TUONGEE KISHKAJI: Asichokijua Shabani Kaoneka kuhusu Mandonga Mtu Kazi

HISIA ZANGU: Mandonga amepigwa lakini anabakia kuwa mshindi

SHAABAN Kaoneka, bondia aliyempiga Karim Mandoga hivi majuzi alikuwa analalamika kwamba waandishi wa habari ni wanafiki sana, yeye ndiye aliyeshinda pambano, lakini ajabu ni kwamba waandishi wanamfuata Mandonga na kumhoji kwa kumpa ‘air time’ badala ya kumhoji mshindi.

Kwa kunukuu maneno yake Kaoneka anasema: “Nyinyi waandishi wanafiki sana. Mimi ndiye niliyeshinda pambano, lakini badala yake mnamfuata Mandonga na kumfanyia sapraizi badala ya kunifuata mimi. Yaani mnampa madili Mandonga, mimi mshindi nabaki na umaskini. Mimi nitajisikiaje?” Lakini asichokijua Kaoneka ni kwamba alitakiwa kumshukuru Mandonga tu, kwani licha ya kumpiga Mandonga na kupata ushindi ukweli ni kwamba Mandonga amefanya kazi kubwa sana ya kulitangaza lile pambano. Bila mbwembwe za Mandonga, bila mdomo wa Mandonga lile pambano lingekuwa kama mengine ya kawaida ya utangulizi tu. Pambano lingeisha bila maajabu yoyote lingeisha bila kuongelewa na yeyote zaidi ya mashabiki kindakindaki wa mchezo wa ngumi.

Lakini lile pambano lilifuatiliwa kuliko hata pambano kuu. Lile pambano liliangaliwa hadi na watu wasiofahamu chochote kuhusu ngumi, lakini yote ni kwa sababu ya nani? Mandonga.

Mandonga anapata ushindi wa kushobokewa na waandishi leo kwa sababu alijiandaa hivyo. Pengine Mandonga hakujiandaa sana kwenye ngumi na ndio maana akapigwa, lakini alijiandaa sana kwenye kulitangaza pambano. Kwa lugha rahisi ni kila mtu kamaliza akiwa na alichotakiwa kuwa nacho. Kaoneka kamaliza na ushindi wa mechi, Mandonga kamaliza na umaarufu.

Kabla ya pambano mtandaoni kulikuwa na video za Mandonga kibao akiwa zake Coco Beach akifanya mazoezi ya kubeba magogo kama mtengeneza tanuri la mkaa. Mara kwenye video zingine anaonekana anapiga ngumi mti hadi magome yanabanduka. Yaani kuna muda ulikuwa ukiangalia zile ‘clip’ za mazoezi ya Mandonga ulikuwa unaona kabisa huyu bwana lazima apigwe.

Lakini wakati unaona lazima apigwe, mara unakutana na video nyingine inayomuonyesha akipewa zawadi ya gari na shabiki wake. Halafu kwa tambo anasema: “Dah! Ebwaaana yaani mtu nimepewa Jeep (gari) halafu unipige? Hiyo itakuwa dharau.” Yaani ilikuwa ni vituko.

Na vituko vyake havikuwa na mwisho hujamaliza video yake ya kupewa Jeep unakutana na video nyingine akimchimba mkwara Kaoneka. Anamwambia: “Shabani Kaoneka safari hii utakoma, aliyekushauri mdogo wangu upigane na mimi kakuponza. Njoo na jeneza maana utarudi nyumbani ukiwa sio wewe.”

Sasa niambie kama umewahi kuona video ya Kaoneka akifanya vitu kama hivyo kabla ya pambano. Hakuna. Haipo. Nina uhakika wakati Kaoneka anatazama video za Mandonga akawa anajisemea mwenyewe: “We’ ongea ongea tu kwenye mitandao mimi niko nafanya tizi kali halafu tutakutana ulingoni.”

Na kweli, baa ya pambano Kaoneka kapata malipo ya mazoezi yake. Kamaliza mchezo kwa ushindi. Na Mandonga naye mbwembwe zake zimemlipa kamaliza mchezo kwa kupigwa, lakini akiwa staa vyombo vya habari vikimgombania na madili ya pesa kama yote - si haba.

Hivyo Kaoneka ajifunze kuheshimu ushindi wa Mandonga kwani haujaja bure, kuna kazi imefanyika.