Prime
Ununuzi holela wa klabu si afya kwa soka
KLABU nyingi za soka huko Brazil hivi sasa zinapitia mageuzi makubwa ya umiliki na uendeshaji, zikitoka katika muundo wa zamani wa kuwa taasisi zisizoendeshwa kibiashara na kubadilika kuwa mashirika au kampuni za kibiashara.
Hii ni baada ya bunge la nchi hiyo ya Amerika ya Kusini kupitisha sheria namba 14193/21 ya mwaka 2021 ambayo ililenga kuboresha uendeshaji na usimamizi wa kifedha kwa klabu za Brazil ambayo imejaliwa kuwa na vipaji vya soka.
Wakati mahitaji yalikuwa makubwa wakati zikiendeshwa kwa mtindo wa zamani, klabu zilijikuta katika dimbwi la madeni yaliyotishia uhai wake na pia ushiriki katika mashindano mbalimbali, huku klabu za barani Ulaya zikijichotea wachezaji kwa bei nafuu.
Lakini wanasheria wawili, Rodrigo Monterro de Castro na Jose Fransisco Manssur walifanya utafiti wao kuangalia mfumo wa biashara ya soka kwa kulinganisha na wa nje na mwaka 2019 Seneta Rodrgo Pacheco aliwasilisha muswada bungeni. Na miaka miwili baadaye ukapitishwa kuwa sheria.
Hii ni sheria maarufu inayoitwa Sociedade Anonima du Futebol (SAF), ambayo inageuza uendeshaji wa klabu kuwa wa mfumo wa mashirika makubwa (corporate organisations), ambayo humilikiwa na wanahisa na kuongozwa na bodi ya wakurugenzi inayowaajiri watendaji wakuu.
Sheria hiyo inazisaidia klabu kuongeza mtaji kutokana na kuvutia wawekezaji wa ndani na nje wanaonunua hisa za umiliki, inaboresha uongozi kwa kulazimisha viongozi wawe na uwazi na uwajibikaji.
Klabu kama Palmeiras, Cruzeiro, Botafogo, Vasco da Gama, Bahia, Sao Paulo na Flamengo zimeshaamua kuachana na mfumo wa zamani wa kutojiendesha kibiashara.
Magwiji wa zamani wa soka wa nchi hiyo ya Brazil, Edson Arantes maarufu kama Pele na Zico ndio walikuwa wa kwanza kujaribu kufanya mageuzi ya umiliki na uendeshaji wa klabu za soka, lakini hawakupata mafanikio sana zaidi ya kuwazindua wengine.
Mfalme huyo wa soka duniani aliibuka na Sheria ya Pele mwaka 1998, wakati Zico alijaribu mwaka 1993. Pele alijaribu kuboresha sheria ya Zico, lakini klabu zikaamua kubakia na mfumo wa zamani.
Sheria ya SAF imebadili mtazamo wa wawekezaji na viongozi wa klabu na sasa nyingi zinaanza kufuata mageuzi hayo ili zijiendeshe kibiashara na kuvutia wawekezaji zaidi.
Klabu za Simba na Yanga zinajaribu kufanya mageuzi hayo, lakini kwa njia ambayo ni viongozi tu wanaelewa na kibaya zaidi ni kama zilishajiwekea kuwa mfanyabiashara fulani ndio atanunua hisa nyingi na kuwa na sauti kubwa.
Kwa Simba ni kama imeshamaliza mageuzi hayo, licha ya kukumbana na kikwazo cha kisheria hadi sasa. Hata hivyo, tayari mwekezaji anaonekana kufanya uamuzi mkubwa, huku chombo kilichoundwa kwa ajili ya kumiliki asilimia 51 ya hisa, yaani Simba Sports Club Company kikiwa hakionekani kabisa na kilishasimamishwa na Kamisheni ya Ushindani (FCC) kuchukua mamlaka ya Simba SC.
Yanga ndio imetangaza thamani yake, ikiwa ni sehemu ya mchakato wa kuanza kuuza hisa za klabu. Kanuni zinataka asilimia 49 ya hisa ziuzwe kwa wawekezaji zaidi ya mmoja.
Wakati Simba na Yanga zikihangaika na muundo na ukamilishaji wa mchakato wa mageuzi, kwingineko klabu zinauzwa na kununuliwa kama njugu. Na si hivyo tu, zikishanunuliwa zinahamishwa kutoka maeneo zilikopatia umaarufu hadi kufikia Ligi Kuu au Ligi ya Championship.
Taarifa za wiki iliyopita zilidai kuwa mdhamini wa vifaa wa Yanga, GSM ana mpango wa kuinunua Tabora United, ambayo awali ilikuwa inaitwa Kitayosce, ikiwa imeanzishiwa mkoani Kilimanjaro 2018 kabla ya kununuliwa na Yusuf Kitumbo na kuhamia Dar es salaam.
Klabu ya Singida Black Stars ya mkoani Singida ilipachikwa jina hilo kutoka klabu ya Ihefu FC ya mkoani Mbeya ambayo ilianzishwa mwaka 2016 na kupanda Ligi Kuu mwaka 2020.
Kwa wanaokumbuka timu ya DTB iliyoanzishwa mwaka 2010 na baadaye ikabadilishwa kuwa Singida Big Stars ilipopanda Ligi Kuu na baadaye ikaitwa Singida Fountain Gate mwaka 2023 baada ya kuungana na Fountain Gate katika biashara ambayo haikueleweka kwa wengi na hivi sasa inaitwa Fountain Gate, ikiwa imehamishia makazi yake mkoani Manyara.
Pamba Jiji imechukua jina hilo kutaka kurudisha mapenzi ya wakazi wa mkoa wa Mwanza kwa klabu baada ya ile ya zamani, Pamba FC, iliyokuwa ikimilikiwa na Bodi ya Pamba kutoweka, hasa baada ya serikali kubadili sera zake za kiuchumi.
Ukiacha klabu hizo na nyingine zilizofika Ligi Kuu kwa kununua klabu nyingine za wanachama zilizokosa uwezo wa kifedha, klabu zenye historia katika ligi hiyo ya juu nchini ni Simba, Yanga, Coastal Union, Namungo na Azam FC ambazo ni za wananchi, huku timu nyingine Prisons, Mashujaa, KMC, Dodoma Jiji, JKT Tanzania -- zikimilikiwa na taasisi za serikali.
Ukiangalia klabu hizo zote utaona kuna makundi matatu; klabu za wanachama, klabu za watu au kampuni binafsi na klabu za taasisi za serikali, ambazo zinazidi kuingia kwenye mpira tofauti ilivyokuwa awali kabla ya mabadiliko ya sera za kiuchumi wakati mashirika mengi ya serikali kama bima, benki, viwanda na bodi zilipokuwa zikimiliki klabu za michezo.
Uwezekano wa klabu za wananchi kutoweka ni mkubwa kwa kuwa zinapata shida kukabiliana na gharama za kiuendeshaji kutokana na mfumo wake kutokuwa rafiki kwa wawekezaji. Baadhi zinapata msaada kutokana na hekaheka za wakuu wa mikoa na baadhi wafadhili.
Hii si afya kwa mpira wa miguu. Kuwepo na klabu nyingi zinazomilikiwa na taasisi za serikali si afya kwa mpira wa miguu kwa kuwa utawala unapobadilika unaweza kuja mpya ukiwa na sera kama zile za kubana matumizi na sehemu ya kwanza ikawa ni michezo.
Ni muhimu sana kwa mamlaka za soka, wachumi, wabunge na wanasheria kuanza kuliangalia suala hili kwa jicho pana sana. Tumeona Brazil ni wanasheria waliojitwisha jukumu la kufanya utafiti wa uendeshaji na umiliki wa klabu na baadaye matokeo ya utafiti wao kuchukuliwa na wabunge waliopeleka muswada wa kubadili sheria.
Na wanasheria hao walipata wazo kutoka kwa magwiji wa zamani wa soka nchini Brazil, Pele na Zico na wakaboresha juhudi zao hadi kuzalisha sheria ya SAF.
Tunahitaji jitihada kama hizo. Tunahitaji jicho kama hilo la kuona tatizo katika uendeshaji na umiliki wa klabu na kutengeneza sheria ama kanuni za umiliki ili zitumiwe na klabu katika mageuzi yao.
Na hilo lilishasemwa na FCC wakati wa mchakato wa mabadiliko ya Simba walipoeleza kuwa wasimamizi wa mpira wa miguu hawana budi kutengeneza muongozo wa umiliki wa klabu ili utumiwe na klabu kufanya mageuzi.
Haya mabadiliko ya wamiliki yanaoendeshwa kiholela yanapotezea historian a uhalisia wa klabu na hivyo nyingi kuwa mpya na kupata shida kuvutia mashabiki. Takwimu zinaonyesha wastani wa mahudhurio ya mashabiki viwanjani kwa baadhi ya klabu kuwa watu 900. Hii si afya kwa taifa ambalo lina wendawazimu wa mpira wa miguu.
Bila kuongoza mageuzi ya uendeshaji na umiliki wa klabu, nchi itabakia na klabu mbili tu zenye mashabiki wengi, Simba na Yanga. Nyingine zitakuwqa ni zile zinazojaribu kukumbushia zama za klabu maarufu, kama ilivyo kwa Pamba, ama kutafuta mapenzi kwa wakazi wa mkoa, kama ilivyo kwa Tabora United au Singida Black Stars.
Tunahitaji kufikiria mabadiliko zaidi yay ale ya kanuni za Ligi tu. Huu ununuzi holela wa klabu za ligi si afya kwa mpira wa miguu. Tunahitaji muundo utakaovutia wawekezaji, kuimarisha uongozi na uwazi na kuingizaa uwajibikaji na zitakazodhibiti klabu kuhamisha makazi kiholela.