Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Sekunde moja tu yamnyima ulaji

Muktasari:

“Aliniacha sekunde moja tu, ilikuwa niwe bingwa, yeye akanizidi kete akaondoka na Dola 300,000, mimi Dola 100,000.”

Maisha ni safari, Ndio, ni safari ambaye hakuna ajuae mwisho wake utakuaje, wa mateso au mafanikio. Siri hiyo aijuaye ni mmoja tu, Mwenyezi Mungu.

Kila mwanadamu anasafiri, yuko safarini na hata mwanariadha maarufu nchini Fabiano Joseph Naasi ni mmoja wa wasafiri na jana katika makala haya ya simulizi la maisha yake na safari yake yenye misukosuko kibao na iliyojaa machungu, alieleza namna alivyotoroika kijijini kwao Gedamali, Wilaya ya Babati mkoani Manyara kwenda Arusha baada ya kumaliza elimu ya msingi.

Lengo kubwa ni kwenda kujaribu kutimiza ndoto yake kubwa ya kuwa mwanariadha mkubwa.

Hata hivyo, haikuwa rahisi, lakini alipambana na hadi kupata medali ya kwanza ya shaba kupitia mashindano ya Mount Meru Marathoni. Hapo sasa, safari yake ya mafanikio ikaanza baada ya kupata dili kenya na yaliyobaki ni historia. Leo anaelezea safri yake ya Kenya na dili tamu alizoweza kupata huko. Endelea naye....

Anasema katika mbio hizo alilipwa fedha nzuri pia Puma ikawa ikimpa bonusi. “Nilirudi nyumbani Tanzania kwa kocha Max, mafanikio yale yaliishtua familia yangu, pale ndipo walianza kuona umuhimu wa riadha.

“Nakumbuka nilikwenda kijijini, waliponiona wazee walifurahi mno, pale ndipo walinipa baraka zao mimi niendelee kuwa mwanariadha.

Anasema mzee alimhusia kupambana zaidi na kumpa wosia wa kuepukana na makundi mabovu, hakuna aliyekumbuka njia aliyotumia tena kuondoka nyumbani kwao. “Nilikaa kijijini kwa muda nikarejea kwa kocha Max, ambaye wakati ule ndiye alikuwa kama baba yangu.

“Alinishauri mambo mengi, alinilea kama mtoto wake wa kumzaa, hakunibagua na hata nilipokuwa nikipata fedha katika mbio, yeye ndiye alinishauri ninunue kiwanja nijenge, pia alimwandaa na mazoezi wakipigia hesabu ya kuwa nyota mkubwa wa riadha.

Ashinda Dola 100, 000,

anunua Landcruser

Ukiachana na wanariadha wakongwe, Fabiano ni mwanariadha ambaye mpaka sasa yuko katika timu ya taifa mwenye mafanikio zaidi ya wenzake.

Fabiano anakwambia mafanikio hayo hayajatokana na kusoma sana! la hasha! ni kutokana na spidi yake ya miguu.

Mwanariadha huyo anamiliki mjengo wa ghorofa moja uliopo Ilboru nje kidogo ya Jiji la Arusha ambako ndiko anaishi ambao anasema umegharimu Sh110 milioni.

Ukiachana na mjengo huo, Fabiano pia ana nyumba nyingine mbili ambazo amepangisha, kila moja imemgharimu Sh70 milioni. Nyumba moja ni ya kuishi familia ipo Sanawali amepangisha wazungu na nyingine ipo kwa Mrombo ambayo ina vyumba 24 vya kupanga.

Kama haitoshi, Fabiano amenunua lori la kubeba mchanga ambalo anasema alinunua Dola 22,000 mwaka 2004 ambalo analifanyia biashara kwa wiki lina wastani wa kumwingizia Sh800,000, achilia mbali nyumba ya maana tu ambayo anasema amemjengea mama yake kijijini Gedamali.

“Yote hayo nimeyafanya kwa fedha niliyoipata kwenye riadha, sijasoma sana lakini kwa kupitia riadha, naheshimika kwa niliyoyafanya ya maendeleo,” anasema Fabiano.

Katika nyumba ambayo Fabiano anaishi ni moja ya mijengo ya maana katika eneo la Ilboru, ni eneo kubwa tulivu na mwenyewe anasema eneo hilo alinunua kwa maelekezo ya kocha Max na alianza kujenga mwaka 2003 na alimaliza mwaka 2004 baada ya kushinda mbio za Dubai marathoni.

“Kwenye mbio za Dubai nililipwa Dola 100,000, nilitumia Dola 22,000 kununua fuso yangu ya mchanga, nikanunua kiwanja kwa Mrombo na fedha nyingine nilimalizia nyumba yangu ya ghorofa na kuhamia, iliyobaki nikatumia na nikanunua gari aina ya Landcruser milioni 24 ingawa nilinunua kwa mtu,” anasimulia.

Sekunde moja yamkosesha Dola 300, 000

Katika mbio za Dubai marathoni, bingwa alikuwa akiondoka na Dola 300,000 ambazo Fabiano anakumbuka namna sekunde moja ilivyomkosesha kitita hicho. “Ile mbio ilikuwa ngumu, mastaa wote walishiriki, hakuna kati yetu ambaye alitegemea angeshinda kutokana na ushindani.

“Wote tulikuwa tunafahamiana, kila mmoja alijua ile ngoma ngumu, ‘position’ ilikuwa haijulikana, tofauti na mbio nyingine, bingwa anajulikana mapema kutokana na ‘time’ yake, lakini ile ilikuwa tofauti.

“Kulikuwa na ushindani kutoka Tanzania, Ethiopia, Eritrea na Kenya na mshindi alikuwa Wanjiru.

Anasema wao walikimbia nusu marathoni na baada ya kukimbia kama kilomita 10 walianza kupungua,

“Muethiopia na Mueritrea walijipunguza, pale ndipo ilikuwa aliyekwenda ameenda na aliyebaki amebaki, tukawa tumebaki mimi na Wanjiru.

“Tulipofika kilomita 18 Wanjiru aliniacha, lakini nilipambana kumfukuza nikafunga ‘gape’ tulipofika kilomita 20 (kilomita moja kabla ya kumaliza mbio), tukawa sambamba.

“Tukiwa tumebakiza kama mita 10 kumaliza, wakati ule pale uwanjani wanatangaza mmoja kati yetu kuchukua ubingwa, Wanjiru alinizidi ujanja akawahi kukanyaga mstari wa kumaliza mbio. “Aliniacha sekunde moja tu, ilikuwa niwe bingwa, yeye akanizidi kete akaondoka na Dola 300,000, mimi nikachukua Dola 100,000 za mshindi wa pili,” anasimulia.

Anasema fedha hizo walipewa zote bila kukatwa, licha ya kuwa fedha nyingi kutamka lakini kwake ilikuwa ni kitu cha kawaida kwani alikuwa amezoea kushinda fedha katika mbio tofauti tofauti kabla ya hizo japo mara nyingi alikuwa akishinda Dola 50,000, 30,000 na 20,000.

“Wakati ule nilikuwa siangalii sana fedha kwanza, kwangu nilitaka medali kwanza nikiamini baada ya medali fedha zitakuja, kilichoniuma ni kukosa medali ya dhahabu,” anasema.

Mwaka uliofuatia, Fabiano alitimiza ndoto yake nyingine kwa kutwaa medali ya dhahabu ya dunia ya mbio za marathoni nchini Canada. “Nilikuwa nimerejea kunolewa na kocha Max, hadi nakwenda Canada nilikuwa chini yake, medali ile ni matunda ya Max,” anasimulia.

Hakuishia hapo, mwaka 2006, alikoleza ushindi wa mwanariadha mwenzake Samson Ramadhan kwenye michezo ya Jumuiya ya Madola nchini Australia.

Kwenye michezo ile, Samson ambaye sasa amestaafu alishinda medali ya dhahabu ya marathoni, wakati Samson akishinda medali hiyo, Fabiano alishinda medali ya shaba ya mbio ndefu za uwanjani za mita 10,000.

Medali hizo ndizo zilikuwa za mwisho kwa Tanzania katika historia ya michezo ya Jumuiya ya Madola na kwenye michezo ya 2010 India, 2014 Scotland na 2018 Australia Tanzania ilitoka kapa.

Achukuliwa na Jeshi kutokana na kipaji

Riadha imempa Fabiano ajira ya kudumu Jeshi la Wananchi Tanzania (JWTZ) ambako anasema kocha wa JKT, Andrew Panga ndiye alivutiwa na kiwango chake. “Tulikutana naye kwenye mashindano wilayani Karatu, wakati wa mbio kumbe alikuwa akifuatilia nilivyokuwa nakimbia, baadae alinitafuta akaniambia nawafaa jeshini.

“Aliniuliza, huko tayari kujiunga na jeshi? Nikamwambia hilo sio la kuuliza kocha, napenda sana, akaniambia basi ngoja nipeleke taarifa zako kwa wakubwa, nitakutafuta.

“Kweli walipoangalia rekodi zangu kimataifa walinitafuta, sikuwa na muda wa kujivunga, nilijiunga na jeshi,” anasema.

Anasema akiwa jeshini amejifunza vitu vingi, lakini kikubwa jeshi limemfundisha maadili akiwa chini ya kocha Panga wa JKT na sasa Mwingereza wa JWTZ.

Mipango yake ni kuiletea nchi medali ya dunia ya ya majeshi na Olimpiki ya 2020 kabla ya kufikiria kustaafu timu ya Taifa ili awaachie vijana.