Tchakei, Damaro hawana kazi rahisi Yanga
Muktasari:
- Huu ni usajili wa kimkakati na mzuri kwa Yanga kwani wachezaji hao wote ni wazoefu wa mazingira na soka la Tanzania hivyo hapa kijiweni hatudhani kama wanahitaji muda mrefu kumudu maisha ndani ya klabu yao mpya.
HATIMAYE Mohamed Damaro na Marouf Tchakei wamejiunga na Yanga wakitokea Singida Black Stars baada ya timu hizo kufikia makubaliano.
Huu ni usajili wa kimkakati na mzuri kwa Yanga kwani wachezaji hao wote ni wazoefu wa mazingira na soka la Tanzania hivyo hapa kijiweni hatudhani kama wanahitaji muda mrefu kumudu maisha ndani ya klabu yao mpya.
Kwa Damaro ndio wamelamba dume zaidi kwa vile mchezaji huyo atacheza akiwa na leseni ya mchezaji wa ndani kwa sababu hapo nyuma alibadilisha uraia na sasa ni Mtanzania hivyo Yanga hailazimiki kumpunguza mchezaji mmoja wa kigeni ili aingie yeye.
Hata hivyo, hao wachezaji wawili wanatakiwa wafanye kazi ya ziada ili waweze kujitengenezea ufalme wao ndani ya Yanga vinginevyo watajikuta wakipata muda mdogo wa kucheza au kusotea benchini.
Katika nafasi anayocheza yule Damaro kuna Mkenya Duke Abuya ambaye amekuwa na muendelezo mzuri wa kiwango bora katika nafasi ya kiungo wa ulinzi huku pia akiwa mzuri wa kuchezesha timu.
Wakati ukimfikiria Abuya, kuna mkali mwingine ambaye anaweza vyema kucheza hapo na akatoa zaidi ya kujilinda ambaye ni Mudathir Yahya.
Tchakei yeye nafasi yake anapaswa kuonyesha kiwango kizuri zaidi kwani aina ya watu anaowania namba ndio kina Pacome Zouzoua au Maxi Mpia Nzengeli ambao kadri siku zinavyozidi kwenda mbele, wanazidi kuonyesha ubora wa hali ya juu.
Wakati huo tukumbuke Tchakei na Damaro wamejiunga na Yanga katika dirisha dogo la usajili na wameikuta timu tayari ina wachezaji ambao walishaingia kwenye mfumo hivyo haiwezi kuwa rahisi kuwachomoa kikosini.
Kazi iliyo mbele yao sio nyepesi na kwa bahati mbaya kwao wamejiunga na timu inayohitaji matokeo mazuri muda wote na haitoi muda mrefu wa kumsubiria mchezaji.