UBISHI WA MZEE WA KALIUA: Unaijua Yanga au unaisikia?

YANGA wakatangaza kuongeza mikataba na wachezaji wawili raia wa Jamhuri ya Kidemokrasi ya Congo, Yanick Bangala na Djuma Shabaan. Bangala amekuwa mchezaji bora wa msimu. Bila shaka Djuma ndiye beki bora wa Yanga kwa msimu uliomalizika.

Wanastahili kuongeza muda wa kuitumikia Yanga. Imewachukua Yanga miaka kadhaa kuwapata wachezaji wa aina ya Bangala na Djuma. Imewachukua miaka kadhaa kuitengeneza timu waliyo nayo sasa. Timu iliyosheheni mastaa wanaostahili kuicheza Yanga.
Ubingwa hawakuuchukua kwa bahati mbaya, ni hawa mastaa waliowakusanya wamewasaidia kutwaa ubingwa akiwemo Djuma Shabaan na Yanick Bangala. Nafikiri hawa ndio mastaa wawili wanaofuata Yanga baada ya Fiston Mayele. Labda baada yao ndio wanafuata kina Feisal Salum 'Fei Toto', Djigui Diarra, Khalid Aucho, Salum Abubakar 'Sure Boy' na wengineo. Wamekuwa wachezaji muhimu sana kwa Yanga kwa msimu uliomalizika.
Djuma ni beki wa kisasa anayeweza kushambulia sawa tu na anavyoshiriki kwenye ulinzi. Bangala ni mchezaji hodari anayeweza kucheza beki ya kati sawa tu na anavyocheza kiungo mzuiaji. Huwapati sana wachezaji aina ya Bangala. Huwapati sana mabeki aina ya Djuma. Yanga wamegundua hili na kuamua kuwaongeza mikataba mapema.
Yanga wanafahamu kwamba ingefika mwisho wa msimu wangeteseka kuwashawishi kusaini mikataba mipya kwa sababu ya upinzani ambao wangeupata kutoka kwa wapinzani wao wa karibu, Simba. Mara nyingine huwa Simba na Yanga hawajali sana kama hawamhitaji mchezaji.
Huwa wanachohitaji ni kumkomoa tu mpinzani na kutamba kwamba mchezaji yeyote wanayemhitaji wanaweza kumpata. Simba wanaweza kumhitaji Djuma Shaban ili tu kuwakomoa Yanga, licha ya kuwa na Shomari Kapombe bora sana. Yanga wanaweza kumhitaji Aishi Manula licha kuwa na Djigui Diarra asiyekuwa na tatizo lolote. Kwa hiyo wamefanikiwa kuukwepa usumbufu wa Simba kuwaongezea mikataba mapema.
Lakini hapo ufahamu kwamba Bangala na Djuma hawajaongeza tu mikataba kirahisi. Lazima pesa imetumika kuwashawishi. Kwanza kuna ada ya usajili. Hii inaitwa ‘signing on fee’, lakini pia lazima wamelazimika kuwapandishia mishahara. Kwa hiyo Djuma na Bangala watakunja mishahara mikubwa tofauti na ile waliyokuwa wanachukua mwanzo. Lakini hapo tunaweza kuwapongeza Yanga kwa kuleta utulivu mapema katika timu yao. Hakutakuwa na stori za Bangala na Djuma kuondoka mwisho wa msimu.
Mpaka sasa wapo watu wawili ambao wanaweza kuwasumbua zaidi mwisho wa msimu. Wa kwanza ni mlinda mlango wao na mfungaji wao bora wa msimu uliomalizika, Fiston Mayele. Dirisha hili tu wamesumbuliwa na stori za Mayele kujiunga na miamba ya Afrika Kusini, Kazier Chiefs.
Hayo yametokea wakiwa na mkataba hai na Mayele. Vipi mkataba wake utakapokuwa unaelekea ukingoni? Kumbuka mchezaji ana haki ya kuanza mazungumzo na klabu nyingine anapobakiza miezi sita katika mkataba wake. Kama Yanga wataruhusu mkataba wa Mayele ufike huko watateseka sana kumbakiza Mayele.
Nafikiri Yanga hawatakubali msimu ufike mbali kabla hawajamalizana na Mayele. Inawezekana Yanga hawana wasiwasi na Djigui Diarra kwa sababu wanawatazama hali halisi na kuliona lango la Simba likiwa salama na Aishi Manula. Hawaoni ni kwa jinsi gani Simba wanaweza kumtamani Diarra.
Hapohapo wanawatazama Azam na kuona jinsi walivyofanya usajili mkubwa dirisha hili ikiwa ni pamoja na kuimarisha lango na kuamini kwamba hawawezi kurejea kwa Diarra mwisho wa msimu. Ndiyo sababu Yanga hawana wasiwasi na kipa wao.
Kando yao labda ni Khalid Aucho ambaye mkataba wake unafarikia mwisho wa msimu. Huyu Yanga hawana wasiwasi naye kabisa na jina lake linaweza kuwekwa katika kilengeo kwamba nafasi yake ampishe mtu.
Kumbuka Yanga wamemuongeza kiungo wa kimataifa wa Burundi, Gael Bigirimana katika eneo lake na hapohapo tayari wana Sure Boy ambaye amewapa swali gumu makocha tangu atue kutoka Azam. Achilia mbali Zawadi Mauya ambaye Yanga wakienda katika kiwanja chochote kigumu jina lake linakuwa la kwanza katika karatasi ya timu.
Yanga wanaweza kufika mwisho wa msimu na kufikiria kumchinjilia mbali Aucho licha ya uwezo wake na utulivu aliouleta katika safu ya kiungo. Ndiyo maisha ya soka yalivyo. Aucho anaweza kujikuta anaondoka nchini pamoja na Heritier Makambo na Jesus Moloko ambao wanahitaji muujiza mkubwa kupewa kandarasi mpya Yanga.