PAUL PETER; Straika tegemeo JKT Tanzania aliyefichua ugumu kuzifunga Simba, Yanga
Muktasari:
- Mwanaspoti lilifika katika kambi ya JKT Tanzania na kufanya mahojiano maalum na mchezaji huyo ambaye msimu huu 2025/26 ameweka rekodi ya kuifunga Azam FC kwa mara ya kwanza, huku akiweka wazi safu ya ulinzi iliyowahi kumtesa zaidi tangu aanze kucheza Ligi Kuu.
MSHAMBULIAJI wa JKT Tanzania, Paul Peter, ambaye amewahi pia kuichezea Azam FC na Dodoma Jiji, amefunguka kuhusu safari yake ya soka, ugumu wa kucheza dhidi ya vigogo Simba na Yanga, pamoja na siri iliyomvutia kutua katika kikosi hicho cha Wazee wa Mapigo na Mwendo.
Mwanaspoti lilifika katika kambi ya JKT Tanzania na kufanya mahojiano maalum na mchezaji huyo ambaye msimu huu 2025/26 ameweka rekodi ya kuifunga Azam FC kwa mara ya kwanza, huku akiweka wazi safu ya ulinzi iliyowahi kumtesa zaidi tangu aanze kucheza Ligi Kuu.
Pia analieleza gazeti hili siri iliyomvutia kuichezea JKT (Wazee wa Mapigo na Mwendo), kwani baada ya kumaliza msimu uliopita wa 2024/25 kwa rekodi nzuri ya mabao manane na asisti mbili, ofa zilimiminika na anaeleza aliwezaje kuzikwepa.
KUTOKA KITAANI HADI AZAM
Anasema kipaji chake kilianzia mtaani, wakati huo akiishi Sinza, jijini Dar es Salaam, mpaka alipopata kaka wa rafiki yake aliyemuingiza Azam kwa ajili ya majaribio.
“Kuna rafiki nimesoma naye, kaka yake alikuwa anafanya kazi Azam, kwa hiyo watu pale mtaani wakawa wanamwambia anisaidie. Siku moja akanipigia simu nikafanye majaribio.
“Wakati huo nimeshamaliza kidato cha nne, nikaingia chuo ila sikuweza kuendelea tena na harakati za masomo, nikaona nijaribu bahati Azam na nikapita.
“Niliwadanganya tu nyumbani mpaka wakaniacha nifanye ninachotaka. Kwa hiyo nilivyopita nikawa natoka Sinza mpaka Azam kufanya mazoezi, mpaka miezi miwili ndipo nikachaguliwa kwenda kambini.”
MAISHA AZAM
Anasema hayakuwa maisha mabaya kwa sababu ndio waliomshika mkono na kumfanya awe hapo alipo, kwani safari yake ya soka ndipo ilipoanzia.
“Sikufanya vizuri kwa sababu nilikuwa bado kijana mdogo na haikuwa rahisi wakati huo kupata nafasi, bosi anataka kuona waliosajiliwa wanafanya makubwa.
“Mwisho nikaamua kuondoka, kwa sababu ishu ilikuwa ni kupata nafasi. Nikaenda Dodoma. Azam nilikuwa napata hela kwa wakati lakini sichezi na kazi yangu ni kucheza."
AZAM ILINILIZA
“Wakati nimepandishwa kuichezea Azam, nakumbuka nilicheza mechi moja tu Uwanja wa Uhuru na nilianzia benchi, ila nyingine zote nilikuwa jukwaani.
“Yani kati ya mechi 15 nimecheza moja tu, kama mchezaji hilo lilikuwa linaniumiza sana. Nikiwa peke yangu nalia kabisa, najiuliza kwa nini imekuwa hivi.
“Kocha alikuwa Etienne Ndayiragije, ilikuwa ngumu wakati ule kwa mchezaji kutoka timu B kuanza kucheza tu moja kwa moja. Anataka kuona pesa yake aliyoweka (kusajili) inafanya kazi, huku wewe pia ni mchezaji mdogo.”
KUIFUNGA AZAM
Paul ambaye msimu huu aliifunga Azam kwa mara ya kwanza anasema hawezi kufurahia kuifunga, ila kwa kuwa yuko kazini lazima atimize majukumu yake kama mchezaji.
Bao aliloifunga Azam ni katika mchezo wa Ligi Kuu Bara wa Oktoba Mosi kwenye Uwanja wa Meja Jenerali Isamuhyo, jijini Dar es Salaam, akifunda dakika za mwisho kuisawazishia timu yake na kutoka sare ya bao 1-1.
“Kwanza nilishajiwekea siwezi kushangilia nikifunga Chamazi. Azam ni familia, bila wao nisingefika hapa. Kwa hiyo ujue ukikulia kwenye akademi kuna malezi ya soka ya tofauti unakuwa nayo.”
UGUMU KUZIFUNGA SIMBA, YANGA
Katika rekodi zake, Paul amebakiza timu chache zinazoshiriki Ligi Kuu Bara ambazo hadi sasa hajazifunga kabisa, zikiwemo Simba na Yanga.
“Unajua natamani nifunge, pia Watanzania hawaamini kama wewe ni mchezaji mzuri hadi uzifunge Simba na Yanga, na hiyo ni kwa sababu hawafuatilii mechi za timu ndogo.
“Lazima kwanza uweze kuwafunga hawa wachezaji wa ‘level’ yako kabla ya kwenda kushindana na wale wakubwa. Wapo wanaokamia mechi hizo kubwa na kufunga lakini zingine hawana maajabu.
“Mimi sipendi kuzikamia mechi kubwa ili nionekane, ila nahakikisha kwenye ngazi yangu nimefanya makubwa na nimeongezeka kiwango, ili hao wakubwa iwe rahisi kuwachapa pia.”
BEKI NGUMU ZAIDI
Paul ambaye ameichezea Ligi Kuu Bara kwa takribani miaka mitano ameweka wazi Yanga ndiyo timu yenye safu ngumu zaidi ya beki.
“Yanga ndiyo safu ngumu zaidi kwa upande wangu, halafu wamejitahidi kuchaguana. Yani mabeki wao wana uzoefu mkubwa ambao huwezi kuwapita kirahisi.
“Pale walifanya skauti nzuri ya mabeki wao wa kati, watu kama Bakari Mwamnyeto, Ibrahim Bacca na Dickson Job. Hawa ni Waswahili wenzetu tofauti na wageni, kwa hiyo tunawajua na kuna vitu Mungu amewajalia.”
MAISHA YA DODOMA
Anasema alifika Dodoma Jiji kwa mkopo na kabla ya kwenda hapo viongozi walimuita na kumshawishi kama atapata timu kubwa basi atokee pale.
“Nilikubali kwenda Dodoma wakati huo iko chini ya Kocha Masoud Juma. Msimu mzima nikafunga bao moja tu na asisti kama mbili hivi na msimu ulivyoisha ndiyo mkataba wangu wa mkopo ukaisha.
“Bahati nzuri viongozi waliniita na kuniambia hata kama sijacheza bado wananihitaji ni baki na wakaniambia wananiamini.
“Kwa hiyo imani yao kwangu ikanipa nguvu ya kuendelea kukaza na nikaongeza misimu miwili. Kwa hiyo mwaka unaofuata nikafunga mabao matatu na mwaka wa pili mabao manane na asisti mbili.”
SIYO KWELI
Paul ambaye alizua utata msimu uliopita baada ya maneno kuwa mengi, huku ikisemekana alisaini mkataba JKT Tanzania wakati hajamalizana na Dodoma, anajibu:
“Hapana siyo kweli, wakati ule nilikuwa sijasaini ila nilikuwa kwenye maongezi nao kwa sababu mkataba wangu bado haujaisha.
“Nilipewa ushauri wakati mkataba wangu uko ukingoni kama kuna timu ndogo zaidi ya Dodoma ikinitaka nisikubali, ila kubwa sawa niende.”
MAISHA YA JKT
Anasema kulinganisha na timu alizotokea, JKT ina afadhali kubwa kwa sababu anapata kila kitu kwa wakati.
“Maisha ya JKT ni mazuri, lakini hata malengo yangu yameongezeka. Niliyoyafanya mwaka jana huu uwe zaidi ili niweze kukamilisha majukumu yangu kama mchezaji.”
KILICHONIVUTIA JKT
Anaweka wazi kilichomvutia zaidi ni mbinu za mwalimu ambazo zinaweza kumfanya mchezaji yoyote awe bora na kuinua kiwango chake.
“Napenda timu inavyocheza. Dodoma tulikuwa tunapata matokeo lakini hapa unacheza na mtu, unaonyesha kipaji chako na watu wanakuona.
“Nikaona bora kuja hapa na timu inavyocheza itakuwa rahisi kushirikiana na wenzangu, lakini hata mimi mazoezi na nidhamu ya hapa vitakuza kipaji changu.”
UTOFAUTI UKO HAPA
Paul ambaye amepitia Azam na Dodoma kabla ya kutua JKT Tanzania anasema utofauti wa hizo timu mbili alizotoka ni nafasi ya kucheza na maokoto.
“Mchezaji yeyote kabla ya pesa, furaha yake ni kucheza. Kwa hiyo kama hupati nafasi basi huwezi kuona thamani yako. Japokuwa Azam maisha mazuri na mnalipwa kwa wakati ila sikuwa nacheza.
“Dodoma hapa unapata nafasi ya kucheza lakini mfukoni hakuna kitu. Watu wanakuona kwenye TV wanadhani una hela, lakini familia pia inasubiri chakula kwako ila mshahara haujaingia.”
UGUMU WA NAMBA
Anasema katika timu mpya aliyoanza kuichezea hivi karibuni ugumu upo na wachezaji wanaocheza nafasi kama yake ni wengi zaidi.
“Unajua hapa wachezaji tuko wengi, kwa hiyo ugumu upo. Timu nzima tuko kama 40 hivi, kwa hiyo kila eneo lazima kutakuwa na watu wa kutosha na wenye uzoefu.
“Ukipata nafasi unatakiwa utoe 200% siyo 100% tu, na unatakiwa ufuate maelekezo kwa sababu kocha amenyooka na hataki ufanye ambacho hajakuelekeza.
“Ana mipango sana, huwezi kukuta kwenye timu yetu mtu anapiga chenga nyingi. Kama ni kukimbia au kutoa mpira kila kitu kinafanywa kwa maelekezo.”
AMERITHI
Paul anasema:
“Mpira nimerithi kwa marehemu baba yangu, maana ndugu wengi wananiambia nafanana namna ya kucheza na mzee wangu.
“Ila kwa kumbukumbu zangu, waliachana na mama nikiwa mdogo. Kwa hiyo alikuwa akitaka kuniona anakuja uwanjani nikiwa nacheza na wenzangu, ananipa zawadi ya mpira.
“Hajacheza ngazi kubwa ila sikupata nafasi ya kujua aliwahi kucheza wapi. Ila na mimi pia mwanangu wa kiume amerithi, maana humwambii kitu bila mpira.”
MAFANIKIO
“Mpira umenipa familia na marafiki hawa. Kila nilichonacho ni matokeo ya soka kuanzia gari na namna ninavyoendesha maisha kwa jumla, hadi ndugu wasionijua wamenifahamu.”
WAZAWA WOTE
JKT Tanzania ni miongoni mwa timu chache katika ligi yenye wachezaji wote wazawa ukilinganisha na zingine ambazo zinachanganya.
“Nilichopenda kwa JKT ni wanaamini kupitia wazawa kwamba wana kitu. Muda mwingi wageni wanafanana na sisi ila hela tu. Mchezaji yeyote mpe hela na nafasi, baasi.
“Mimi ukinipa pesa ndogo siwezi kutulia. Mambo ni mengi na familia zinatusubiri, halafu hapo hapo mgeni unakwenda kumpa pesa ndefu, nitajisikia vibaya.”
WAGENI UTATA
“Sasa hivi kuwa na wageni wengi kwenye hizi timu kubwa nne kumeshaanza kuleta shida. Unakuta mechi moja wanacheza wageni tisa, wazawa wawili.
“Mfano mimi nimetoka hapa nimeenda Singida kwa mfano, kila siku wageni wanaongezeka na wanaanza wengi kucheza kikosi cha kwanza. Wazawa, kipa labda. Hii inawakatisha tamaa wachezaji wengi.
“Nchi zingine kama za Uarabuni wageni mwisho watano au wanne. Hii inasaidia hata kwenye timu ya taifa zinakuwa vizuri. Hizi kubwa haziangalii mambo hayo, wenyewe wanataka matokeo.”
STARS PATAMU
Paul ameitwa kwa mara ya kwanza safari hii baada ya kocha kubadilishwa na kuwa Miguel Gamondi, anasema amependa kutumikia taifa lake na imempa morali.
“Imeniongezea thamani kubwa kuitwa timu ya taifa. Hata msimu uliopita nilipokuwa nafanya vizuri sikuitwa. Wengi walikuwa wanahoji mpaka wananiuliza kama nina ugomvi na TFF.
“Lakini lilikuwa ni suala la muda. Unajua Mungu ana mipango yake. Ukifanya vizuri watu wanaona na kupongeza pia na kuona aibu.”
BIASHARA FRESHI
Paul ambaye aliacha chuo cha biashara na kukimbilia soka, anasema kwa sasa hana malengo ya kurejea shule kwa haraka, ila ikibidi ataendelea alipoishia.
“Tuombe Mungu, mpira huu unanibana kidogo, ila nikipata nafasi baadaye nitarudi kujifunza mambo ya biashara kwa sababu ndiyo jambo ninalopenda kulifanya zaidi nje ya soka.
“Mpira ni kazi ya muda mfupi, kwa hiyo lolote litakalotokea hapa katikati nitaanzisha biashara zangu ili nifanye ninachokipenda kingine.”