Zinaanza upya kuisaka Ligi Kuu Bara
Muktasari:
- Licha ya Ligi hiyo kukua kwa kasi kutokana na aina ya wachezaji wakubwa na wazoefu ambao wamejiunga na klabu mbalimbali, ila zipo timu zilizowahi kushiriki Ligi Kuu Bara na sasa zinapambana kurejea tena, kama Mwanaspoti linavyozielezea.
MSIMU mpya wa 2025-2026, wa Ligi ya Championship unatarajia kuanza rasmi Ijumaa hii ya Oktoba 10, 2025, huku ukitazamiwa kuleta ushindani mkubwa, kutokana na maandalizi na wachezaji bora kwa timu zote 16, zinazosaka tiketi ya kupada daraja.
Licha ya Ligi hiyo kukua kwa kasi kutokana na aina ya wachezaji wakubwa na wazoefu ambao wamejiunga na klabu mbalimbali, ila zipo timu zilizowahi kushiriki Ligi Kuu Bara na sasa zinapambana kurejea tena, kama Mwanaspoti linavyozielezea.
AFRICAN SPORTS
Timu hii ya jijini Tanga ambayo hufahamika kwa jina la utani la ‘Wanakimanumanu’, inakabiliwa na kibarua cha kupambana kurejea tena Ligi Kuu, baada ya kikosi hicho kushuka daraja msimu wa 2015-2016, kilipomaliza nafasi ya 15 na pointi 26.
Katika msimu huo, ulikuwa ni rekodi pia kwa soka la Tanzania kushuhudia Mkoa wa Tanga ukishusha timu tatu daraja na mbali na African Sports, ila nyingine zilizoshuka zilikuwa ni Mgambo JKT na Coastal Union ambayo kwa sasa iko Ligi Kuu.
Msimu huo, Mgambo JKT ilimaliza nafasi ya 14 na pointi 28, ikishinda mechi sita, sare 10 na kupoteza 14, ikifunga mabao 24 na kuruhusu 36, huku Coastal ikiburuza mkiani na pointi 22, baada ya kushinda mechi tano, sare saba na kupoteza 18.
MBEYA KWANZA
Mbeya Kwanza inayodaiwa imeuzwa kwa Halmashauri ya Manispaa ya Tabora ikitokea Lindi ilipoweka kambi kwa msimu uliopita, ilishuka daraja msimu wa 2021-2022, ilipomaliza mkiani baada ya kikosi hicho kukusanya jumla ya pointi 25 tu kibindoni.
Msimu huo, Mbeya Kwanza, ilishinda mechi tano tu, sare 10 na kupoteza 15, ikifunga mabao 22 na kuruhusu 39, ikiungana na Biashara United iliyomaliza nafasi ya 15 na pointi 28, hivyo ina kazi kubwa ya kupambana ili kurejea tena Ligi Kuu Bara.
KAGERA SUGAR
Kagera iliyodumu katika Ligi Kuu Bara kwa miaka 20 tangu ilipoanza kushiriki 2005, ilishuka daraja msimu wa 2024-2025, baada ya kushinda mechi tano tu, sare minane na kupoteza 17, ikishika nafasi ya 15, baada ya kukusanya pointi zake 23.
Timu hiyo inayonolewa na aliyekuwa nyota wa Simba, Yanga na timu ya Taifa Stars, Juma Kaseja aliyewahi kuitumikia pia Kagera akiwa mchezaji na kocha wa makipa, ana kazi ya kukipambania kikosi hicho ili kirejee tena katika Ligi Kuu Bara.
TRANSIT CAMP
Kwa msimu wa 2024-2025, Transit ilimaliza nafasi ya 14 katika Ligi ya Championship na pointi 21, baada ya kushinda mechi tano, sare sita na kupoteza 19 kati ya 30 ilizocheza, ikifunga jumla ya mabao 19 na kuruhusu nyavu zake kutikiswa mara 50.
Baada ya kumaliza nafasi ya 14, Transit ikacheza mechi mbili za ‘Play-Off’ kusaka tiketi ya kubakia Championship na ilianza kwa kuitoa Kiluvya United kwa jumla ya mabao 3-2, kisha kuiondosha pia Rhino Rangers ya Tabora kwa jumla ya 4-1.
Kikosi hicho kilipanda rasmi Ligi Kuu msimu wa 2004-2005, kikiwa chini ya Kocha, Stephen Matata na mwaka 2005, timu hiyo ilimaliza nafasi ya tisa na pointi zake 30, ikishinda mechi saba, sare tisa na kupoteza 12, kati ya 28, iliyocheza.
Mwaka 2006, Transit Camp ikashuka daraja kwa kuburuza mkiani mwa timu 16 na pointi 20, baada ya kikosi hicho kushinda mechi tano, sare tano na kupoteza 20, kati ya 30 na inapambana ili kurejea tena katika ufalme wake uliozoeleka.
GEITA GOLD
Geita iliyoshuka daraja msimu wa 2023-2024, msimu wa 2024-2025 wa Ligi ya Championship ilimaliza nafasi ya nne na pointi 56, chini ya aliyekuwa Kocha Mkuu, Mohamed Muya na kushindwa kupanda Ligi Kuu Bara, baada ya kufeli mechi za ‘Play-Off’.
Timu hiyo ilicheza ‘Play-Off’ ya kupanda Ligi Kuu Bara dhidi ya Stand United ‘Chama la Wana’ iliyomaliza nafasi ya tatu na pointi 61 na kushuhudia ikiondoshwa kwa jumla ya mabao 4-2, baada ya sare nyumbani ya 2-2 kisha kuchapwa ugenini 2-0.
POLISI TANZANIA
Timu hiyo msimu uliopita wa 2024-2025, haukuwa mzuri sana baada ya kumaliza nafasi ya 10, katika Ligi ya Championship na pointi 33, ikishinda mechi nane, sare tisa na kupoteza 13 na safu ya ushambuliaji ilifunga mabao 44 na kuruhusu 33.
Kikosi hicho kinapambana ili kurejea tena Ligi Kuu Bara baada ya kushuka daraja msimu wa 2022-2023, kilipomaliza nafasi ya 15 na pointi zake 25, kufuatia kushinda mechi sita tu, sare saba na kupoteza 17, kikifunga mabao 25 na kuruhusu 54.
STAND UNITED
Stand United ‘Chama la Wana’, ilishuka daraja msimu wa 2018-2019, ikimaliza nafasi ya 19 na pointi 44, baada ya kikosi hicho chenye maskani yake Shinyanga, kushinda mechi 12, sare minane na kupoteza 18, kikifunga mabao 38 na kuruhusu 50.
Msimu uliopita, Stand ilimaliza ikiwa nafasi ya tatu na pointi 61, ambapo ilicheza ‘Play-Off’ ya kupanda Ligi Kuu Bara, ikianza kwa kuiondosha Geita Gold iliyomaliza ya nne na pointi 56, katika Ligi ya Championship kwa jumla ya mabao 4-2.
Baada ya Stand kuitoa Geita Gold, ikacheza ‘Play-Off’ nyingine na Fountain Gate iliyotolewa pia hatua hiyo na maafande wa Tanzania Prisons kwa jumla ya mabao 4-2 na kikosi hicho kilikwama kupanda baada ya kufungwa jumla ya mabao 5-1.
Kwa upande wa Fountain, ilimaliza nafasi ya 14 na pointi 29 katika Ligi Kuu msimu wa 2024-2025 na kukutana na Tanzania Prisons iliyomaliza ya 13 na pointi 31, kwenye mechi ya mtoano na kikosi hicho cha maafande kushinda jumla ya mabao 4-2.
KENGOLD
Baada ya msimu bora wa 2023-2024, mashabiki na wapenzi wa soka hususani wa Jijini Mbeya walitarajia KenGold ingeendeleza ilichokifanya katika Ligi ya Championship, japo baada ya kupanda daraja mambo yalikuwa ni tofauti na kurejea ilipotoka.
Kwa msimu wa 2023-2024, KenGold ilitwaa ubingwa wa Championship, ikiibuka kinara na pointi 70, ikiungana na Pamba Jiji ya Mwanza iliyomaliza nafasi ya pili na pointi 67, iliyorejea Ligi Kuu baada ya miaka 21, tangu iliposhuka mwaka 2001.
Licha ya kiwango bora ilichokionyesha Championship, ila KenGold ilishindwa kumudu presha za Ligi Kuu na kuburuza mkiani na pointi 16, ikishinda mechi tatu, sare saba na kupoteza 20, ikiungana na Kagera Sugar iliyomaliza ya 15 na pointi 23.