Okwa aanza mikwara Simba

Okwa aanza mikwara Simba

SIMBA imemtambulisha nyota mpya kutoka Rivers United ya Nigeria, Nelson Okwa kama Mwanaspoti lilivyowajulisha mapema, huku mchezaji huyo akifunguka makubwa.

Okwa amesema amekuja kupiga kazi na mashabiki wa Msimbazi wasubiri kupata burudani, wakati Kocha Zoran Maki akipagawishwa naye.

Kocha Zoran amekiri kufurahishwa na usajili wa mchezaji huyo hasa kutokana na kumudu kucheza zaidi na nafasi moja uwanjani, huku Okwa akisema anajua kilichomleta nchini na kusisitiza Simba ni timu kubwa naye ana jukumu la kuipa heshima zaidi barani Afrika.

Okwa aliyeonwa na Simba kwenye mechi ya Ligi ya Mabingwa Afrika msimu uliopita wakati Rivers ilipocheza na Yanga katika raundi ya awali na timu hiyo kushinda nje ndani kwa bao 1-0 na mchezaji huyo kung’ara kwa soka maridadi.

Mwanaspoti ndilo lililokuwa la kwanza kuujulisha umma juu ya usajili wake Msimbazi na hata ujio wake na usiku wa juzi alitambulishwa baada ya kutua Dar es Salaam.

Alipozungumza na gazeti hili alisema amefurahi kucheza soka katika timu kubwa na yenye mafanikio makubwa kama Simba kwani hayo yalikuwa ni malengo yake.

Okwa alisema amekuja Simba kuonyesha kiwango bora na kuipigania timu katika kila mechi ili kupata matokeo mazuri ya ushindi ambayo kila mmoja anatamani kuona wanakuwa nayo na kwamba hatawaangusha wanachama, mashabiki na wapenzi wa klabu hiyo.

“Ni changamoto nyingine mpya kubwa katika maisha yangu ila naamini nitakuwa na msimu mzuri hapa Simba kutokana na uwezo wangu pamoja na ushirikiano nitakaoupata kutoka kwa wachezaji wenzangu, kwani hakika Wanasimba watafurahi.

“Kikubwa nahitaji kuona Simba ikipata mafanikio, nikitamani kuwa sehemu ya wachezaji ambao watatoa mchango katika hilo baada ya hapo hayo mengine yatafuata na nikikaa ndani ya timu kwa muda mwingi zaidi naweza kuongea zaidi ya haya.”


ZORAN AKUNWA

Kocha wa Simba, Zoran Maki akiwa kambini hapa Ismalia Misri, alifurahishwa na usajili wa nyota huyo mwenye uwezo wa kucheza winga zote mbili pamoja na kiungo na uwezo wake wa kufunga na kutengeneza nafasi.

Zoran alisema baada ya kuambiwa siku ya kwanza na uongozi wanakwenda kumalizana na Okwa alitenga muda wake kumwangalia na kubaini ni aina ya wachezaji daraja ambalo anastahili kucheza kwenye kikosi hicho.

Alisema Okwa mzuri katika kutengeneza nafasi za kufunga, anafunga mwenyewe mabao kwa staili mbalimbali, msumbufu kwa mabeki wa timu pinzani, anaweza kucheza nafasi zaidi ya moja uwanjani kiukweli walikuwa wanahitaji mchezaji wa aina yake.

“Atakuja kuongeza kitu katika eneo letu la kushambulia kutokana na uwezo huo aliokuwa nao katika mashindano ya ndani pamoja na yale ya kimataifa kama malengo yetu yalivyo,” alisema Zoran.

“Katika nafasi ambayo anacheza kuna wachezaji wengine wenye uwezo kwa maana hiyo kutakuwa na ushindani wa kutosha kati yao na kila mmoja atataka kufanya au kuonyesha kiwango bora ili kuendelea kupata nafasi ya kucheza zaidi,”

“Kutokuwepo kwenye maandalizi ya msimu si shida tutarudi Tanzania tutakuwa naye pamoja nitamwangalia utimamu wake wa mwili kama upo tayari kushindana.Kama hatakuwa sawa kuna programu za mazoezi na ndani ya muda mfupi atakuwa sawa.

“Naamini katika kiwango chake kama atacheza vile nilivyomuona ni miongoni mwa usajili mwingine bora uliofanyika kwenye dirisha hili kubwa, nahitaji wachezaji kama hawa ndani ya kikosi changu.”

Katika hatua nyingine Zoran alisema unapokuwa na mchezaji anayeweza kucheza kwenye nafasi zaidi ya moja uwanjani maana yake anatoa fursa kwa benchi la ufundi kumtumia katika nafasi tofauti.

“Ngoja tuone baada ya mchezaji kujiunga na wenzake kitu gani kitatokea ila kikubwa naamini katika ubora wake hadi tukavutiwa naye kumsajili,” alisema Zoran.