Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Pipino na hesabu kubwa Ligi Kuu, amtaja Fei Toto

Muktasari:

  • Katika mahojiano baina yake na Mwanaspoti anafafanua maana ya jina la Pipino kuwa ni tango lenye asili ya Italia, ambapo ukoo wake una uhusiano wa mbali na uzungu.

UKITAJA majina ya wachezaji waliofanya vizuri katika Ligi Kuu msimu uliopita jina la kiungo mkabaji wa KMC, Ahmed Bakari  ‘Pipino’ ni miongoni mwao. Alionyesha kiwango kikubwa kilichozivutia baadhi ya timu kuhitaji huduma yake.

Katika mahojiano baina yake na Mwanaspoti anafafanua maana ya jina la Pipino kuwa ni tango lenye asili ya Italia, ambapo ukoo wake una uhusiano wa mbali na uzungu.

“Pipino ni jina la ukoo lina maana ya tango. Limeanzia mbali kwa mababu zetu, walikuwa na asili ya kizungu, ila siwezi kujua sana mambo ya zamani nasikiaga wakisimulia,” anasema. 

Pipino aliyezaliwa Februari 27, 2005 anasema kilichomsaidia kufanya vizuri msimu uliopita ni nidhamu, kujituma na kujifunza kila wakati. Natarajia msimu huu kuwa bora zaidi ya uliopita, nahitaji kupiga hatua na kukua ili niweze kuzifikia ndoto za kuwa mchezaji mkubwa.”


SIMBA, YANGA, AZAM

Pipino ni miongoni mwa wachezaji waliohusishwa na timu za Simba, Yanga na Azam FC kuhitaji huduma yake na analifafanua hilo akieleza kitu gani kilikwamisha asiende huko.

“Taarifa za kutakiwa Simba, Yanga na Azam zilikuwa za kweli, nilikuwa na mkataba na KMC, hivyo viongozi ndio walikuwa wanazungumza na timu hizo, nadhani kilichokwamisha ni maslahi baina yao,” anasema na kuongeza;

“Wakati dirisha la usajili lilipokaribia kufungwa, Simba iliongeza nguvu kutaka kunisajili, lakini ikashindikana, mazungumzo yalikuwa baina ya timu hizo, ndiyo maana nimeendelea kusalia KMC.”

Anasema kwa namna alivyokuwa akiona anazungumzwa katika mitandao ya kijamii, ilimpa moyo kuamini kazi yake inaonekana na kupendwa na watu. “Taarifa za kuhusishwa na klabu hizo kubwa, nilikuwa naona watu wanavyoniona ni mchezaji mwenye kipaji, ilinipa nguvu ya kujituma zaidi.”

Ingawa msimu uliopita alijiunga na KMC kupitia usajili wa dirisha dogo na ilikuwa mara ya kwanza kucheza Ligi Kuu Bara akitokea Magnet, alionyesha kiwango cha juu.

“KMC ni timu ya kwanza kuichezea katika Ligi Kuu na nimewahi kupitia JK Park kabla ya kujiunga na Magnet iliyonifikisha hatua niliyopo, ndiyo maana nasisitiza bado nina safari ndefu ya kuendelea kujifunza mambo mengi,” anasema Pipino na kuongeza;

“Mpira wa miguu unahitaji nidhamu kwa kila kitu, nimejifunza kupambana zaidi na mechi yangu ngumu ingawa haikuwa katika Ligi Kuu ni ya timu ya taifa ya Tanzania ‘Taifa Stars’ dhidi ya Mauritania ambayo niliumia jicho, nilihisi maumivu makali niliyokaa nayo kwa wiki moja.

“|Safari yangu ya soka nilianza kucheza mpira wa makaratasi, waliokuwa wananitazama nikicheza walikuwa wananiambia nina kipaji kikubwa hadi wakapatikana watu wa kunipeleka JK Park.”


JOB, FEI,  AUCHO

Anasema mastaa waliowahi kumfuata na kumwambia ana kipaji kikubwa, anachotakiwa kukifanyia kazi kwa kujituma, kutunza kiwango na kuzidisha nidhamu,  ni beki wa Yanga, Dickson Job.

“Kwanza ni mchezaji ninayemkubali, aliwahi kuniita na kuniambia anaona ninacheza vizuri, ili nifike mbali napaswa kuzingatia nidhamu ya ndani na nje ya uwanja, kubwa zaidi alinisisitiza niweke akili na nguvu katika kazi yangu akiamini nitafika mbali,” anasema Pipino na kuongeza;

“Mchezaji ninayetamani  itokee siku moja kucheza naye timu moja ni kiungo mshambuliaji wa Azam, Feisal Salum ‘Fei Toto’, ana kipaji kikubwa ana uwezo wa kuichezesha timu na kufunga.”

Anamtaja mchezaji anayevutiwa naye katika nafasi anayocheza ni kiungo mkabaji wa Singida Black Stars, Khalid Aucho. “Anatumia akili kubwa kufanya uamuzi na kuepuka kadi, ni kati ya mastaa niliokua nawaangalia na kujifunza baadhi ya vitu kiufundi, na shujaa wangu tangu nikiwa mdogo ni Paul Pogba.”

KOCHA MAXIMO

Anasema ujio wa kocha Marcio Maximo, raia wa Brazil umeongeza kitu kikubwa katika maisha yake ya mpira wa miguu, kutokana na mbinu anazowapa ili kuwa wachezaji bora.

“Ni kocha mwenye CV kubwa amewahi kuifundisha Taifa Stars na Yanga, kuna namna anavyotujenga kuwa wachezaji wakubwa, kuanzia katika mazoezi, mechi na maisha ya kawaida, anatutia moyo na kusimama nafasi ya mzazi, jambo linalochochea kujituma na kupenda kujifunza kwa bidii,” anasema.

PESA YA KWANZA KUBWA

“Mwaka jana katika mashindano ya CECAFA ya U-20 tulifanya vizuri tulipewa bonasi ya Sh1.5 milioni kila mmoja, makocha walituambia wanatupa muda wa saa moja kwenda kufanya manunuzi, niliichukua ile pesa na kwenda kumpa baba nyumbani, kisha nikarejea kambini,” anasema Pipino na kuongeza;

“Nilikuwa sijawahi kuishika pesa kama hiyo na tulipewa mkononi, ikanipa nguvu ya kuongeza bidii katika kazi hiyo, mimi ni kijana wa mwisho kuzaliwa kati ya watoto watatu na wa kiume pekee, unaweza ukaona ni kazi ya ziada kuhakikisha naisaidia familia yangu.”

Mbali na hilo anasema mchezo anaoupenda ni ngumi na asingeona mwanga katika mpira wa miguu basi angekuwa bondia: “Mabondia ninaowapenda ni Ibrahim Class na Hassan Mwakinyo pia wapo wa nje ambao nawafuatilia.”