” kilisema chanzo hicho ambacho hakikutaka kutaja jina lake.

Beki huyo anayesifika kwa kukaba kwa nguvu na akili sambamba na kutengeneza mashambulizi na mkali wa kupiga krosi zenye macho, alianza kucheza soka la kulipwa KCCA mwaka 2016, akizitumikia pia timu za taifa za Vijana U20 na U23 za Uganda kabla ya kupanda timu ya wakubwa The Cranes mwaka 2019 na kudumu nayo hadi sasa.

Mbali na mchakato huo wa usajili unaoendelea pia uongozi wa klabu hiyo upo kwenye mazungumzo na mastaa wake ambao mikataba yao inaelekea ukingoni tayari ili kuwaongezea mipya.

Mastaa hao wanaomaliza mikataba yao, japo sio wote wanaoweza kusalia katika kikosi cha msimu ujao ni nahodha Bakar Mwamnyeto, Shomari Kibwana, Said Ntibazonkiza, Yacouba Songne, Zawadi Mauya, Paul Godfey ‘Boxer’ na Abdallah Shaibu ‘Ninja’.

Advertisement