Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Raundi 15 Championship zilivyobamba

CHAMPIONSHIP Pict

Muktasari:

  • Kwa upande wa timu nyingine zinahitaji kuongeza nguvu zaidi ili kujinasua na nafasi za hatari, kama ambavyo Mwanaspoti linaelezea matukio muhimu ya kuvutia na ya kusisimua yaliyotokea katika raundi hizi 15, zilizopigwa hadi sasa msimu huu.

BAADA ya raundi 15 kuchezwa Ligi ya Championship, ushindani umeonekana mkali kwa kila timu kuendelea kuonyesha uthabiti kwa kukusanya pointi muhimu, huku kukiwa na tofauti ndogo kuanzia inayoongoza hadi ya nne.

Kwa upande wa timu nyingine zinahitaji kuongeza nguvu zaidi ili kujinasua na nafasi za hatari, kama ambavyo Mwanaspoti linaelezea matukio muhimu ya kuvutia na ya kusisimua yaliyotokea katika raundi hizi 15, zilizopigwa hadi sasa msimu huu.

CHAMP 01

GEITA GOLD HAIKAMATIKI

Geita Gold ndiyo timu pekee hadi sasa katika Ligi ya Championship ambayo haijapoteza mechi yoyote msimu huu, kwani kikosi hicho kutoka mjini Geita kimeshinda 11 na kutoka sare minne kati ya 15 iliyocheza, kikiongoza msimamo na pointi zake 37.

Timu hiyo iliyoshuka daraja msimu wa 2023-2024, msimu wa 2024-2025 wa Ligi ya Championship ilimaliza ya nne na pointi 56, chini ya aliyekuwa Kocha Mkuu, Mohamed Muya na kushindwa kupanda Ligi Kuu Bara, baada ya kufeli mechi za mchujo (play-off).

Geita ilicheza mchujo kupanda Ligi Kuu Bara dhidi ya Stand United 'Chama la Wana' iliyomaliza nafasi ya tatu na pointi 61 na kushuhudia ikiondoshwa kwa jumla ya mabao 4-2, baada ya sare nyumbani ya 2-2, kisha kuchapwa ugenini 2-0.

CHAMP 02

KAGERA YAWEKA REKODI MPYA

Kagera Sugar imeweka rekodi mpya katika Ligi ya Championship msimu huu, baada ya kikosi hicho kinachonolewa na Juma Kaseja kushinda mechi tisa mfululizo, ikifuatiwa na Geita Gold na Mbeya Kwanza zilizoshinda mara nane kila mmoja.

Kagera iliyodumu katika Ligi Kuu Bara kwa miaka 20 tangu iliposhiriki 2005, ilishuka daraja msimu wa 2024-2025, baada ya kikosi hicho kushinda mechi tano, sare minane na kupoteza 17, ikishika nafasi ya 15, kufuatia kukusanya pointi zake 23.

Timu hiyo tangu ilipoanza ufunguzi wa Ligi ya Championship msimu huu kwa suluhu (0-0), dhidi ya maafande wa Transit Camp Oktoba 10, 2025, ilishinda mechi tisa mfululizo, ikiwa ni rekodi mpya kwa kikosi hicho kwani ilikuwa haijawahi kutokea.

Baada ya suluhu hiyo, Kagera ilizifunga Barberian mabao 2-1, (1-0) v Bigman FC, (4-1) v African Sports, (4-0) v Stand United, (2-0) v Polisi Tanzania, (1-0) v B19 FC, (3-1) v Hausung FC, (1-0) v TMA FC, kisha kuichapa Mbuni FC mabao 2-0.

Kwa sasa timu hiyo inashika nafasi ya pili na pointi 36, baada ya kushinda mechi 11, sare mitatu na kupoteza mmoja kati ya 15, iliyocheza, ikifunga mabao 28 na kuruhusu manane, nyuma ya vinara Geita Gold kutoka mkoani Geita yenye pointi 37.

CHAMP 03

HAUSUNG YAPEWA USHINDI WA BURE

Katika raundi 15 zilizochezwa hadi sasa, Hausung ndiyo timu pekee iliyopata ushindi wa bure wa mabao 3-0 na pointi tatu msimu huu, baada ya mechi ya kikosi hicho dhidi ya Stand United 'Chama la Wana' kushindwa kufanyika, Novemba 8, 2025.

Mechi hiyo ya raundi ya nne ilishindwa kufanyika Novemba 8, 2025, kwa mujibu wa ratiba iliyopangwa baada ya Stand United kushindwa kusafiri kwenda kwenye Uwanja wa Amani uliopo Mkoa wa Njombe, kwa kile kilichodaiwa kuandamwa zaidi na ukata.

Hata hivyo, Novemba 12, 2025, Bodi ya Ligi Kuu Bara (TPLB), ilitoa taarifa ya kuipa ushindi wa bure Hausung wa mabao 3-0, na pointi tatu, baada ya kikosi hicho cha Stand kushindwa kufika kwenye Uwanja huo wa Amani bila ya sababu za msingi.

Pia, Stand United ilitozwa faini ya Sh10 milioni, huku mwenyekiti wa kikosi hicho, Stivian Antitius akifungiwa mwaka mmoja kwa kosa la klabu hiyo kushindwa kabisa kufika uwanjani kwa kuzingatia kanuni ya 31:1 (1.1, 1.2, 1.3 & 1.4) ya Championship.

Ushindi huo wa Hausung iliyopanda daraja kwa msimu huu wa 2025-2026, ulikuwa wa kwanza baada ya timu hiyo kuchapwa mechi tatu mfululizo, ikianza na bao 1-0, dhidi ya African Sports, (2-0) v Polisi Tanzania, kisha kuchapwa tena 3-1 na Mbuni.


MAKOCHA SABA WATIMKA

Hadi sasa tayari imeshuhudiwa makocha saba wakiachana na timu walizoanza nazo msimu huu kutokana na mwenendo mbaya wa matokeo, akianza Sharifu Joseph Ndokezi wa African Sports, kisha akafuatia, Babou Salim aliyekuwa anaifundisha B19 FC.

Makocha wengine ni Hussein Rupia aliyeifundisha Hausung ya Njombe aliyoipandisha daraja msimu huu baada ya kikosi hicho kuongoza First League kikitokea kundi A na pointi 25, kikiungana na Gunners ya Dodoma iliyoongoza kundi B na pointi 35.

Wengine ni kocha wa zamani wa Azam FC, Pan Africans na Cosmopolitan, Idd Nassor 'Cheche', aliyeachana na Stand United, Habibu Kondo (TMA FC), Moris Katumbo 'Kamongo' (Barberian FC) na Juma Ikaba aliyekuwa anaifundisha Gunners FC ya Dodoma.


HAT-TRICK MBILI

Wakati ikisubiriwa kuanza kwa mechi za raundi ya pili, ila hadi sasa tayari zimeshafungwa (Hat-Trick) mbili, ikibakia nne ili kuifikia rekodi iliyowekwa msimu wa 2024-2025, wa Ligi ya Championship, ambao tulishuhudia nyota sita wakifunga.

Mshambuliaji wa Kagera Sugar, Mzambia Obrey Chirwa ameweka rekodi ya mchezaji wa kwanza wa Ligi ya Championship msimu huu kufunga mabao matatu (Hat-Trick), wakati kikosi hicho kilipoifunga Hausung kutoka Njombe mabao 3-1, Desemba 2, 2025.

Katika mechi hiyo iliyopigwa kwenye Uwanja wa Kaitaba Bukoba, mshambuliaji huyo wa zamani wa Yanga, Azam, Namungo, Ihefu ambayo kwa sasa Singida Black Stars na KenGold, alifunga mabao hayo na kufikisha idadi ya manane akiwa na kikosi hicho.

Nyota mwingine aliyefunga (Hat-Trick) ni Boniface Mwanjonde wa Mbeya Kwanza aliyekifungia kikosi hicho katika ushindi wa mabao 5-0, dhidi ya B19 FC, Desemba 17, 2025 na mshambuliaji huyo amejiunga na Fountain Gate inayoshiriki Ligi Kuu.

Mshambuliaji huyo amehusika na mabao 13, katika mechi 14, alizoichezea Mbeya Kwanza, baada ya kufunga tisa na kuasisti manne, akionyesha kiwango kizuri kilichowavutia mabosi wa Fountain Gate kumsajili katika dirisha dogo la Januari 2026.

CHAMP 04

VITA YA UFUNGAJI

Sehemu nyingine inayovutia ni katika vita ya ufungaji bora na  mshambuliaji wa maafande wa Transit Camp, Adam Uledi, ndiye anayeongoza baada ya kufunga mabao 11, akifuatiwa na Boniface Mwanjonde aliyeifungia Mbeya Kwanza aliyoachana nayo tisa.

Mwanjonde amejiunga na Fountain Gate dirisha hili la Januari 2026, baada ya kuonyesha kiwango kizuri msimu huu na Mbeya Kwanza, huku wanaofuatia ni Abrahaman Mussa wa Gunners FC na Obrey Chirwa wa Kagera Sugar wenye manane kila mmoja.

Nyota wengine wanaofuatia kwa kufunga mabao mengi msimu huu ni Raymond Lulendi anayekichezea kikosi cha Songea United, Maulid Shaban (Geita Gold), Ramadhan Hashim (B19 FC) na Joseph Ambokege wa Mbeya Kwanza, waliofunga saba kila mmoja wao.