Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Omary Marungu afichua viongozi Simba walivyotibua dili lake

MARUNGU Pict


JINA la Omari Marungu lilikuwa miongoni mwa sajili zilizotajwa kujiunga na Simba msimu huu, ikiwa ni moja ya mapendekezo ya aliyekuwa kocha wa timu hiyo, Fadlu Davids.


Hata hivyo, mshambuliaji huyo wa Mtibwa Sugar hakutua Msimbazi kama ilivyotarajiwa na sababu hazikuwekwa wazi.


Mwanaspoti limefanya naye mazungumzo na amefunguka mambo mbalimbali, ikiwamo kushindwa kutua Simba licha ya kupata ofa ya kuitumikia timu hiyo.


DILI LA SIMBA LILIKWAMA HAPA

Anasema dili hilo lilianza kwa mazungumzo baina yake na Kocha Fadlu na wakati ikitarajiwa anatua Msimbazi, mambo yakaenda kombo akitaja tatizo lilikuwa kwa viongozi.

“Ni kweli kulikuwa na mpango wa mimi kucheza Simba na kila kitu kilienda vizuri, kuna vitu vichache vilikwamisha mpango huo na ndiyo maana nimeendelea kucheza Mtibwa Sugar,” anasema na kuongeza;

“Si sahihi kuyaweka wazi sasa kwani dirisha hilo lilishapita na mimi nilikubali, pia si kazi yangu kuzungumza, mimi natakiwa kucheza, hayo nilimwachia meneja wangu ambaye huenda hakuona sababu ya kuyaweka wazi.”

MARU 01

YEYE NA FADLU DAMU DAMU

Pamoja na Marungu kushindwa kuwa sehemu ya kikosi cha Fadlu, kocha huyo ambaye hayupo nchini bado anaendelea kumfuatilia mshambuliaji huyo na kumkumbusha nini anatakiwa kufanya ili awe bora, jambo ambalo anafurahia.

“Bado naendelea kuwasiliana na Fadlu, amekuwa akinisisitiza kupambana na kuamini katika kipaji nilichonacho, pia nisichoke kupambana ili nifikie malengo,” anasema na kuongeza;

“Ppia amekuwa akinipa mbinu mpya kila tunapowasiliana ili niweze kufanya kile anachokiamini kutoka kwangu. Naamini imani yake kwangu inaniongeza nguvu.”

MARU 06

ANAVAA LAKI TATU

Kwenye ishu ya mavazi, wapo nyota wengi wa soka wanaopenda kupendeza akiwamo yeye na anasema bajeti yake ya mavazi ukimtazama juu hadi chini si bei ndogo na kuwataja mastaa wanaomvutia wakipiga pamba.

“Sina gharama kubwa sana kwenye kununua nguo. Siwezi kutaja bei ya nguo moja moja, lakini nikisema nipange bajeti kuanzia chini hadi juu haizidi laki tatu,” anasema na kuongeza;

“Hapo ni kuanzia T-shirt, jeans na viatu, naweza kutumia laki tatu, lakini inategemea aina ya nguo. Kuhusu nyota ambao nimekuwa nikiwatazama na kuvutiwa nao kwa namna wanavyotupia, siwezi kuacha kumtaja Idd Nado, Lusajo Mwaikenda na Zuberi Foba, wote wanakipiga Azam FC.”

Marungu pia amemtaja David Kameta ‘Duchu’ na Awadh Salum huku akiweka wazi kwa upande wa mastaa wanaocheza soka nje ya Tanzania amekuwa akimtazama Rafael Leao anayecheza AC Milan.

MARU 02

MSUVA, SUAREZ WAMPA MBINU

Anasema hadi kufikia alipo sasa amejifunza mengi kutoka kwa baadhi ya nyota anaowafuatilia huku akiwataja Simon Msuva na Luis Suarez wa Inter Miami ndiyo wanaomvutia na wamempa madini mengi.

“Nimezaliwa na kipaji na ili niwe mchezaji kwani ndiyo ndoto yangu tangu nikiwa na umri mdogo, sijui kama siyo soka ningekuwa nani. Nilipata sapoti kubwa kutoka kwa familia yangu kwani wao pia ni watu wa mpira,” anasema na kuongeza;

“Hadi nimefikia hapa kuna watu nimekuwa nikiwatazama ili kujifunza vitu vipya; kwa wachezaji wa ndani nimekuwa nikimtazama sana Simon Msuva, ni miongoni mwa wachezaji bora ambao nimekuwa nikiwaangalia kujifunza vitu kwani amenitangulia kuingia kwenye mpira;

“Pia nimekuwa nikimtazama mshambuliaji wa Inter Miami, Luis Suarez. Ni mchezaji ambaye licha ya umri wake kwenda, lakini bado ana ubora na anafanya mpira uonekane rahisi; nimekuwa nikitenga muda wangu kumfuatilia.”

MARU 03

BANDA AMPA KASHIKASHI

Anasema amekutana nmabeki wengi lakini hajaona msumbufu na tishio kwake, lakini kwa Abdi Banda anakiri alipa tabu walipocheza na Dodoma Jiji.

“Sijabahatika kukutana na beki ambaye ni msumbufu akawa tishio kwangu, lakini nakutana na mabeki wanaonizidi ujanja nikiwa na mpira na kufanikiwa kunipora au kuniondoa kwenye nafasi,” anasema na kuongeza;

“Unaweza ukawa kwenye nafasi beki akakuwahi akaondoa au kuharibu mipango, huwezi kusema huyo ni msumbufu; hizo ndizo nakutana nazo mara nyingi, lakini kuna mechi nakumbuka tulicheza dhidi ya Dodoma Jiji nilikutana na kashikashi kutoka kwa Abdi Banda, huyu ndiye naweza kumtaja kuwa alinipa shida.”

MARU 04

JERAHA LAMSHTUA

Anasema moja ya mambo ambayo yalimshtua, ni baada ya kushonwa nyuzi kutokana na jeraha la paji la uso alilolipata wakati wa mechi ya ligi akiwa anaenda kufunga bao na kulazimika kukaa nje kwa muda mrefu.

“Mambo ya kuona wachezaji wanapasuka uwanjani yalikuwa yakinitisha na kuniogopesha na mimi nikakutana na tukio hilo ambalo sasa ni historia kwangu," anasema na kuongeza;

"Nakumbuka tulikuwa tunacheza mechi ya ligi dhidi ya Geita Gold, nikiwa katika harakati za kutaka kufunga nilikosa mpira na kudondoka chini; beki wa timu pinzani akaupata na kuokoa na aliruka juu na wakati anatua aliniangukia juu ya paji langu la uso na kunipasua.”

Marungu anasema dakika zilikuwa zimeisha baada ya tukio hilo kutokea na mwamuzi alimaliza mechi na kupelekwa hospitali.

“Baada ya kufika hospitali nilimuuliza daktari kama kwa jeraha langu naweza kutibiwa bila kushonwa na aliniambia nimeumia sana natakiwa kushonwa. Nilikuwa muoga sana kwani ndiyo ilikuwa mara yangu ya kwanza, hivyo nilishonwa na nilikaa nje ya uwanja kwa muda, siwezi kusahau.”


NJUMU ZAKE LAKI SABA

Anasema suala la kupendeza au kuvaa anapenda vitu vizuri na siyo nje ya uwanja tu, hata uwanjani na anafunguka ana pea nyingi za viatu na kutaja gharama za moja ya viatu hivyo.

“Nina viatu vingi, sijui idadi na kiatu cha gharama kubwa nilikinunua nikiwa nje ya Tanzania. Nakumbuka nilikuwa Israel na nilikinunua kwa kiasi cha Sh700,000,” anasema na kuongeza;

“Napenda kuvaa vitu vizuri na naipenda kazi yangu; ninapopata nafasi ya kununua vitu nanunua kwa lengo la kufurahia ninachokifanya, si nikiwa nje ya uwanja tu, hata ndani ya uwanja nataka kuwa bora.”

MARU 05

ANAPENDA KUFUNGA

Anasema ishu ya kufunga mabao ni ya washambuliaji na hilo kwake ndilo analolipenda pale anapopata nafasi ikiwa pia ndiyo nafasi iliyomtambulisha.

“Ni kweli kuna wachezaji wanaoweza kucheza nafasi mbili na zaidi; kwa upande wangu eneo la mbele, ushambuliaji naweza kucheza nafasi zote, lakini nakuwa bora zaidi nikicheza mshambuliaji wa mwisho namba tisa,” anasema na kuongeza;

“Nikipangwa namba tisa nakuwa huru kucheza kwa sababu ndiyo nafasi niliyoanza kuicheza tangu nikiwa na umri mdogo baada ya kubaini kipaji changu ni kucheza hapo na ndiyo nafasi imenitambulisha hadi nafahamika.”