Pep na wenzake wasaka mbinu za kuikabili real Madrid hadi usiku mnene
KATIKA toleo lililopita katika kitabu cha Pep Confidential, mwandishi Marti Perarnau aliuchambua mchezo wa Bayern na Real Madrid jinsi ulivyoisha kwa Bayern kulala jambo lililoibua mjadala kuhusu staili ya uchezaji ya kocha Pep Guardiola. Sasa endelea…
Kimsingi Bayern ilicheza katika namna ya kipekee ya ubora isipokuwa tatizo kubwa lilikuwa katika umaliziaji uliokuwa wa hovyo, na licha ya mapungufu ya wageni katika mechi hiyo, hoja kubwa iliyozungumzwa kwenye vyombo vya habari ni bao la Benzema pamoja na nafasi mbili za Ronaldo na Di Maria.
Kulikuwa na pongezi chache mno zilizohusu uwezo wa Bayern kutawala mchezo katika mechi hiyo na umahiri wa wachezaji wa timu hiyo kiuchezaji na kuonekana ni moja ya mambo makubwa duniani. Uchambuzi huo ulionekana kutokuwa hitimisho sahihi. Katika tukio lile lile la mara kwa mara, Pep kwa mara nyingine alijikuta akiwa katika mshtuko wa utamaduni wa Kijerumani pamoja na soka la asili ya Ujerumani. “Naelewa aina hii ya uchezaji si katika utamaduni wa soka la Ujerumani,’’ alitoa ufafanuzi huo wakati wa chakula cha jioni baada ya mechi.
“Watu ni lazima wafahamu hilo nalielewa, hapa Ujerumani klabu zinapenda kucheza staili ya soka ambayo ni tofauti na staili yangu na hapana shaka watu wanapenda staili ya uchezaji soka la Madrid au Dortmund.”
“Lakini jamaa wa Bayern wamenichagua mimi, hapo nalazimika kuwa katika hali ya kukubaliana kati ya mawazo yangu na yale ya soka la Ujerumani lakini mwishowe ni aina ya wachezaji ulionao, hilo ndilo jambo la msingi kuzingatia na naweza kukwambia kitu, wachezaji wanaunga mkono mawazo yangu.”
Unaweza kutafsiri huu mgongano wa kitamaduni katika soka kwa namna unavyoona sawa, iwe ni kwa uzuri au ubaya lakini huo ndio uhalisia, kama Bundesliga soka lao lina husisha zaidi mashambulizi mazuri ya kushtukiza na kukimbia moja kwa moja, hapo utaona mambo ya Pep yanakinzana na hayo.
Staili ya Pep ya uchezaji ya kukaba maeneo inahusisha utaratibu ulio wazi wa washambuliaji namna wanavyojipanga na hapo kuna suala zima la kuwa makini na wenye nguvu katika maeneo ya mbele ya uwanja, ni kama vile wapanda mlima walio katika kamba moja, wanakwea kilima hatua kwa hatua katika utaratibu uliokamilika.
Ni mfano unaohusisha falsafa inayoruhusu kujirudi kwa kuanzia nyuma kwa mara nyingine pale inapotokea mpango wa awali kukwama, haijalishi ni pasi ngapi mnacheza kwa nia ya kumvuruga mpinzani wenu badala yake mnatakiwa kuendelea kupasiana.
Ni jambo ambalo isingewezekana liepukwe kutokea, ni jambo la kawaida kulitokea mlinganio uliokuwa ukifanywa kati ya aina hii ya uchezaji ya Pep na utamaduni wa soka la Ujerumani.
Baada ya kupata chakula cha jioni mjini Madrid katika Hoteli ya Intercontinental, Rummenigge na Matthias Sammer waliungana na benchi la ufundi la timu yao kwenye meza moja, lengo lilikuwa ni kuongeza hamasa na ari ya ushindi kwa kocha.
Walikuwa na wasiwasi kocha alikuwa katika hali ya kukata tamaa na kumsihi asiachane na mawazo yake, walikuwa na imani naye kwa asilimia 100 pamoja na wachezaji wake na mipango yake katika mechi ambayo iliwafikisha hatua waliyofika.
Walimsisitizia klabu ina dhamira ya dhati ya kuunga mkono mawazo na fikra zake na kutaka kuziendeleza fikra na mawazo hayo katika miaka michache ijayo. Pep, Domenec Torrent na Carles Planchart walitumia saa nyingine zilizofuata wakiichambua mechi na kuijadili katika namna bora ambayo ingeweza kuwapa mafanikio katika mechi ya marudiano.
Kocha Pep anakumbusha ingekuwa vizuri kuanza na mabeki watatu wa kati nyuma na kuwa na utawala mkubwa katika eneo la kati ya uwanja ili kuwa na nguvu na hatimaye kupunguza nafasi ya Madrid kufunga mabao ya mbali.
Walifanyia kazi mambo hayo hadi usiku mnene na mwishowe Pep akamtaka Torrent kuhakikisha habadili mawazo bila kujali chochote kitakachojitokeza. Pep anajua fika ni vipi anataka timu hiyo icheze na hataki kuona anabadili mipango yake.
Pep hajakata tamaa kwa sababu ya kufungwa au matokeo ya shutuma alizokuwa akipewa, ukweli alikuwa ndio kwanza amepokea taarifa za daktari akimwarifu kuhusu hali ya afya isiyo ya kuridhisha ya Kocha Tito Vilanova.
Itaendelea Jumamosi ijayo…