Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Vipigo vikubwa hatua ya makundi CAFCL

Vipigo Pict

Muktasari:

  • Kupitia makala haya, Mwanaspoti inakuletea vipigo vikali vilivyotokea kwa baadhi ya timu mbalimbali katika michuano ya CAF kwenye hatua ya makundi ambavyo hadi leo hii vinabaki kumbukumbu kwa mashabiki na ni ngumu kusahaulika au kufutika.

WAKATI hatua ya makundi ya Ligi ya Mabingwa Afrika ikiisha na sasa ikisubiriwa tu michezo ya robo fainali, tumeshuhudia vipigo vikali na vya fedheha ambavyo vimetokea na kuacha simanzi katika historia ya michuano hiyo inayoendelea kubamba.

Kupitia makala haya, Mwanaspoti inakuletea vipigo vikali vilivyotokea kwa baadhi ya timu mbalimbali katika michuano ya CAF kwenye hatua ya makundi ambavyo hadi leo hii vinabaki kumbukumbu kwa mashabiki na ni ngumu kusahaulika au kufutika.


VP 02

TP MAZEMBE 8-0 CLUB AFRICAIN

Hiki ndicho kipigo kikubwa kinachoshikilia rekodi katika hatua ya makundi ya Ligi ya Mabingwa Afrika ambapo TP Mazembe ya DR Congo, ambao ni mabingwa mara tano wa michuano hiyo ilikitoa kwa Club Africain kutoka Tunisia, Februari 2, 2019.

Katika mchezo huo wa kundi C, uliifanya TP Mazembe kumaliza kinara wa kundi na pointi 11, ikifuatiwa na CS Constantine ya Algeria iliyomaliza na pointi 10 sawa na Club Africain, huku Ismaily SC ya Misri ikiburuza mkiani na pointi mbili tu.


VP 03

SIMBA 7-0 HOROYA AC

Simba ikihitaji tiketi ya kufuzu hatua ya robo fainali ilishusha kichapo kikali cha mabao 7-0, dhidi ya Horoya AC kutoka Guinea hivyo, kuingia katika historia ya vipigo vikali vya kihistoria vilivyowahi kutolewa kwenye michuano ya kimataifa.

Katika mchezo huo wa kundi C, uliopigwa Machi 18, 2023, ulishuhudia 'Mwamba wa Lusaka', Clatous Chama ambaye kwa sasa anaichezea Yanga akifunga mabao matatu 'Hat-Trick', na kuifanya kumaliza nafasi ya pili na pointi zake tisa kibindoni.

Raja Casablanca ya Morocco iliongoza na pointi zake 16, huku Horoya ikimaliza ya tatu na pointi saba wakati Vipers SC ya Uganda ilimaliza na pointi mbili, ambapo kwa msimu huo Simba ilishindwa kuwika na kutolewa tena hatua ya robo fainali.

Katika msimu huo, Simba ilitolewa na Wydad Casablanca ya Morocco kwa mikwaju ya penalti 4-3, baada ya kikosi hicho cha Wekundu wa Msimbazi kushinda bao 1-0, mchezo wa kwanza jijini Dar es Salaam, kisha mechi ya marudiano kuchapwa pia 1-0.


ASEC MIMOSAS 7-0 CR BELOUIZDAD

Hiki ni kipigo kingine kikubwa ambacho kinaendelea kuishi katika historia ya michuano ya CAF hatua ya makundi, ambapo ASEC ya Ivory Coast ilikitoa kwa CR Belouizdad ya Algeria, mchezo uliopigwa Uwanja wa Felix Houphouet Boigny Oktoba 7, 2001.

Katika mchezo huo wa kundi B, ulishuhudia Petro Atletico ya Angola ikiongoza na pointi 12, sawa na Al Ahly kutoka Misri, huku ASEC ikimaliza ya tatu na pointi zake 10, wakati CR Belouizdad iliburuza mkia kipindi hicho na pointi yake moja tu.


VP 04

RAJA CASABLANCA 6-0 YANGA

Usishangae kuona kichapo hicho ilichokutana nacho Yanga, ilikutana na kipigo hicho katika mchezo wa hatua ya makundi ya Ligi ya Mabingwa Afrika dhidi ya Raja Casablanca ya Morocco, mechi iliyopigwa Uwanja wa Mohammed V, Septemba 18, 1998.

Katika mchezo huo wa kundi B, ulishuhudia ASEC Mimosas ya Ivory Coast ikiongoza na pointi zake 13, ikifuatiwa na Manning Rangers ya Afrika Kusini iliyokuwa na 10, Raja Casablanca ikiwa ya tatu na pointi nane, huku Yanga ikimaliza na pointi mbili tu.

Kwa wakati huo, mechi ya kwanza tu Yanga ilichapwa mabao 6-0 na Raja Casablanca, ikachapwa 3-0 na ASEC Mimosas kwenye Uwanja wa Uhuru, kisha ikaenda Afrika Kusini kupambana na Manning Rangers na kuambulia kichapo kingine cha mabao 4-0.

Baada ya hapo ikapoteza ugenini 2-1 dhidi ya ASEC Mimosas, 1-1 na Manning kisha sare ya mabao 3-3 na Raja Casabalanca kwenye Uwanja wa Uhuru na kumaliza michezo yake sita ya hatua ya makundi ikiwa imefunga mabao matano tu na kuruhusu 19.

Baada ya hapo timu hiyo ikachukua miaka 25, kufika tena hatua ya makundi ya Ligi ya Mabingwa Barani Afrika ilipofanya hivyo msimu wa 2023–2024, ilipomaliza nafasi ya pili kundi D, nyuma ya mabingwa wa kihistoria wa michuano hiyo Al Ahly ya Misri.

Katika kundi hilo, Yanga ilimaliza na pointi zake nane sawa na CR Belouizdad ya Algeria iliyoshika nafasi ya tatu, huku Medeama SC ya Ghana ikiburuza mkiani na pointi nne, wakati Al Ahly ilikuwa kinara ikijikusanyia jumla ya pointi zake 12.

Msimu huo, Yanga ilijiandikia rekodi nyingine ya kibabe ambapo ilifika hadi hatua ya robo fainali ya michuano hiyo kisha kutolewa kwa penalti 3-2 na Mamelodi Sundowns ya Afrika Kusini, baada ya timu hizo kutoka suluhu (0-0) mechi zote mbili.


ENYIMBA 6-0 NYASA BIG BULLETS

Enyimba ya Nigeria iliyojizoelea umaarufu mkubwa katika michuano hii, iliichapa Bakili Bullets ambayo kwa sasa ni Nyasa Big Bullets ya Malawi mabao 6-0, kwenye mchezo huo wa kuvutia na wa kusisimua wa kundi A, uliopigwa Julai 25, 2004.

Katika kundi hilo, Etoile Sportive du Sahel ya Tunisia iliongoza na pointi zake nane, ikifuatiwa na Enyimba iliyomaliza na pointi sita, Africa Sports d'Abidjan ya Ivory Coast ilimaliza ya tatu na pointi tano sawa na Big Bullets iliyoburuza mkia.


VP 05

SIMBA 6-0 JWANENG GALAXY

Simba ikiwa kwenye Uwanja wa Benjamin Mkapa jijini Dar es Salaam, ilishusha kipigo hicho kikali katika mchezo wa mwisho wa hatua ya makundi dhidi ya Jwaneng Galaxy ya Botswana, ambao uliifanya kushika nafasi ya pili na kufuzu robo fainali.

Katika mchezo huo wa kundi B uliopigwa Machi 2, 2024, uliifanya Simba kumaliza nafasi ya pili na pointi tisa sawa pia na Wydad Casablanca ya Morocco iliyomaliza ya tatu, nyuma ya vinara ASEC Mimosas ya Ivory Coast iliyomaliza na pointi 11.

Jwaneng iliburuza mkia na pointi zake nne tu katika michezo sita iliyocheza, ambapo msimu huo Simba iliishia hatua ya robo fainali baada ya kutolewa na Al Ahly ya Misri kwa jumla ya mabao 3-0, ikichapwa nyumbani bao 1-0, kisha ugenini 2-0.


CR BELOUIZDAD 6-0 STADE D'ABIDJAN

Hiki ni kipigo ambacho kimetokea msimu huu ambapo CR Belouizdad ya Algeria ilikitoa dhidi ya Stade d'Abidjan ya Ivory Coast, katika mchezo wa mwisho wa kundi C wa Ligi ya Mabingwa Barani Afrika hatua ya makundi uliopigwa Januari 18, 2025.

Licha ya ushindi huo ila CR Belouizdad ilimaliza ya tatu na pointi tisa, wakati Stade d'Abidjan iliburuza mkia na pointi moja tu, huku Orlando Pirates ya Afrika Kusini ikiongoza na pointi 14, ikifuatiwa na Al Ahly ya Misri iliyomaliza na 10.


VP 01

PYRAMIDS FC 6-0 DJOLIBA AC

Djoliba AC ya Mali ilikumbana na kichapo hicho katika mchezo wa mwisho wa makundi ya Ligi ya Mabingwa Afrika uliopigwa Januari 18, 2025, ambapo matajiri wa Misri, Pyramids FC ilijihakikishia kumaliza nafasi ya pili katika kundi lake la D.

Katika kundi hilo, Pyramids FC ilimaliza na pointi 13 ambazo ni sawa na vinara Esperance Sportive de Tunis ya Tunisia, huku G.D. Sagrada Esperanca ya Angola ikimaliza ya tatu na pointi tano, wakati Djoliba AC ilimaliza na pointi mbili tu.