Prime
Simba, Yanga kumenyana kwa saa, siku
KUNA wakati kwenye soka ubora wa kikosi hautoshi. Kuna wakati ratiba, safari, muda wa kupumzika na uwezo wa wachezaji kuhimili uchovu huwa na mchango mkubwa kuliko hata mbinu za makocha.
Ndiyo hali ilivyo sasa Ligi Kuu Bara ikiwa imebakiza raundi tano pekee kabla ya msimu wa 2025/26 kufungwa rasmi mwishoni mwa Juni.
Ndani ya siku 15 zijazo, timu zote 16 za Ligi Kuu Bara zitaonyeshana ubabe katika Uwanja wa Lake Tanganyika (Kigoma), Sheikh Amri Abeid (Arusha), CCM Kirumba (Mwanza), Majaliwa (Lindi), Mkwakwani (Tanga), Airtel (Singida), Tanzanite Kwaraa (Manyara), Azam Complex na KMC Complex vya Dar es Salaam huku kila upande ukipigania jambo lake.
Yanga itaingia katika raundi hizi za lala salama ikiwa kileleni mwa msimamo wa ligi hiyo ikiwa na pointi 60, Simba ikiwa pointi mbili nyuma yake na Azam FC ikiwa na pointi 52. Chini ya msimamo, KMC yenye pointi tisa, Tanzania Prisons (20), Mbeya City (22), Namungo (25), Mtibwa Sugar (27) na Mashujaa (27) zinaendelea kupigania kusalia.
Tofauti ya mafanikio na kushindwa inaweza isiwe tu ndani ya dakika 90 za mchezo, bali kwenye safari zitakazofanywa kabla ya filimbi ya kwanza kupulizwa.
RAUNDI ZA MWISHO
Miongoni mwa timu zinazowania ubingwa, Yanga ndiyo inayokabiliwa na ratiba yenye safari ndefu zaidi katika raundi tano za mwisho. Mabingwa hao wataanza kwa safari ya kwenda Kigoma kucheza dhidi ya Mashujaa FC katika Uwanja wa Lake Tanganyika Juni 13 kabla ya kuelekea Arusha kwa mchezo dhidi ya Fountain Gate Juni 18 katika Uwanja wa Sheikh Amri Abeid.
Kutoka Arusha watarejea Dar es Salaam kwa pambano kubwa dhidi ya Azam FC Juni 24 wakati huo watakuwa wamecheza mechi ya nusu fainali ya Kombe la CRDB dhidi ya timu hiyo, kisha kucheza mechi mbili za mwisho dhidi ya TRA United na JKT Tanzania jijini Dar es Salaam.
Iwapo safari hizo zingefanywa kwa barabara pekee, Yanga ingelazimika kusafiri takribani kilomita 4,100 hadi 4,300. Safari ya Dar es Salaam kwenda Kigoma ni zaidi ya kilomita 1,200, Kigoma kwenda Arusha ni zaidi ya kilomita 1,500 na Arusha kurejea Dar es Salaam ni takribani kilomita 650.
Hata hivyo, kwa mazingira ya kawaida ya Ligi Kuu Bara na kutokana na muda mfupi uliopo kati ya mechi hizo, kuna uwezekano mkubwa Yanga kutumia usafiri wa anga katika safari za Dar es Salaam-Kigoma na Kigoma-Arusha.
Katika hali hiyo, umbali wa safari unabaki uleule wa kijiografia, lakini muda wa usafiri hupungua kwa kiasi kikubwa na kupunguza uchovu wa wachezaji.
Hata hivyo, hata kwa kutumia ndege, Yanga bado ndiyo timu yenye ratiba ngumu zaidi miongoni mwa wanaowania ubingwa kwa sababu italazimika kucheza katika kanda tatu tofauti za nchi Magharibi (Kigoma), Kaskazini (Arusha) na Mashariki (Dar es Salaam) ndani ya siku 17.
Simba ambayo imebaki pointi mbili nyuma ya Yanga, inaonekana kuwa na ahueni. Wekundu hao wataanza Juni 14 kwa kuikaribisha Pamba Jiji katika Uwanja wa KMC Complex kabla ya kusafiri kwenda Mbeya kucheza na Mbeya City kwenye Uwanja wa Sokoine Juni 17.
Baada ya hapo watakuwa wageni wa Mtibwa Sugar Juni 24 kabla ya kurejea Dar es Salaam kuikabili Singida Black Stars Juni 27 katika Uwanja wa KMC Complex. Mchezo wao wa mwisho utakuwa dhidi ya KMC Juni 30.
Tofauti na Yanga, Simba haitalazimika kwenda Kigoma wala Arusha katika kipindi hiki, jambo linalopunguza mzigo wa safari na kuipa nafasi kubwa ya kuingia kwenye kila mchezo ikiwa na nguvu zaidi.
Kwa ujumla, Simba inaweza kutumia takribani kilomita 1,500 hadi 1,800 kwa usafiri wa barabara katika raundi hizi tano za mwisho huku umbali huo ukishuka hadi kati ya kilomita 800 na 1,000 iwapo safari zake kubwa zitafanyika kwa ndege.
Azam FC nayo ina ratiba ambayo inaweza kuamua hatma ya msimu wake. Itaanza kwa safari ya Arusha kucheza na Fountain Gate katika Uwanja wa Sheikh Amri Abeid Juni 12 kabla ya kuikaribisha Mashujaa FC kwenye Azam Complex Juni 16.
Baada ya siku nane, Azam itashuka dimbani dhidi ya Yanga katika mechi ambayo inaweza kubadili mbio za ubingwa kabla ya kwenda Tanga kucheza na Coastal Union kwenye Uwanja wa Mkwakwani na kumalizia dhidi ya Dodoma Jiji kwenye Azam Complex Juni 30. Azam itasafiri takribani kilomita 2,000 hadi 2,200 katika raundi hizi tano za mwisho.
SINGIDA, JKT NA TRA
Katika vita ya nafasi za CAF, Singida Black Stars inaonekana kuwa na ratiba yenye mitego mingi. Itaanza Dar es Salaam dhidi ya JKT Tanzania katika Uwanja wa Meja Jenerali Isamuhyo Juni 13 kabla ya kurudi nyumbani kucheza na Dodoma Jiji na Tanzania Prisons kwenye Uwanja wa Airtel.
Juni 27 itakuwa mgeni wa Simba katika Uwanja wa KMC Complex kabla ya kufunga msimu Arusha dhidi ya Fountain Gate katika Uwanja wa Sheikh Amri Abeid.
Kwa safari hizi, Singida Black Stars itasafiri takribani kilomita 1,600 hadi 1,900 kwa jumla.
JKT Tanzania nayo itaanza kwa Singida Black Stars na Tanzania Prisons katika Uwanja wa Meja Jenerali Isamuhyo kabla ya safari za Dodoma na Mwanza kucheza dhidi ya Dodoma Jiji na Pamba Jiji. Mechi yake ya mwisho dhidi ya Yanga inaweza kuwa na uzito mkubwa katika kuamua nafasi za CAF.
Kwa upande wake, JKT Tanzania itakuwa na safari ya takribani kilomita 2,200 hadi 2,600. Hii inatokana na mzunguko wa Dar es Salaam kwenda Dodoma (km 800 kwenda na kurudi), Dar es Salaam kwenda Mwanza (km 1,800 kwenda na kurudi), pamoja na safari za ndani kuelekea KMC na Isamuhyo.
TRA United ndiyo timu inayoweza kusafiri umbali mrefu zaidi katika raundi hizi za mwisho. Itaanzia Dar es Salaam dhidi ya KMC katika Uwanja wa KMC Complex, kisha kwenda Lindi kucheza na Namungo kwenye Uwanja wa Majaliwa.
Kutoka Lindi watasafiri hadi Tanga kucheza na Coastal Union katika Uwanja wa Mkwakwani kabla ya kurejea Dar es Salaam kuifuata Yanga kwenye Uwanja wa KMC Complex na kumalizia Mbeya dhidi ya Mbeya City katika Uwanja wa Sokoine.
Kwa TRA United, mzigo wa safari ni mkubwa zaidi takribani kilomita 3,200 hadi 3,600 ambazo watazikata kwa barabara.
VITA YA KUEPUKA SHUSHA DARAJA
Katika vita ya kujiokoa kushuka daraja, Namungo itaanza safari yake Tanga dhidi ya Coastal Union kwenye Uwanja wa Mkwakwani kabla ya kuikaribisha TRA United, Fountain Gate na Mtibwa Sugar katika Uwanja wa Majaliwa huku ikisafiri Dar es Salaam kucheza na KMC. Kwa Namungo, jumla ya safari inakadiriwa kuwa takribani kilomita 1,800 hadi 2,200.
Mtibwa Sugar itaanza Mbeya dhidi ya Mbeya City katika Uwanja wa Sokoine kabla ya kwenda Mwanza kucheza na Pamba Jiji kwenye Uwanja wa CCM Kirumba. Kisha itakutana na Simba, Tanzania Prisons katika Uwanja wa Airtel na kumalizia safari yake Lindi dhidi ya Namungo. Kwa Mtibwa Sugar, safari kwa takribani kilomita 2,400 hadi 2,800.
Mbeya City nayo haina nafasi ya kufanya makosa. Baada ya kuanza nyumbani dhidi ya Mtibwa Sugar na Simba katika Uwanja wa Sokoine, itaenda Mwanza kucheza na Pamba Jiji katika Uwanja wa CCM Kirumba, kisha Dodoma kabla ya kurejea Mbeya kuhitimisha msimu dhidi ya TRA United. Kwa Mbeya City, jumla ya safari zake ni kilomita 2,000 hadi 2,400.
KMC iliyopo mkiani ikiwa na pointi tisa itaikaribisha TRA United, Coastal Union na Namungo katika Uwanja wa KMC Complex kabla ya kusafiri hadi Kigoma kucheza na Mashujaa kwenye Uwanja wa Lake Tanganyika na kumalizia dhidi ya Simba. Kwa KMC, mzigo wa safari ni mkubwa ukizingatia itatoka Dar es Salaam kuelekea Kigoma kisha kurudi tena kwa ratiba ya mwisho wa msimu.
Jumla ya safari zake inakadiriwa kuwa takribani kilomita 1,900 hadi 2,450. Hata hivyo ratiba hizo zinaweza kubadilika katika mechi za mwisho za msimu ambapo zitatakiwa kupigwa zote kwa wakati mmoja.