Uamuzi wa kumtimua refa Coote utupe somo

Muktasari:
- Refa huyo, ambaye katika siku zake za mwisho alikuwa akifanya kazi ya refa msaidizi wa video (V.A.R) amefukuzwa kazi baada ya video kusambaa mitandaoni ikimuonyesha akitoa maneno yanayoonekana kukiuka maadili dhidi ya kocha wa zamani wa Liverpool, Jurgen Klopp.
KAMPUNI ya Waamuzi wa Mechi za Kulipwa (PGMOL), chombo kinachosimamia waamuzi wa mpira wa miguu nchini England, imemfukuza kazi refa David Coote baada ya kumfanyia uchunguzi wa kina kuhusu vitendo vyake.
Refa huyo, ambaye katika siku zake za mwisho alikuwa akifanya kazi ya refa msaidizi wa video (V.A.R) amefukuzwa kazi baada ya video kusambaa mitandaoni ikimuonyesha akitoa maneno yanayoonekana kukiuka maadili dhidi ya kocha wa zamani wa Liverpool, Jurgen Klopp.
Maneno yake yanahusishwa na mechi aliyochezesha kati ya Liverpool na Burnley iliyofanyika Julai mwaka 2020. Mechi hiyo iliisha kwa sare ya bao 1-1 na Klopp akalalamikia kitendo cha Coote kutowaonyesha kadi wachezaji wa Burnely kila walipowachezea rafu wachezaji wake.
Refa huyo pia aliwahi kujikuta matatizoni baada ya video nyingine kumuonyesha akinusa unga mweupe, ikimaanisha alituhumiwa kutumia dawa wa kulevya, ingawa alikanusha tuhuma hizo.

Mbali na uchunguzi wa tukio lililosababisha atimuliwe, refa huyo pia alituhumiwa kujadili suala la kumuonyesha mchezaji kadi ya njano kabla na baada ya mechi ya Leeds na West Brow mwaka 2019, ingawa alikanusha tuhuma hizo.
Gazeti la The Sun lilihusisha majadiliano hayo na kadi ya njano aliyoonyeshwa beki wa Leeds, Ezgjan Alioski. Haikusemwa kama Coote alinufaika kifedha na kadi hiyo lakini baadaye ilithibitika kuwa kadi hiyo ilikuwa halali.
PGMOL ilianza uchunguzi wa kwanza Novemba 13 ikisema tuhuma zimekuwa nzito baada ya picha kuzagaa zikimuonyesha akivuta unga unaodhaniwa kuwa ni dawa za kulevya. Uchunguzi zaidi ukaanzishwa Novemba 27 baada ya tuhuma hizo za kujadili kadi ya njano kabla na baada ya mechi.
Nimejaribu kuweka picha kamili ya matukio ya Coote kuwapa taswira nzuri ya jinsi waamuzi wanavyoweza kushughulikiwa kimaadili kukomecha vitendo ambavyo vinachafua mchezo wa mpira wa miguu au fani ya uamuzi.
Suala la Coote halikuamuliwa na watu wachache waliokaa mezani baada ya raundi nzima ya Ligi Kuu, bali lilihitaji jopo la watu waliopewa ushahidi wa kutosha kuhusu tuhuma zilizoko mezani.
Ilibidi hadi Coote mwenyewe akiri kwamba video iliyosambaa ni yake, ingawa akasema hakumbuki alichoongelea, kitu kinachoonyesha alitaka kukwepa kutetea alichokisema.
Katika mchezo ambao kasoro zilizobatizwa jina la “makossa ya kibinadamu”, ni lazima kuweka na hatua stahiki za kurekebisha hali hiyo na ionekane kuwa ni kweli hatua zimechukuliwa na zinalenga kukomesha vitendo hivyo.
Na lazima kuwe na chombo sahihi cha kushughulikia makossa hayo na fani nzima ili kuwe na maamuzi sahihi na yanayolenga kuilinda fani.
PGMOL ni chombo huru kilichoundwa na Ligi Kuu ya England (Premier League) kwa ajili ya kusimamia waamuzi na kwa sababu mpira nchini Uingereza ni kiwanda, chombo hicho kinaajiri waamuzi, kinafanya mafunzo, kinawapangia mechi na mambo mengine muhimu.
Hii inazuia siasa za mpira na nyinginezo kujipenyeza katika mchezo na kuvuruga ukuaji wa fani.

Tangu PGMOL ianzishwe imekuwa ikiwajibika kwa makosa yote ya waamuzi, ikiwa ni pamoja na kutoa ufafanuzi wa uamuzi unaoonekana kuwa una makosa na kubuni mbinu za kuboresha uamuzi na pia kuwezesha mashabiki kujenga imani na watu waliomo kwenye fani hiyo.
Kwa sasa mwenyekiti wake ni Martin Glenn, ambaye alikuwa Ofisa Mtendaji Mkuu wa Chama cha Soka cha Engand (FA).
Kutokuwa na kamati imara ya waamuzi kumesababisha waamuzi wengi kuadhibiwa kisiasa na bila ya uchunguzi wa kina na wako waliokaa nje ya mchezo kwa miaka miwili na wapo waokaa miezi michache na wapo wanaopumzishwa mechi kadhaa.
Hatujakuwa na uchunguzi wa kina wa “makossa ya kibinadamu” kama ni kweli ya kibinadamu au yanafanyika kwa majadiliano ya waamuzi na wahusika kabla na baada ya mechi.
Hatujafanya uchunguzi wa kina kujua ni makosa gani yanayojirudiarudia na dawa yake inaweza kuwa nini kwa kutumia uzoefu wa nchi nyingine zinazofanya vizuri kiuamuzi.
Hivi sasa kuna tuhuma kwamba kuna vijana wameajiriwa na klabu au matajiri kwa ajili ya kutumiwa kuhonga waamuzi kwa kuwa ni vigumu kwa macho ya sheria za mpira kuwaona na kuwaadhibu, huku rushwa ikiwa ni siri kubwa kati ya mtoaji na mpokeaji.
Haya yote yakifanyiwa uchunguzi wa kina ndipo majibu ya waamuzi yanapokuwa ya ajabu kama ambavyo Coote alijibu kuwa “hakujua alichozungumza” baada ya kuulizwa kama video iliyosambaa ni yake halisi au imetengenezwa.
Majibu kama hayo yanaweza kuwa mengi kama wahusika watakuwa wakali kushughulikia “makosa ya kibinadamu” ambayo yamegeuzwa kitu cha kawaida kwa kuwa hakuna chombo kinachowajibika kwa makosa hayo zaidi ya waamuzi kufungiwa na kurejeshwa.