Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

UCHAMBUZI: Uzalendo ni muhimu, unahitajika hata katika soka

Muktasari:

Neno hilo la uzalendo lilitumika vibaya katika soka na kupoteza maana halisi ya neno uzalendo ambalo tafsiri yake inabeba hisia ya kujali na kuthamini nyumbani kwanza kuliko nje kwa kuzingatia sheria. Lakini ilivyotumika ni pale waamuzi walipopindisha sheria za soka kila walipochezesha mechi katika mikoa hiyo tofauti na wanapokuwa mikoa mingine.

Uzalendo si neno geni kwa mwa wanamichezo, hasa mashabiki wa soka. Neno hilo limekuwa likizungumzwa na kutumiwa mara nyingi ingawa utumikaji wake katika soka huwa hauzingatii maana halisi ya neno hilo na badala yake kutumika vibaya.

Wakati nacheza soka la ushindani kipindi ambacho Ligi Kuu ilikuwa ikiitwa Ligi Daraja la Kwanza, baadhi ya mikoa ilipewa sifa ya kuwa na uzalendo pale timu za mikoa hiyo zilipokuwa zikicheza viwanja vya nyumbani.

Timu zilizokuwa zikienda nyumbani kwa timu hizo zilizosifika kwa uzalendo ziliishia kulalamikia uzalendo zilizokutana nao katika mechi zao, wakimaanisha kuonewa na waamuzi na kufanyiwa vitimbi.

Mfano mikoa iliyotajwa kuwa kinara wa uzalendo ni Lindi iliyokuwa na timu ya Kariakoo-Lindi, Rukwa na Ujenzi Rukwa nk.

Neno hilo la uzalendo lilitumika vibaya katika soka na kupoteza maana halisi ya neno uzalendo ambalo tafsiri yake inabeba hisia ya kujali na kuthamini nyumbani kwanza kuliko nje kwa kuzingatia sheria. Lakini ilivyotumika ni pale waamuzi walipopindisha sheria za soka kila walipochezesha mechi katika mikoa hiyo tofauti na wanapokuwa mikoa mingine.

Upo uzalendo mwingine wa miaka hiyo ambao ndio ninaouzungumzia uliokuwa na mchango mkubwa katika kukuza soka na kuongeza ushindani ambao nadhani hata sasa ukiendelezwa unaweza kuwa na tija kubwa.

Uzalendo huu ni ule ulioanzia kwa timu za mikoani zilipokuwa zikitumia wachezaji wengi wanaotoka mikoa hiyo kuliko kuchukua wa mikoa mingine.

Hiyo ilifanya wachezaji hao wa kuwa na uzalendo uliojengeka sambamba na mapenzi kwa timu za mikoa yao. Mwishoni mwa miaka ya 1980 nakumbuka RTC Kigoma ilipopanda daraja na kucheza Ligi Daraja la Kwanza, ilikuwa na wachezaji wengi wa ndani ya mkoa wa Kigoma waliokuwa mhimili wa timu hiyo na kuifanya kuwa moja ya timu imara na tishio kipindi hicho.

Kina Ramadhani Bilal, Yusufu Mfaume, Khalid Rehani, Mavumbi Omari, Muhoza Bonga, Wastara Baribari na hata Abeid Mziba na Makumbi Juma walikuwa na unasaba na mkoa huo hivyo kuwa wazalendo kwa mkoa na hivyo kukubali kupambana pale timu ya mkoa wao ilipohitajika kufanya hivyo.

Utaratibu huo ulikuwa ukitumika pia kwa klabu za Pamba- Mwanza ya kina Juma Amir Maftah, Beya Simba, Hussein Marsha, George Gole na wengine, huku ukienda Tukuyu  Stars ya Mbeya kina Assanga Aswile, Mwakibibi, Mwasimanga na wengine wengi.

Ukienda Milambo ya Tabora utakutana na Mikidadi Jumanne, Dionis Paul, Abbas Mchemba, Shaaban Moshi, Mrisho Moshi, Iddi Moshi na wengineo. Utaratibu huu ulijenga ushindani wa asili kwani hata mashabiki walishabikia timu zao, walijiona nao ni sehemu ya timu hiyo kwa kuwa zipo mitaani mwao na hata wachezaji waliokuwa wakizichezea ni wale walikuwa wakiishia nao mitaani tangu utotoni mwao.

Imani yangu ni kuwa timu zinazotoka nje ya Dar es salaam kama zitaelekeza mipango yao ya kutumia wachezaji wanaotoka maeneo au mikoa hiyo, upo uwezekano mkubwa kukaongezeka ufanisi kupitia dhana ya uzalendo ambao kwa kiasi kikubwa utasaidia hata kupunguza matumizi ya fedha za usajili zinazotumika sasa.

Utakuwa msaada mkubwa kwa timu zisizo na uwezo mkubwa kifedha. Na utaratibu huu si mgeni kwa wafuatiliaji wa soka, hata Hispania kuna timu ambazo zimetengeneza na kutekeleza sera ya kutumia wachezaji wanaotoka maeneo au mikoa yao tu na si nje ya mikoa hiyo na timu hizi zimefanikiwa kwa kiasi kikubwa. Kwa mfano Hispania kwenye La Liga kuna Atletico Bilbao ambayo ni kati ya timu tatu kubwa nchini humo inaongozwa na sera ya CANTERA ambayo inatamka kuwa timu hiyo isajili wachezaji wanaotoka au waliozaliwa Jimbo la Basque tu na si nje ya hapo. Sera hiyo hiyo imeifanya timu hiyo kushiriki La Liga na kuweka historia kuwa kati ya waasisi wa ligi hiyo, pia ni miongoni mwa timu tatu ambazo hazijawahi kushuka daraja tangu ligi hiyo ilipoanza rasmi mwaka 1929. Hivyo haitakuwa kitu kigeni iwapo itatokea timu yoyote ya mkoani ikawa na sera kama hiyo kwani itasaidia pia kuwahakikishia wachezaji wanaotoka mkoa huo kucheza na kupata nafasi ya kuonekana.