Straika mtata wa Mbao huyu hapa

VITA ya Kiatu cha Dhahabu kwa msimu huu wa Ligi Kuu Bara inaendelea kuwatoa udenda nyota wa timu mbalimbali kwa kila mmoja kuhitaji tuzo hiyo.
Tulishuhudia msimu uliopita ushindani ulivyojitokeza na kusababisha tuzo hiyo kuchukuliwa na wachezaji wawili, Saimon Msuva aliyekuwa Yanga na Abdulrahaman Mussa wa Ruvu Shooting kwa kuwa na mabao 14 kila mmoja.
Hata msimu huu dalili zinaonyesha vita hiyo itaendelea kuwa kubwa kwani, hadi sasa wachezaji sita kutoka vilabu tofauti wanaweza kuibuka na tuzo hiyo ya Mfungaji Bora.
Wachezaji hao ni pamoja na nyota wa Simba raia wa Uganda, Emmanuel Okwi ambaye anaongoza kwa mabao manane na kufuatiwa na Mohamed Rashid (Prison) na Obrey Chirwa wa Yanga wenye mabao sita kila mmoja.
Wengine ni Ibrahim Ajib (Yanga), Shiza Kichuya (Simba) na Habib Kiyombo wa Mbao FC ambao, kila mmoja ametupia kambani mabao matano katika mechi 11.
Kutokana na kasi hiyo na vita ya kimya kimya ya kugombea tuzo ya mfungaji bora, makala hii imeteta na nyota wa Mbao, Habib Kiyombo ambaye anafunguka mipango na mikakati ya kuhakikisha hakosi kiatu hicho na malengo yake kwenye soka la kisasa.
UFUNGAJI BORA
Straika huyo anasema kuwa malengo yake msimu huu ni kuwania tuzo ya mfungaji bora kwa kuhakikisha anawazidi wapinzani wake tena mapema tu.
Anasema kuwa amepanga kujituma zaidi na kutochezea nafasi ya kufunga mara aipatapo ili kuendana na kasi ya vita ya ufungaji bora, ambayo inaonekana kuvaliwa njuga na nyota wa timu pinzani.
“Kwanza ni kujituma, kufuata kile kocha anachoelekeza na zaidi kutumia nafasi ninayopata kwenye umaliziaji. Niseme tu lengo langu nataka kiatu cha mfungaji bora msimu huu,” anasema Kiyombo anayeitumikia Mbao kwa msimu wa pili.
USHINDANI UKOJE
Kinda huyo, ambaye ni msimu wa pili kucheza Ligi Kuu, anakiri kuwa ushindani uliopo kwenye kuwania kiatu cha mfungaji bora ni mkubwa lakini atakomaa mpaka kieleweke.
Anasema kuwa licha ya kutanguliwa na nyota wa Simba, Okwi na Chirwa wa Yanga, anaamini uwezekano wa kufunga mabao kwenye mechi moja na kuwafikia au kuwazidi upo.
“Kwa mfano kama Okwi alibahatika kufunga mabao mengi kwenye mechi moja, ni jambo ambalo linawezekana hata kwangu, niseme nitapambana kadri ya uwezo wangu,” alisema Kiyombo.
ANA DENI MBAO
Kinda huyo anasema kuwa licha ya kutazama mafanikio yake mwenyewe, bado ana deni kubwa kwa timu yake kuhakikisha inamaliza ligi ikiwa nafasi nzuri.
Anasema kuwa hadi sasa Mbao haijapata matokeo mazuri na nafasi waliyopo haimpi raha na badala yake inahitajika nguvu na bidii kubwa kuisaidia kuwa kwenye nafasi nzuri.
“Mafanikio ya Mbao ndio fahari yetu wachezaji, wakati napambana kuhakikisha nafunga, vivyo hivyo naifikiria timu yangu kuwa sehemu nzuri,” anasema Straika huyo.
SIMBA NA YANGA
Kinda huyo anayekuja kwa kasi anasema kuwa, anapenda kucheza moja ya timu hizo za Dar es Salaam, lakini kwa masharti ikiwamo kupata namba kikosi cha kwanza, kuheshimiwa na kuthaminiwa na kupewa stahiki zote za msingi.
Anasema kuwa anasikia tetesi za kutakiwa na moja ya timu hizo haswa Yanga, na hana kizuizi kwani hata mkataba wake haumbani kutokana na makubaliano yake yaliyopo na Mbao.
“Mkataba wangu haunibani uko wazi sana kwamba pakitokea timu inayonihitaji, basi tunakaa meza moja kuzungumza na klabu itaniruhusu,” anasema..
Anaeleza kuwa kazi yake ni soka, hivyo kuhama siyo tatizo kwani ni moja ya changamoto katika kazi yake hiyo ya kusakata kandanda.
“Tunapenda kucheza Simba na Yanga, lakini tatizo ni benchi, hii inarudisha nyuma viwango na uwezo kwa mchezaji, ila nikihitajika kwa mojawapo ya timu hizo nipo tayari,” anasema Kiyombo.
Anaongeza kuwa mara kadhaa vilabu hivyo huwatumia zaidi wachezaji wa kigeni na kwamba, hiyo huchangia kwa kiasi kikubwa hata soka la nchi kushuka kiwango.
Anashauri kuwa wachezaji wa kigeni wawepo kwenye timu, lakini wachanganywe ili hata wazawa wapate uzoefu kucheza na wageni badala ya kuwa watazamaji tu.
“Bora wachanganywe kwa pamoja, wakiingia wawe watatu uwanjani halafu nane wawe wazawa, hii itasaidia kupata wachezaji wazuri kitaifa,” anasema.
KWENDA NJE
Mshambuliaji huyo anasema kuwa, dua zake za kila siku ni kuona anacheza soka la kulipwa nje ya Tanzania kama walivyo Simon Msuva na Mbwana Samatta.
Anasema kuwa anaamini siku akipata dili la kukipiga nje bila kujali aina gani ya timu, atashukuru maradufu kwani soka la nje linawajenga zaidi vijana katika soka.
“Yaani dua zangu za kila siku ni kuomba kucheza moja ya timu za nje ya hapa Tanzania, naamini nikipata nafasi huko nje nitafanya zaidi ya hapa, kule ni kutamu sana,” anaeleza
“Angalia Msuva na Samatta wanapokuja kwenye timu ya Taifa, utawapenda tu, lakini hata wengine kama Ulimwengu (Thomas) nao wako vizuri, na hii inadhihirisha jinsi gani huko nje palivyo bomba kumjenga mtu.