Soka Kenya laachwa kwa mataa

Soka Kenya laachwa kwa mataa

WAZIRI wa Michezo, Balozi Amina Mohammed ameendelea kusalia kimya kuhusu uongozi wa soka nchini baada ya muhula wa Kamati ya Mpito kufika mwisho na kumalizika kwa msimu.
Kumekuwepo na taarifa kwamba kamati mpya, Kamati ya Usimamizi (Management Committee)  imeundwa kuchukua mahala pa Kamati ya Mpito (Transition Commitee) na kwamba tayari imepokea baraka zake Waziri Mohammed.
Hata hivyo, Waziri alijitenga na kamati hiyo iliyobuniwa na wanachama 13 wa  matawi ya Shirikisho la soka nchini FKF. Kamati hiyo ya Usimamizi inaongozwa na mwenyekiti Robert Macharia.
“Tupo tayari kufuata sheria kwa kuchukua usimamizi wa soka letu tukitegemea sapoti ya serikali. Matawi ya FKF yamekuwa yakiendesha Divisheni ya pili na tupo tayari sasa kuchukua majukumu haya ili kuanza mchakato wa kujiondolea marufuku ya  FIFA,” Macharia ambaye ni mwenyekiti wa FKF tawi la Murang’a alisema.
Hali hii imeacha hali tete hasa baada ya Kamati  ya Mpito kumaliza muhula wake wa wiki tano toka ilipoteuliwa na Balozi Alhamisi 16, Juni 2022 na kuchapichwa rasmi kwenye sajili ya serikali. (Kenya Gazzette)
Kwa sasa hali ni tete isijulikane na nani anayeongoza soka. Kamati ya Mpito inasisitiza bado ipo madarakani licha ya muda wao kumalizika rasmi, huku Kamati ya Usimamiz yake Macharia ikisema ipo tayari kuendelea na kazi. Ni nini sasa kitakachofuata? Bado haijulikani.