Prime
Uamuzi unaanzia hapa
Uamuzi unaanzia hapa raundi ya 27 wakati Ligi Kuu Bara inaendelea leo Jumatano Juni 24, 2026 kwa kuchezwa mechi nane ambazo zote zitaanza saa 10:00 jioni, huku kukiwa na Dabi ya Dar es Salaam kati ya wenyeji Yanga dhidi ya Azam.
Dabi hiyo inachezwa Uwanja wa New Amaan Complex uliopo Zanzibar, huenda ikatukumbusha kile kilichotokea mara ya mwisho timu hizo kukutana hapo ambapo ilikuwa nusu fainali ya Kombe la Muungano, Aprili 25, 2026, Yanga ilishinda 2-1.
Kwa msimu huu, hii itakuwa mara ya tatu timu hizi zinakutana visiwani hapa baada ya awali kucheza fainali ya Kombe la Mapinduzi 2026 kwenye Uwanja wa Gombani uliopo Pemba, kisha nusu fainali ya Kombe la Muungano 2026 kwenye Uwanja wa New Amaan Complex, Unguja. Zote Yanga ilishinda.
Lakini kwa ujumla, msimu huu itakuwa mara ya tano, Yanga ikishinda mbili na Azam moja ya nusu fainali ya Kombe la Shirikisho la CRDB, huku ile ya ligi mzunguko wa kwanza matokeo yakiwa 0-0.
Hata hivyo, Yanga itakuwa na nafasi ya kulipa kisasi baada ya siku tatu nyuma kutoka kufungwa 3-2 na Azam katika nusu fainali ya Kombe la Shirikisho la CRDB, mechi iliyopigwa Juni 21, 2026 kwenye Uwanja wa CCM Kirumba, Mwanza.
Pia, Azam nayo itataka kukataa unyonge kwa kupoteza mechi ya tatu mfululizo mbele ya Yanga kisiwani hapa, hali inayofanya mechi hiyo kuwa tamu.
Mbali na hilo, msimamo wa ligi ulivyo unafanya mechi hii kutolewa macho na wote, si Yanga na Azam pekee, bali hata Simba ambayo yenyewe itakuwa Morogoro kukabiliana na Mtibwa Sugar.
Hiyo inatokana na kwamba, Yanga inayoongoza msimamo wa ligi ikiwa na pointi 66, inafuatiwa na Simba yenye 64, tofauti yao ni pointi mbili pekee, huku atakayeteleza kipindi hiki zikisalia mechi tatu, ubingwa asahau.
Kitu hicho Yanga haitaki kimtokee kwani hesabu zake ni kushinda mechi zote na kwenda kutetea ubingwa watakaouchukua bila ya kuangalia wapinzani matokeo yao, lakini wakiteleza kidogo, itabidi waiombee mabaya Simba nayo iteleze.
Simba inaufukuzia ubingwa wa ligi baada ya kuukosa misimu minne mfululizo ukichukuliwa na Yanga.
Azam haiko mbali sana, inashika nafasi ya tatu ikikusanya pointi 58, imeachwa nane na Yanga, katika mechi tatu zilizobaki, yenyewe inaamini lolote linaweza kutokea huenda ikabeba ubingwa, huku ikitangaza kuivurugia Yanga, kisha kutembeza vichapo mechi zitakazofuata dhidi ya Coastal Union na Dodoma Jiji, huku pia ikiziombea mabaya Yanga na Simba zifikishe pointi 67 kitu ambacho kinaweza kuwa kigumu kwani Yanga sare moja tu inafika hapo. Kumbuka inakwenda kucheza dhidi ya Azam, TRA United na JKT Tanzania.
Kuelekea mechi hiyo itakayoanza saa 10:00 jioni, Kaimu Kocha Mkuu wa Yanga, Abdihamid Moallin, alisema: "Tumejiandaa vizuri licha ya kwamba hatukuwa na muda huo wa kutosha kutoka mechi iliyopita, jambo zuri ni kwamba hakuna majeruhi mpya aliyepatikana baada ya mechi iliyopita.
"Hakuna namna ya kufanya, lazima tushinde mechi hii kwani tunataka kutetea ubingwa wetu wa ligi na ukiangalia tukishinda mechi zetu tunafikia malengo hayo."
Kwa upande wa Kocha Msaidizi wa Azam, Kassim Liogope, alisema: "Tunajua mchezo utakuwa mgumu, kikubwa msimu huu tunakwenda kukutana kwa mara ya nne, tunajua aina ya mpinzani tunayekwenda kukutana naye, Yanga ni timu nzuri, pia ina wachezaji wazoefu.
"Sisi kama Azam tumejiandaa vizuri, tumetoka kucheza nao siku chache zilizopita, muda tulioupata tumeangalia sehemu zenye upungufu na kuzifanyia kazi kuhakikisha tunafanya vizuri."
MTIBWA SUGAR VS SIMBA
Uwanja wa Jamhuri uliopo Morogoro, wenyeji Mtibwa Sugar wataikaribisha Simba ikiwa ni mechi ya kuwania ubingwa upande mwingine kuepuka kushuka daraja.
Simba inahitaji ushindi kuendelea kuifukuzia Yanga kileleni, wakati Mtibwa iliyopo nafasi ya13, inaingia uwanjani ikiwa inafahamu inahitaji kutoka kwenye eneo la mtoano wa kuepuka kushuka daraja, hivyo inahitaji kupambana ili kuwa salama zaidi.
Kuanza na Simba katika harakati hiyo, ni mtihani mzito kwa Mtibwa, huku ikienda kucheza dhidi ya Tanzania Prisons na Namungo wakiwa ni wapinzani wa moja kwa moja katika vita hii, inafanya kila dakika kwao ni ya thamani.
Mechi ya mzunguko wa kwanza baina ya Simba dhidi ya Mtibwa, matokeo yalikuwa sare ya bao 1-1.
DODOMA JIJI VS JKT TANZANIA
Mechi hii itachezwa Uwanja wa Jamhuri, Dodoma. Inakumbuka mzunguko wa kwanza, JKT Tanzania wakiwa wenyeji, walifungwa 1-0, safari hii wanaenda ugenini wakiwa hawana presha ya ubingwa wala kushuka daraja kutokana na kushika nafasi ya sita na pointi 38, hivyo kazi itakuwa kwa Dodoma Jiji ambayo bado haipo salama.
Dodoma Jiji ipo nafasi ya nane ikikusanya pointi 33, ushindi katika mechii, utaiweka salama na presha ya kushuka daraja ikibakisha mechi mbili dhidi ya Mbeya City na Azam.
TRA UNITED VS COASTAL UNION
Uwanja wa Sheikh Amri Abeid uliopo Arusha, utapigwa mchezo huu ambao TRA United inahitaji kushinda kupambania kuishusha Singida Black Stars nafasi ya nne, wakati Coastal ikisaka pointi za kujitoa kwenye hatari ya kushuka.
TRA ipo nafasi ya tano ikikusanya pointi 41, imezidiwa sita na Singida Black Stars iliyopo nafasi ya nne. Zote zimebakiwa na mechi tatu zikiifukuzia nafasi ya kucheza kimataifa msimu ujao kwa kumaliza ndani ya nne bora.
Coastal Union iliyopo nafasi ya tisa na pointi 32, hesabu zake kwa sasa inahitaji pointi nne ili kufikisha 36 za kuiweka salama isishuke huku ikianza na TRA ugenini, kisha Azam (nyumbani) na Pamba Jiji (nyumbani).
Mechi dhidi ya Pamba Jiji inaweza kuwa ya kuamua nani anakaa sehemu salama zaidi, wakati huohuo, Coastal ina bahati inamaliza mechi tatu dhidi ya timu zote ambazo zipo salama, huku mechi mbili za nyumbani zikionekana zinakwenda kuwabeba kwani ina rekodi nzuri hapo dhidi ya wapinzani wake ikishinda mechi tano, sare tano na kupoteza tatu kati ya 13 ilizocheza dimba la nyumbani.
Coastal inakumbuka mzunguko wa kwanza dhidi ya TRA matokeo yalikuwa 1-1.
FOUNTAIN GATE VS MASHUJAA
Wanakutana makocha wenye presha ya kuviweka salama vikosi vyao. Fred Felix Minziro wa Fountain Gate atamkaribisha Jamhuri Kihwelo 'Julio' wa Mashujaa kwenye Uwanja wa Black Rhino, Arusha.
Fountain Gate inahitaji kushinda mechi mbili na kupata sare moja ili kufikisha pointi 36 zitakazoiweka salama isishuke daraja. Kwa sasa inakamata nafasi ya kumi ikiwa na pointi 29, wakati Mashujaa ni ya 12 na pointi 27, tofauti yao ni pointi mbili pekee. Mzunguko wa kwanza, matokeo yalikuwa 1-1.
PAMBA JIJI VS MBEYA CITY
Vijana wa Francis Baraza, Pamba Jiji wanawakaribisha Mbeya City wanaonolewa na Salum Mayanga. Mechi itapigwa Uwanja wa CCM Kirumba, Mwanza.
Pamba Jiji ipo nafasi ya saba ikikusanya pointi 36, haina presha ya kushuka zaidi ya kusaka nafasi bora zaidi, mtihani upo kwa Mbeya City inayokamata nafasi ya 15, katika eneo la kushuka daraja moja kwa moja ikikusanya pointi 25, ipo katika hali mbaya zaidi. Inahitaji ushindi katika mechi zote tatu zilizobaki na kuziombea njaa zilizo juu yake ili kuepuka kurudi Ligi ya Champioship ilipopanda sambamba na Mtibwa Sugar.
Kumbuka ikimalizana na Pamba Jiji ugenini, itaifuata Dodoma Jiji kisha kumalizia nyumbani dhidi ya TRA United.
SINGIDA BS VS PRISONS
Wenyeji Singida Black Stars, wanatazamia kumaliza nafasi nne za juu na wanahitaji pointi tatu pekee kukamilisha lengo hilo ikibakiwa na mechi tatu.
Kwenye Uwanja wa Airtel uliopo Singida, wataikaribisha Tanzania Prisons iliyoamka kwa siku za karibuni ikipambana isishuke daraja.
Prisons inakamata nafasi ya 14 ikikusanya pointi 26, inafahamu kwamba kuteleza kidogo tu, kunatoa nafasi kwa washindani wake kumuacha na hatari ya kushuka daraja.
Ikimalizana na Singida ambapo mzunguko wa kwanza Prisons ilifungwa 2-1 nyumbani, mechi zitakazofuata ni dhidi ya Mtibwa Sugar (nyumbani) na Mashujaa (ugenini).
Mechi mbili za mwisho dhidi ya Mtibwa na Mashujaa ni 'fainali' halisi za nani anabaki na nani anakumbwa na janga la kushuka daraja.
KMC VS NAMUNGO
Tayari KMC imeshuka, hivi sasa inakamilisha ratiba kwani hata ikishinda mechi zote tatu, haiwezi kusogea nafasi yoyote zaidi ya kubaki ya mwisho.
Inakutana na Namungo kwenye Uwanja wa KMC Complex jijini Dar, wakati ambao Wauaji hao wa Kusini wakiwa na presha ya kubaki eneo salama.
Kwa sasa Namungo inakamata nafasi ya 11 na pointi 27, mechi zilizobaki ni dhidi ya KMC (ugenini), Fountain Gate (nyumbani) na Mtibwa Sugar (nyumbani).
Ratiba yao inaonekana kuwa na unafuu kidogo kwani mechi mbili za mwisho itamalizia nyumbani baada ya kutoka ugenini kuikabili KMC, lakini mechi dhidi ya Mtibwa Sugar itakuwa ya kufa au kupona.
Hata hivyo, pia inahitaji kuweka hesabu sawa kuanza kuichapa KMC ambayo mzunguko wa kwanza, Namungo ilishinda 1-0.