MTENJE: Kuna Pacome, halafu kuna Fei Toto
Muktasari:
- Wakati wengi wakiwa na mitazamo hiyo, mchezaji kiraka wa Geita Gold, Mtenje Albano ana mtazamo tofauti kabisa. Yeye anaamini kwamba kiungo wa Azam FC, Mtanzania Feisal Salum ‘Fei Toto’ ndiye mchezaji bora wa Ligi Kuu Bara msimu uliopita.
KUELEKEA mwisho wa msimu uliopita, kulikuwa na mijadala mikubwa kuhusu mchezaji anayestahili kushinda tuzo ya Mwanasoka Bora wa Msimu 2024-25 baadhi wakiona kiungo wa Simba, Jean Charles Ahoua anastahili, wengine wakiamini staa wa Yanga, Pacome Zouzoua ndiye MVP. Ni nani zaidi?
Wakati wengi wakiwa na mitazamo hiyo, mchezaji kiraka wa Geita Gold, Mtenje Albano ana mtazamo tofauti kabisa. Yeye anaamini kwamba kiungo wa Azam FC, Mtanzania Feisal Salum ‘Fei Toto’ ndiye mchezaji bora wa Ligi Kuu Bara msimu uliopita.
“Watanzania wengi wetu tuna roho mbaya, hatuthamini vya kwetu, lakini mimi nakiri na nitaendelea kusema kuwa Fei Toto ni mchezaji mzuri sana. Ana kila kitu kinachokamilisha sifa za mchezaji bora.
"Kwangu ndiye MVP wa msimu ulioisha pia ni mchezaji wa kuigwa na nyota wengine wanaocheza na hata wanaochipukia. Ipo siku mtakuja kuielewa hii kauli," anasema Mtenje.
Katika mahojiano maalumu na Mwanaspoti, mchezaji huyo wa zamani wa Fountain Gate ambaye sasa anakipiga katika Ligi ya Championship akitokea kwenye Ligi Kuu Bara, amefunguka mambo mbalimbali ikiwa ni pamoja na ndoto yake ya kuwa mwanamitindo.
PACOME? KUNA FEI
Wakati wadau na baadhi ya wachezaji wakikubali uwezo wa kiungo wa Yanga, Pacome wakimtaja kama profesa wa boli, kwa upande wa Mtenje anaona nyota huyo ni wa kawaida sana.
“Kila mmoja na namna anavyotazama mpira na kuuelewa. Mimi nikiamshwa usingizini na kuambiwa nimtaje mchezaji wangu bora katika Ligi Kuu, jina ni moja tu – Fei Toto. Navutiwa na uchezaji wake, ni mchezaji mzuri sana uwanjani. Hata hao wachezaji wa kigeni wanaocheza ligi wanatakiwa kujifunza vitu kutoka kwake.”
Mtenje anasema wachezaji wa kigeni wanaocheza ligi, ukimuondoa Fei Toto, pia wana kitu cha kujifunza kutoka kwake.
“Huyo Pacome ni mchezaji wa kawaida sana na hii kauli nilishawahi kuizungumza nairudia tena na wala sijawahi kujutia kuizungumza. Ni mchezaji wa kawaida mno,” anasema Mtenje ambaye anakipiga Geita Gold, akiamini timu yake itafanya vizuri msimu huu kutokana na usajili walioufanya.
COASTAL HADI KIFO
Coastal Union ni moja ya timu ambazo zimekuwa zikiibua vipaji na kuvisambaza kwenye timu nyingine za Ligi Kuu zikiwamo Yanga, Simba na Azam FC. Mfano mzuri ni mabeki Bakari Mwamnyeto anayekipiga Yanga na ni nahodha wa timu hiyo ya Jangwani, winga Abdul Suleiman ‘Sopu’ na beki wa kati Lameck Lawi, ambao wako Azam FC na Mtenje.
“Licha ya kupita timu mbalimbali za Ligi Kuu, hadi sasa nikipita timu nne, Coastal Union ndiyo timu iliyonitambulisha kwenye soka la ushindani na kunifanya nikajulikana na kuwa sehemu ya wachezaji wenye vipaji vikubwa. Coastal Union imenifanya nijenge nyumba, hivyo ndiyo kitovu changu cha mafanikio. Najivunia kupita kwenye timu hiyo na ndiyo timu ya maisha yangu. Hata ukinichana hapa mwilini kwangu basi damu ya 'The Fox' utaiona.
“Nimeitumikia Coastal Union kwa muda mrefu kuanzia timu ya vijana hadi nikapewa kitambaa cha unahodha. Nilifurahia maisha ndani ya timu hiyo, nilikuwa naaminiwa kwa kupata nafasi ya kucheza mara kwa mara. Pia kupewa kitambaa cha unahodha ilikuwa heshima kubwa sana kwangu.”
KAMBI POPOTE
Kiungo huyo anasema licha ya kutambulika zaidi akicheza nafasi ya kiungo, ana uwezo wa kucheza nafasi yoyote uwanjani kikubwa kocha akimpa jezi.
“Ninaweza kucheza nafasi yoyote. Ni kama askari aliye vitani, hawezi kukataa kisu na kuchagua panga. Anatumia silaha yoyote. Hivyo, kocha akiamua kunipanga beki wa kati, nacheza kwa sababu ni kazi yangu.
“Nacheza kiungo mkabaji, lakini muda mwingine kiungo mshambuliaji. Hii ndiyo maana halisi ya mchezaji na ndiyo maana kila timu ninayopata nafasi ya kusajiliwa napata nafasi kikosi cha kwanza. Sababu ni kutochagua nafasi ya kucheza. Kukiwa na kiungo bora nitacheza beki, kukiwa na beki bora nitapanda juu. Sichagui.”
MITINDO NAKO YUMO
Anasema soka ndilo limempa ajira, lakini kama asingekuwa mchezaji, angekuwa mwanamitindo – fani nyingine ambayo anaipenda na angeitumia kutangaza mitindo nje ya nchi.
“Kama siyo soka naamini ningekuwa mwanamitindo. Ni kitu kingine nakipenda zaidi ukiachana na soka ambalo limenipa ajira kupitia Coastal.
“Kucheza soka hakujakatisha ndoto yangu ya kuwa mwanamitindo. Ikitokea nikaamua kuachana na soka nitaibukia kwenye sanaa hiyo ya mitindo. Natamani kuwa bora kwenye sekta hiyo,” anasema kiungo huyo anayependa kuvaa vizuri na anatamani awe na mtu wa kumbunia mavazi.
THAMANI KUBWA, UWEZO MDOGO
Tanzania imejaaliwa vipaji vingi vikubwa na bora, lakini wachezaji wengi hawapewi thamani na kuaminiwa kama anavyothibitisha Mtenje, ambaye amekiri kuwa ubora wa wazawa ni mkubwa lakini hawaaminiwi.
“Mazoea yaliyopo kuanzia viongozi hadi benchi la ufundi ndiyo sababu kubwa inayoturudisha nyuma wachezaji wa ndani na kuwapa wageni kipaumbele. Kuna Mudathir Yahya, Fei Toto – wanafanya vitu vikubwa lakini hawaimbwi sana tofauti na inapotokea kitu kimefanywa na kina Pacome na Clatous Chama.
“Mimi naweza nikafanya kitu kikubwa leo, lakini hakipewi muda wa kuzungumzwa. Akifanya mchezaji wa kigeni, ataimbwa na kuzungumzwa sana. Hivyo tunaangushwa na viongozi na wadau wa soka. Mfano, kulikuwa na kina John Bocco kipindi hicho, alifanya makubwa sana lakini hapewi thamani kama kina Fiston Mayele ambao wamekuja Tanzania, wamecheza misimu miwili tu, lakini hadi sasa wanatajwa.”