Simba yaizidi akili Platinum

PLATINUM FC wanatua leo Dar es Salaam. Lakini wanalia kwamba Simba inawafanya kitu ambacho kinawachanganya akili wasijue nini cha kufanya.
Wanadai kwamba wamenasa habari za uhakika kuwa Simba inataka kusajili mmoja wa mastaa wao watatu na inawasiliana nao kwa siri sana.
Wameenda mbali zaidi kwa kuwataja mastaa hao ambao ni Perfect Chikwende, Gift Bello na Petros Mhari.
Chikwende ndiye aliyewazidi nguvu mabeki wa Simba akapachika bao pekee kwenye mechi ya awali ya Ligi ya Mabingwa waliyokutana Jijini Harare.
Ofisa Habari za Platinum, mwanadada, Chido Chizondo alidai kwamba wanajua kuna mawasiliano ya chinichini ya kutaka mmoja wa mastaa hao haswa Chikwene.
“Hawajaja klabuni rasmi, tunaamini kwamba hii haiwezi kuwa mchezo mchafu, kuwatoa wachezaji mchezoni,” alidai Chido.
Viongozi wa Platinum wana wasiwasi kwamba baadhi ya vigogo wa Simba wanawadanganya wachezaji hao kwamba itawasajili ili wadanganyike kwenye mechi ya Jumatano ambayo mshindi anaingia makundi ya Afrika.
Simba inahitaji ushindi wa mabao 2-0 ili kusonga mbele kwenye makundi ya Afrika inayoanza mwezi ujao mwanzoni.
Licha ya Platinum kulia kwamba mastaa hao wanawindwa na Simba lakini Mwanaspoti linajua kuwa vigogo wa Azam ndiyo wanapambana kumshusha Chikwende na huenda wakamalizana nae baada ya mechi na Simba ili achukue mikoba ya Obrey Chirwa ambaye anaonekana kuchuja.
Azam wanatumia ushawishi wa wachezaji wake raia wa Zimbabwe kumnasa Chikwende na ameshaingia laini.