Moto wa Simba waitisha Orlando

Saturday April 23 2022
Moto PIC
By Khatimu Naheka

SIMBA ikiwa na hazina ya ushindi wa nyumbani wa bao 1-0, inatarajiwa kutua Johannesburg kesho, tayari kwa mchezo wa marudiano dhidi ya wenyeji wao Orlando Pirates, lakini kuna joto flani linalowasumbua Wasauzi kabla ya mchezo huo kutokana na moto mkali iliyonayo Simba na mabadiliko wanayoweza kukutana nayo katika mechi hiyo ya Jumapili ya robo fainali ya Kombe la Shirikisho Afrika.

Kocha wa Orlando inayoshiriki Ligi Kuu ya Afrika Kusini (PSL), Fadlu Davids anayefanya kazi kwa ushirikiano mkubwa na kocha Mandla Ncikazi ambaye alichafua hali ya hewa mara baada ya mchezo wa kwanza jijini Dar es Salaam, amesema wanaamini timu yao itashinda mchezo huo, lakini kitu ambacho wanatakiwa kuwa nacho makini ni mabadiliko ya eneo la kiungo ambayo watayafanya katika mchezo ujao utakaopigwa Jumapili.

Davids alisema anafahamu kwamba Simba itamrudisha kikosini kiungo Sadio Kanoute raia wa Mali ambaye uwepo wake utaongeza ubora katika eneo la kiungo la Wekundu hao.

Kocha huyo anayeheshimika kwa kazi ya kujua kuwasoma wapinzani aliongeza kuwa wamewaambia wachezaji wao kwamba lazima wawe bora katika dakika 45 za kwanza kuweza kupata mabao huku pia wakitakiwa kuwa makini na viungo washambuliaji wa pembeni wa timu hiyo pamoja na mabeki wao.

“Tunafahamu Kanoute atarudi uwanjani katika mechi hii huyu ni kiungo mzuri ambaye anacheza kisasa, nikwambie tu kuna wakati tulikaribia kumsajili wakati akitoka mashindano ya Afrika (CHAN), lakini tulibadili mawazo,” alisema Davids na kuongeza;

“Watakuwa na maboresho katika safu yao ya kiungo tunachotakiwa na tumewaambia wachezaji ni kwamba lazima tupate mabao katika dakika 45 za kwanza lakini itategemea na ubora wetu kuweza kufungua eneo lao la kiungo na lile la ulinzi.

Advertisement

“Kuna beki wao pia atarudi yule wa Kenya (Joash Onyango), hatupaswi kudharau watu wa kule mbele Simba kuna watu wana kasi sana hasa wale wa pembeni sambamba na wale mabeki wao wa pembeni pia.”


BM3 AMPA AHUENI

Aidha, Davids alizungumzia kutokuwepo kwa mshambuliaji wao wa zamani, Bernard Morrison ‘MB3’ akisema kumewapa nafuu fulani na kuwapunguzia presha kubwa kutokana na ubora wa raia huyo wa Ghana.

“Morrison tunamfahamu nafikiri ubora wake ni kitu kinachojieleza hata ukiangalia alivyowasaidia katika mechi iliyopita kuna mashambulizi mawili bora ambayo Simba waliyafanya kwa kila kipindi na yote yalifanywa na Morrison , kukosekana kwake katika mechi hii ni kitu muhimu kwetu ingawa nasema bado tunatakiwa kuwa makini na wachezaji wengine.”

Morrison mwenye mabao matatu na asisti nne katika michuano hiyo, ndiye aliyesababisha penalti iliyoimaliza Orlando jijini Dar es Salaam iliyokwamishwa kimiani na Shomary Kapombe.

Wakati Kocha wa Orlando wakiwa matumbo joto, mwenzao Pablo Franco ameendelea kuwapika vijana wake kwenye mazoezi yanayofanyika Mo Simba Arena kabla ya kulipanga jeshi lake atakalosafiri nalo saa 1:00 asubuhi leo kwenda kumaliza kazi Jumapili akipania kuivusha Simba nusu fainali ya michuano hiyo ya pili kwa ukubwa ya klabu.

Advertisement