Okwa, Kanoute waliamsha Simba

Okwa aanza mikwara Simba

NYOTA saba waliokwama kuwepo kambi ya maandalizi ya timu ya Simba kwa msimu mpya (pre season) akiwamo Nelson Okwa na Sadio Kanoute juzi walijumuika wenzao kwenye mazoezi ya timu hiyo iliyorejea nchini kutoka Ismailia.

Kocha Zoran Maki aliwapata wachezaji mapumziko mafupi kwenda kusalimia kwao baada ya kutua juzi mchana na kuwataka jana mchana kuwahi kambini kabla ya jioni kujifua kwenye Uwanja wa Mo Simba Arena uliopo Bunju wakiungana na wenzao.

Nyota waliokuwa Stars waliokuwa sehemu ya mazoezi ni Aishi Manula, Mohammed Hussein, Kibu Denis, Mzamiru Yassin na Kennedy Juma ambao Zoran mapema alisema ana hamu ya kukutana nao ili kumrahisisha kazi ya kusuka kikosi kabla ya mechi ya Simba Day watakaotesti mitambo na St George ya Ethiopia.

Meneja wa Habari wa Simba, Ahmed Ally alisema Kanoute alikuwa na changamoto ya hati ya kusafiria ila sasa mambo ni mazuri ndio maana ameungana na wenzake kambini na kuwa na ratiba kama wengine.

“Hakuwa na timu kutokana na sababu hiyo na taarifa niliyonayo leo (jana) alikuwa kambini na alikuwa sehemu ya mazoezi ya kwanza baada ya kikosi kurejea hapa nchini,” alisema Ally.

“Jana tumemtangaza mchezaji mpya mshambuliaji mwenye wasifu mkubwa ambaye naye atapata wiki moja ya kufanya mazoezi na wenzake kabla ya kwenda kucheza mechi ya Ngao ya Jamii dhidi ya Yanga.”