RIPOTI MAALUMU: Kifo cha Sonso ni mapenzi ya Mungu lakini...-2

KUNA misiba lakini kuna msiba wa aliyekuwa mchezaji wa Timu ya Taifa ya Tanzania (Taifa Stars), Ali Mtoni ‘Sonso’. Namaanisha nini? Namaanisha ipo misiba ambayo ikitokea unasema kazi ya Mungu haina makosa lakini sisi kama wanadamu, ni lazima wakati mwingine tuulizane maswali magumu kidogo.
Jana kwenye sehemu ya kwanza ya ripoti hii ya kifo chake niligusia mambo mengi ikiwemo tatizo linalojulikana kitaalamu kwa jina la Deep Vein Thrombosis (DVT). Hilo ni tatizo la kiafya linalosababishwa na kuganda kwa damu kwenye mishipa ya damu. Ni kama vile damu inakuwa kwenye mabonge na wakati mwingine linakuwa bonge la mafuta ambalo wataalam walinidokeza kwamba ndilo haswa lililochukua uhai wa mpendwa wetu.
Lakini nikauliza maswali mengi tata ambayo hayana majibu kuhusiana na mazingira ya kifo cha Sonso. Lakini kwa sababu sisi sio mbuzi wala ng’ombe na Mwenyezi Mungu ametuumba pia kuwa viumbe vya kuwaza na kutafakari, ningependa kuuliza maswali mengine kadhaa kupitia makala hii;
Swali langu hapa ni je, nani alimpa Sonso mbadala wa namna hii? Kulikuwa na mtu aliyewahi kumwambia haya na Sonso akakataa? Taarifa nilizonazo ni kwamba Muhimbili hawakutaka kumwachia na aliondoka kwa kitu kinachoitwa DAMA yaani Discharged Against Medical Advise (kuondolewa hospitalini kinyume na matakwa ya madaktari).
Wakati Muhimbili wanamwachia Sonso kwa DAMA, yeye na familia yake walielezwa kinagaubaga kuhusu mbadala au waliambiwa tu “mkitaka kuondoka bila kibali chetu jazeni fomu hii?”.
Nauliza maswali haya si kwa sababu ya kutafuta mchawi katika suala hili la kifo cha Sonso. Lakini naamini kwamba mwanadamu hawezi kupoteza uhai – tena mwanadamu ambaye anatakiwa kuchukuliwa kama shujaa wa taifa, halafu nchi ikakaa kimya kana kwamba aliyekufa ni ng’ombe wa mnadani.
Ni nani aliwahi kumfuata Sonso na kumnong’oneza sikioni kwamba huko alikoenda kutafuta tiba kutahitimisha maisha yake? Je, mfumo wetu wa kulea wachezaji unatoa fursa ya kuwa na watu wa aina ya wataalamu wa saikolojia wenye uwezo wa kuzungumza na wachezaji kama watu wanaohitaji kuelekezwa na kufundishwa yale wasoyajua?
Sonso hatakiwi kulaumiwa kwa uamuzi wowote aliouchukua kuhusu afya yake. Ninachojua mimi ni kwamba mtu akiumwa na kuwa katika maumivu makali, wakati mwingine akili yake inakuwa haiko sawa. Lilikuwa ni jukumu letu kama wanajamii ya soka kumsaidia na kumrudisha kwenye mstari. Kama Sonso angesema dawa ya kupona kwake ni kujitumbukiza kwenye moto, hakuna ambaye angemkubalia.
Lakini alikubaliwa alilolisema kwa sababu inawezekana walio karibu yake – waajiri na familia, waliamini maneno yake. Hawakujua hali yake kichwani kwake ilikuwaje. Hawakumsaidia sana kuamini katika upande ambao akili yake haikuwa na imani nao.
Ninajiuliza pia madaktari au wataalamu wa sayansi ya michezo wanaotumika katika klabu za mpira wa miguu Tanzania. Je, huwa wana utaratibu wa kubadilishana taarifa kuhusu kinachoendelea ndani ya klabu zao. Kwa mfano, kama daktari wa JKT Ruvu kaona tatizo kwa Sonso ambalo hajawahi kuliona kwenye maisha yake ya utabibu, huwa anauliza kwa wenzake kujua tatizo linaweza kuwa nini?
Madaktari wanatofautiana kwa utaalamu, uzoefu, uzoefu na mafunzo. Ndiyo sababu, katika nchi zilizoendelea, madaktari wa michezo huwa wanakutana mara kwa mara kujadiliana kuhusu kinachoendelea katika tasnia yao. Wanafahamu kwamba kuna magonjwa na changamoto mpya za kiafya zinaibuka kila mara kutokana na mabadiliko kwenye aina ya vyakula wanavyokula wachezaji, kukua kwa sayansi na teknolojia na mengineyo.
Sijawahi kusikia Tanzania kuna mkutano wa madaktari wa michezo na mkutano wao wa mwaka wanazungumza na kujadiliana nini. Ninasoma sana habari za michezo kwa kipindi cha miaka 15 sasa lakini sikumbuki siku ambayo nilisikia wataalamu wetu wa afya wakituambia nini kinaendelea katika sayansi ya michezo kwenye nyakati hizi.
Tanzania imewahi kupoteza wachezaji kwa maradhi ya moyo uwanjani wakiwa tangu enzi zakina Hussein Tindwa miaka 40 iliyopita - kabla hata hatujaanza kusikia hadithi za akina Marc Vivien Foe wala kunusurika kwa kina Fabrice Muamba na Christian Eriksen. Na sasa Ulaya wataalamu wa huko wameanza kujadiliana kama chanjo ya Covid 19 imechangia kuongeza matukio ya magonjwa ya moyo michezoni au la. Ndiyo kazi ya wataalamu wa afya.
Kama wataalamu wetu wanafanya kazi kwa kushirikiana, wataalamu wa Ruvu Shooting waliwahi kuwasiliana na wenzao wa timu nyingine kuomba ushauri wa kitaalamu kuhusu suala la Sonso? Hii ni kwa sababu, kama ugonjwa wa marehemu unatibika hospitali, kulikuwa na fursa ya kutuma timu ya madaktari kwa familia, ndugu na jamaa wa Sonso kuwahakikishia kwamba ugonjwa wake unaweza kabisa kupona hospitali.
Tunatokaje hapa tulipo?
Nini kiliokoa maisha ya Eriksen wa Denmark kwenye mashindano ya Euro yaliyopita? Ni kifaa kinaitwa Defribillator. Ni kifaa kinachoweza kuzimua mapigo ya moyo na kurejesha uhai wa mhusika kutoka katika hali ya umauti. Nimeuliza madaktari wengi wa Tanzania na wameniambia kuna timu mbili hapa nchini ambazo zinajulikana kuwa na kifaa hicho – Simba na Azam. Inawezekana kuna timu zaidi zinamiliki kifaa hicho lakini nimeambiwa kwa uhakika kuhusu timu hizo mbili.
Hiki ni kifaa ambacho bei yake haizidi dola 1,500 (zaidi kidogo ya shilingi milioni tatu) lakini kina uwezo wa kuokoa maisha ya mchezaji, waamuzi na hata shabiki uwanjani, endapo kitakuwepo katika wakati na mahali sahihi. Lakini timu nyingi zimeamua kwamba kifaa hicho si muhimu. Hakipo.
Kuna timu ngapi, angalau kwa ngazi ya Ligi Kuu, zilizoajiri madaktari halisi kwa ajili ya kuhudumia timu zao? Madaktari wanaweza kuonekana kuwa kazi yao ni kuwakanda wachezaji kwa barafu na kuwapa Panadol tu wakizidiwa lakini nje ya macho yetu mchango wao ni mkubwa sana.
Mara zote mimi husikitika nikiona timu imemfukuza kazi daktari wake. Na bahati mbaya sisi waandishi huwa hata hatufuatilii kujua timu gani imeajiri daktari yupi. Napenda sana kutumia mfano wa Bayern Munich linapokuja suala la umuhimu wa madaktari. Daktari wao, Hans Mueller Wohlfart alidumu kwa takribani miaka 40. Akikua katika kazi yake, akijifunza na kuibua vitu vipya. Kawatibu kuanzia kina Franz Beckenbauer mpaka Arjen Robben.
Tanzania utakuta daktari mzuri na aliyezoea mpira kwa takribani miaka 10 anaachwa kurudi mitaani na kuingizwa wapya. Ni muhimu sana kuwaheshimu madaktari walioacha shughuli zao wodini na kuhamia kwenye viwanja vya mpira. Kadri daktari anavyodumu na kupata maarifa mapya, ndivyo anavyokuwa mzuri zaidi.
Uzoefu hujenga uzeefu (skills). La kwanza ni kupata madaktari wengi kadri inavyowezekana. Kama wako wachache, ni lazima wawekewe mazingira ya kuwafanya watake kuingia michezoni na wakiingia wabaki. Bila madaktari wataalamu, wanaofahamiana na kushirikiana, nchi yetu itaendelea kupoteza vijana wengi na tutasema ni “mapenzi ya Mungu”.
Ni muhimu sana kutengeneza mfumo wa soka unaolinda afya na hatma ya vijana wetu wadogo wanaotafuta maisha kupitia michezo. Wachezaji si maroboti kusema kazi yao ni kucheza tu na wakiugua au kuumia sisi kazi yetu ni kutafuta watu wa kuziba nafasi zao.
Jukumu la kumhudumia mchezaji ni la klabu yake. Kama kaumia kwenye timu ya taifa, ni jukumu la klabu na TFF kuhakikisha anapona na kurejea mchezoni. Kama kwa bahati mbaya hakupona, ni jukumu la familia ya soka kuwatafutia maisha mengine ndani ya tasnia ya mpira. Kazi zipo nyingi kuanzia za utunzaji vifaa, ukocha, umeneja, usomaji mchezo na mambo mengine.
Nitashukuru sana kama tutatumia neno kazi ya Mungu haina makosa pale tutakapojitazama kama familia ya mpira na kusema tulifanya kila lililowezekana lakini hatukufanikiwa. Kwa bahati mbaya, kwa maoni yangu, Sonso hakufanyiwa kila alichostahili wakati akiwa hai.
Kifo cha kijana huyu na kitufundishe kitu. Tuseme neno moja tu; Never Again.