RIPOTI MAALUM -2 : Changamoto ya lishe kwa wanamichezo wa kike nchini

Mwandishi wa makala haya akiwa na mwanariadha Failuna Matanga
KATIKA sehemu iliyopita tuliona jinsi lishe ya wanamichezo wanaume na wanaume isivyokuwa na tofauti, lakini maumbile yanaleta utofauti mdogo katika uhitaji wa lishe yenyewe. Endelea na makala haya ili ujue umuhimu wa lishe kwa wanawake wanamichezo na vyakula wanavyopaswa kula. Sasa endelea...
Wanamichezo wa kike wanakula nini?
Katika utafiti, nimepita kwenye timu mbalimbali za michezo ya wanawake pamoja na wanamichezo binafsi wa kike na kufahamu kile kinachoendelea huko kuhusu lishe.
Katibu wa timu ya soka ya wanawake ya Mkwawa Queens ya Iringa, Enock Mchala anasema: “Lazima tukiri kweli, hapa Mkwawa sisi tunakula chakula kulingana na bajeti tuliyokuwa nayo au tuliyokuwa tumepanga. Tungekuwa na uwezo tungezingatia sana lishe, katika kutambua vyakula gani vyenye madini yanayohitajika ili kuwapatia wachezaji wetu.”
Naye Mwenyekiti wa Mkwawa Queens, Joel Musiba anasema: “Kwa mfano niongezee, kitaalamu inawezekana kweli hatufanyi, ama kwa kujua au kutokujua. Tukizungumzia aina ya vyakula vinavyohitajika kwenye kambi kwa watoto wa kike, mara nyingi inakuwa sawa tu na watoto wa kiume. Lakini, hapa kulingana na bajeti hatuwezi kuwa na mpangilio wa vyakula kama ilivyo kwenye timu kubwa. Sisi tunajua kambini, chakula kinachoweza kuliwa kwa urahisi na mchezaji ni lazima liwepo dagaa, ambapo ndani yake kuna madini chuma. Sisi tuna maharage kwenye protini, kuna mboga za majani hizo hazikauki, zinakuwapo karibu katika kila mlo wa wachezaji wetu. Matunda kwa ajili ya vitamini C na D, huwa tunawapa kwa wingi.
“Tunajifunza, kumbe wenzetu wakiwa kwenye ile ibada yao kuna vyakula wanavyohitaji kipindi hicho, tunajua tuwalishe vyakula ambavyo vitawafanya warudishe madini yao waliyopoteza ili kuwafanya kuwa kwenye viwango bora.”
Mwanzilishi wa timu ya soka ya Amani Queens ya Lindi, Ally Mpeni anasema: “Chakula ni gharama sana. Kingine wale wenzetu wana ibada yao ya kila mwezi, achana na gharama za zile taulo, kwenye chakula ni muhimu. Hivi vitu ni changamoto kubwa sana, kwa sababu chakula ni muhimu na uchumi wetu ni wa kujikongoja. Hili ni eneo tunalohitaji sapoti ya wadau mbalimbali kwani Amani Queens inaitangaza Lindi.”
Kwa upande wa kocha wa timu hiyo, Omary Chinola anaongeza: “Changamoto kubwa ipo kwenye uchumi. Eneo la uchumi linagusa mazingira mengi sana. Kwenye timu zetu hizi, kwenye ishu ya uchumi, kuna vyakula. Kwa sababu ni lazima tuwatafutie vyakula vya kurudisha ile nguvu iliyopotea. Lakini, sasa kutokana na uchumi wetu, wanalazimika kula vyakula vilevile siku zote, hilo nalo ni tatizo.”
Kocha wa timu ya soka ya wanawake Alliance Queens ya Mwanza, Ezekiel Chobanka, anasema: “Mimi ndiye kocha niliyewatengeneza wachezaji kama Enekia Kasonga, Aisha Masaka, Aisha Juma, Ester Mabanza, nina uzoefu wa kutosha wa soka la wanawake. Kuhusu chakula, kwa kusema ukweli, hapa Alliance, chakula ni kile kile wanachopangiwa hapa shule. Isipokuwa, tunapokuwa kwenye maandalizi ya mashindano, hawa wanaojiandaa kwa mashindano, kulingana na mazoezi tunayofanya, hao chakula chao kinaboreshwa kinakuwa tofauti kidogo ili kurudisha nguvu ile wanayopoteza. Kinasaidia kwa sababu unaona mchezaji anapotumia muda mwingi mazoezini, lazima apate chakula cha kurudisha ile nguvu aliyopoteza.
“Vyakula ni vilevile vya kawaida vya wanga, samaki, nyama, mihogo ya kuchemsha kwa ajili ya chai. Sekretarieti ya shule kwa kweli inajitahidi kwenye masuala ya lishe na chakula. Hii ni timu ya taasisi, hivyo inajiendeesha kitaasisi.”
Mwenyekiti wa Baobab Queens ya Dodoma, Innocensia Massawe anasema: “Gharama kubwa ya kambini ni chakula. Mtoto wa kike ana gharama kubwa kuliko wa kiume. Maisha ya shida hawajayazoea. Hatuwalishi sana vyakula vigumu. Tunafanya kulingana na bajeti ya mwezi, na bajeti ya mwezi lazima kuwa na samaki, kuku, nyama ya ng’ombe, mayai, mboga za majani. Mlo wetu kila siku lazima uwe na mboga za majani. Tunawapa chakula katika mzunguko kutokana na maumbile yao pamoja na mfumo wa jinsia yao. Hawawezi kuishi maisha magumu kama wanaume kwa sababu hawa ni wa kike, kwa hiyo tunawabadilishia sana. Mara nyingi dagaa tunawalisha mara moja kwa wiki kwa sababu ya stamina pamoja na wapate madini ya chuma, ambayo huyapoteza sana.
“Nyama ya mbuzi huwa hatuwalishi kwa sababu ya kuogopa kupata magonjwa ya miguu.”
Mshiriki wa mashindano ya mitumbwi mkoani Mwanza, Grace Charles anasema: “Sisi tunakula vyakula vya kawaida tu, tunakula ugali, mboga ambazo hazina mafuta, mboga za majani kwa wingi, maziwa na huwa hatuli kabisa nyama. Hatuna mafunzo yoyote ya kuhusu lishe, hivyo hivi vitu tunafanya sisi wenyewe tu.”
Nguli wa riadha wa mbio fupi na za kati, Lwiza John anasema: “Kwa mwanariadha wa mbio za mita 100 au 200 lazima uwe umeshiba, usiwe kimbaumbau, lazima uwe na nguvu. Mbio hizo fupi unatakiwa uende gym ili uwe mwenye nguvu. Mtu wa mbio za kati na kwenda juu naye pia gym anaingia, uvumilivu na ukakamavu ni kitu anachotakiwa kuwa nacho sana. Mafuta ni kitu muhimu sana kwa sababu, unapokimbia mwili unaounguza kiasi kikubwa cha mafuta, hivyo lazima upate ya kuja kurudisha pale palipopungua.
“Suala la chakula, kwenye riadha linatofautiana na vipindi. Kama ni kipindi cha maandalizi kwa maana ya kufanya mazoezi, wakati huo mwanariadha anaweza kula maharage, wali, ugali, mboga za majani zisipungue, ni hivyo. Lakini, kipindi cha mashindano, ninachoelewa mimi, mchezaji hawezi akala nyama ya ng’ombe kwa sababu mmeng’enyo wake unachukua muda mrefu, inameng’enywa taratibu hivyo mtu anaweza kupata tatizo kwenye misuli.
“Kwa hiyo maharage, samaki, kuku anaweza kula kwa sababu mmeng’enyo wake unafanyika kwa haraka. Kuhusu chakula hiyo ndiyo miko yake.”
Mwanariadha wa kike wa mbio ndefu wa Tanzania, Failuna Abdi Matanga anasema: “Kama mkimbiaji wa kike, ishu ya asile chakula gani, siwezi kusema asile nini isipokuwa kinachotakiwa, afanye mazoezi, aweke sawa mwili wake. Kwa mfano, leo unafanya mazoezi halafu unapumzika, unafikiri hii miili yetu inashukrani?
“Inachobidi afanya mazoezi kila siku, hata kama chakula atakachokula si chakula kinachofaa, afanye mazoezi kila siku. Sio kwamba usile chakula hiki, hapana. Sijui kwa wataalamu wengine, lakini kwangu mimi, tuseme kwa mfano leo umekula, kisha kesho kukufanya mazoezi, kilo zinaweza kuongezeka. Kwa mwanariadha, mafuta hayatakiwi sana, hata madaktari wanatuambia, tusitumie sana mafuta.
“Kwangu mimi kwa kuwa nafanya mazoezi kila siku, huwa natumia sana calcium kutokana na uzito wangu. Unapoona mwili umekuwa mwepesi sana, lazima kwenye chakula chako uweke calcium. Huwa nafanya hivyo.”
Bondia wa kike wa uzito wa Fly, Mtanzania Stumai Muki anasema: “Vyakula vipo ambavyo ni muhimu vinavyohitajika kwa ajili ya kuongeza nguvu, ila kwa mwenye uchumi wa chini, aliyekuwa na uongozi unaomsimamia na kuratibu lishe yake, basi unajikuta unakula tu chakula kile ambacho unachokipata ilimradi tumbo limepata kitu, na ukachukua maji yako ukanywa, kwa sababu tumbo halina kioo. Unakula zako mihogo unakuja mazoezini, ila kiukweli, vyakula vipo vinavyostahili kwa mwanamichezo hasa wa kike, ila changamoto tu ni ya kukosa kipato cha kutosha.”
Wataalamu wa lishe wanasemaje
Ofisa Lishe wa Hospitali ya Mawenzi RRH iliyopo Moshi, Ester Wazoel amechambua umuhimu wa lishe kwa wanamichezo wa kike, vyakula gani wanapaswa kula na vipi wasiguse kabisa kwa ajili ya kulinda viwango vyao michezoni.
“Kwa kawaida mwanamke anapaswa kutumia mafuta yatokanayo na mimea kwa ajili ya usalama wake. Kuacha kutumia vyakula vya kufungasha kwa haraka kama chipsi, kuku wa kukaanga na vingine vilivyokaangwa kwa muda mrefu na mafuta kwa sababu ya lehemu inayoweza kusababisha matatizo ya moyo na kuanguka michezoni”.
“Kinachopaswa, kiwango cha mafuta kinategemea na mazoezi anayofanya mchezaji. Ajiepushe pia na vinywaji vya viwandani kwa sababu vimeongezwa sukari ya ziada pamoja na dawa za kuhifadhi. Badala yake anywe maji, chai ya kijani na juisi ya matunda asilia,” anasema Wazoel. Itaendelea kesho.
Imeandaliwa na kushirikiana na Bill and Melinda Gates