Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Tusker kicheko, mabao kuamua ubingwa

Tusker kicheko, mabao kuamua ubingwa

MECHI ambayo Kakamega Homeboyz walikuwa nayo mkononi, hawakuitumia vyema hivyo kuwafanya mabingwa watetezi, Tusker FC, kuwa katika nafasi nzuri kutetea taji lao.

Tusker FC wamekabana koo na Homeboyz kileleni mwa msimamo Ligi Kuu Kenya wote wakiwa na pointi 57 lakini Wanamvinyo wana idadi nzuri ya tofauti ya mabao ya kufunga na kufungwa.

Vijana hao wa Robert ‘Simba’ Matano hawakuwa na mechi ya FKFPL wikendi iliyopita hivyo walikuwa wanafuatilia kwa karibu mtanange kati ya Homeboyz inayonolewa na mzawa Bernard Mwalala dhidi ya AFC Leopards inayofundishwa na Mbelgiji Patrick Aussems.

Mchezo huo uliyohudhuriwa na idadi kubwa ya mashabiki ulichezwa katika Uwanja wa Bukhungu, Kaunti ya Kakamega na kumalizika kwa Ingwe kutamba kwenye Ingo derby mabao 2-0 yakipachikwa na Collins Shivachi na Kingsley Olaniyi.

Sare tu ingetosha kuwarudisha Homeboyz kileleni wakati ushindi ungewafanya wawazidi kwa pointi tatu Tusker FC hivyo kuufanya ubingwa kuwa mikononi mwao kupoteza.

Hesabu za Homeboyz sasa ni kushinda mechi mbili zilizosalia dhidi ya Talanta FC na Kariobangi Sharks na kuomba Tusker FC watelezi katika mechi zao mbili za mwisho wa msimu dhidi ya Posta Rangers na Bidco United.

Leopards walipanda kwenye msimamo hadi nafasi ya sita na pointi 45.

Bandari FC nao walipoteza nafasi adimu kupunguza pengo la pointi na vinara wa ligi walipolazimishwa sare ya kutofungana na Ulinzi Stars pungufu mechi iliyopigwa Kericho Green Stadium.

Licha ya kuambulia pointi moja ugenini, Bandari FC bado wapo kwenye mbio za ubingwa ila watahitaji kushinda mechi zao zote zilizobaki dhidi ya Sofapaka na Police FC, na kuwaombea Tusker FC na Homeboyz wapoteze mechi zao.

Vihiga Bullets na Wazito FC bado wapo kwenye ‘danger zone’ hususan baada ya kupoteza mechi zao za mwishoni mwa wiki; Vihiga Bullets walifungwa bao 1-0 na Sofapaka wakati Bidco United wakawakaranga Wazito FC mabao 2-0.

Wanaojikongoja kujiweka katika hali salama kubaki FKFPL msimu ujao ni Nzoia Sugar kufuatia ushindi wa bao 1-0 dhidi ya KCB.


MABAO KUAMUA UBINGWA, MWALALA AJIPA ROHO

Baada ya kuvurugiwa mahesabu na AFC Leopards kwenye harakati zao za kushinda ligi kuu, Kocha Bernard Mwalala amebaki kujipa roho tu.

Huku sasa timu zote zikiwa zimesalia na mechi mbili tu, kama farasi hao wawili watafanikiwa kuzishinda, basi bingwa atalazimika kuamuliwa kwa idadi ya mabao.

Kipigo cha wikendi kimemwacha Mwalala na maruweruwe akishindwa kutoa utathmini wa kikosi chake ambacho wakati mmoja kilikuwa kimefungua gepu la pointi 15 kati yao na Tusker kileleni.

“Vitu hivi hutokea kwenye mpira, kusema kweli siwezi kukuelezea na wapi tulikosea ama nini kilichotokea hadi tukapoteza mechi hiyo muhimu. Nahisi ni uchovu wa msimu mzima unatukosti. Ila yameshatokea lakini kubwa ni bado tupo kwenye kinyangányiro. Tutaendelea kupambania taji la ligi hadi dakika ya mwisho” Mwalala kajipa roho.

Mechi ijayo ya Homeboyz ni dhidi ya FC Talanta waliowatandika bao moja mtungi kwenye mzunguko wa kwanza. Kisha watamaliza kazi na Kariobangi Sharks.

Kwa mpinzani Tusker, mechi zijazo ni dhidi ya Bidco United waliowatandika 2-1 kwenye mzunguko wa kwanza kisha wamalize shughuli kwa kulipiza kisasi dhidi ya Posta Rangers waliowafinya 1-0 kwenye mzunguko wa kwanza.


Otanga asubiria msimu ujao

Baada ya KCB FC kujipotezea rada kwenye ufukuziaji wa taji la ligi kuu msimu huu, kile walichobakia kupambania ni kiatu cha dhahabu.

Straika wao Derrick Otanga anaongoza orodha ya wafungaji akiwa na mabao 14 huku akifuatiwa kwa karibu na Clifton Miheso 13, aliyepachika mawili juzi wikendi dhidi a Posta Rangers.

Baada ya kumaliza wa pili msimu uliopita wakipoteza uongozi zikiwa zimesalia mechi mbili tu na kuwaruhusu Tusker kupita na kombe, KCB walianza msimu huu kwa vishindo.

Otanga anakiri msimu huu wameshachemsha lakini amewaahidi mashabiki, kuwapa ubingwa huo msimu ujao.

“Kwa jinsi mambo yalivyo kwa sasa, hatuwezi kushinda kombe la ligi kuu ila tutajitahidi kushinda mechi mbili tulizosalia nazo ili tuone mwisho wa siku tutamalizia wapi msimu huu. Ningependa tu kuwaomba mashabiki wetu watuwie radhi, huu haukuwa msimu wetu licha yetu kuanza vizuri, ila msimu ujao tutarejea kwa nguvu zaidi,” kafunguka.

Kocha Zedekiah Otieno tayari alishakataa tamaa akilalamikia majeruhi kuwa chanzo cha kuwavurugia tempo yao. Uongozi wa KCB umesema kuwa hauna mpango wa kumtimua licha yake kushindwa kutimiza malengo waliyompa msimu huu baada yake kuikosa kombe 2020/21.