NYUMA YA PAZIA: Cristiano Ronaldo ameaga Manchester United kitoto

KUNA nyakati ambazo mambo hufika mwisho. Kwa Cristiano Ronaldo mambo yalifika mwisho Manchester United, Julai 2009, aliponunuliwa kwa dau la uhamisho wa dunia na Real Madrid. Akaenda zake kucheza mpira Hispania.

Akazunguka kwenda Italia halafu akarudi zake Manchester United hivi majuzi. Ilikuwa lazima aondoke tena Old Trafford. Hakuwa na maisha marefu sana. Lakini safari hii ameaga kitoto zaidi. Ni wazi kwamba tulitazamia ataondoka zake muda mfupi ujao lakini ukweli ni kwamba ameondoka isivyotarajiwa. Narudia. Ameondoka kitoto sana.

Wote tunajua kinachoendelea. Kwa sasa kuna mahojiano yake na Piers Morgan ambaye ni rafiki yake wa karibu. Ronaldo ameishambulia Manchester United kwa nguvu zake zote. Hakuna jiwe ambalo hajalifunua.

Msimu huu hakuwa na raha. Kocha wake ni mpya, Erik Ten Hag. Inachoonekana ni kwamba Ronaldo hakuwa katika mipango yake, lakini hata hivyo Mdachi huyu hakuwa na kitu cha kufanya. Alilazimika kumtumia Ronaldo katika namna alivyotaka lakini Ronaldo hakupenda.

Huu ndio mwanzo wa hasira zote za mahojiano ya Ronaldo na Morgan. Alichofanya, kwa mujibu wa Morgan, ni kwamba yeye Ronaldo ndiye aliyempigia simu Morgan kumwambia kwamba anataka kufanya mahojiano ya kuufungua moyo wake.

Mahojiano yalishafika siku kadhaa zamani lakini Ronaldo alikuwa anasubiri pambano la mwisho la Manchester United kabla ya Kombe la Dnia ili atoe mahojiano hayo ambayo yangevunja daraja lake la uhusiano na klabu hii ambayo kwa kiasi kikubwa imemsaidia kuwa supastaa mkubwa duniani baada ya kumtoa Lisbon akiwa kinda.

Alimwambia Morgan ayaachie mahojiano hayo mara tu baada ya pambano dhidi ya Fulham. Ni pambano ambalo pia aliamua kulikwepa. Kilichotokea baada ya mahojiano hayo kufanyika kwa kiasi kikubwa kilisaidia kufunika utamu wa bao la dakika za majeruhi la kinda wa Kiargentina, Alejandro Garnacho.

Lakini pia mahojiano yalikuwa yanamaanisha kwamba Ronaldo hatarudi tena Old Trafford. Amewashambulia matajiri wa timu, wachezaji wenzake wa zamani, wachezaji wenzake wa sasa, wapishi, lakini zaidi ni kocha wake, Ten Hag.

Ronaldo anajua kwamba Kombe la Dunia litamalizika Desemba 18. Zitakuwa zimebaki takribani siku 10 kabla ya kufunguliwa kwa dirisha dogo la uhamisho wa wachezaji barani Ulaya. Baada ya hapo atapata timu na kuondoka zake Old Trafford.

Inawezekana mpango wake umetimia mapema tu na ana uhakika wa kupata timu. Anaweza kurudi kwao kucheza Sporting Lisbon huku akipunguza mshahara wake kwa kiasi kikubwa. Lakini pia anaweza kwenda Uarabuni kulipwa mshahara mkubwa pengine kuliko ule anaolipwa na Manchester United.

Ronaldo kama angekuwa na busara angekaa kimya tu akaondoka zake kimyakimya. Yote aliyoongea yanamuacha akiwa na marafiki wachache Old Trafford. Katika mashabiki mia moja wa Old Trafford wanaomsapoti Ronaldo katika hili ni wawili au watatu.

Utoto wa hiki alichofanya unatokana na ukweli kwamba ana hasira za kutokuwa mchezaji muhimu tena katika kikosi cha Manchester United. Kama Ronaldo angekuwa anapangwa pangapangua ni wazi kwamba asingefanya mahojiano hayo.

Kudai kwamba klabu imemsaliti kunatokana na ukweli kwamba alijua Manchester United imemrudisha ili aendelee kuwa staa mkubwa ndani na nje ya uwanja. Lakini kitendo chake cha kumshambulia Ten Hag kwamba hamheshimu kinatokana na fikra zake kwamba yeye hastahili kukaa nje kwa namna yoyote ile.

Kwamba hastahili kutopangwa kabisa, hastahili kutolewa uwanjani, hastahili kuingia uwanjani kipindi cha pili. Ronaldo asipopangwa anakaa nyuma ya kiti cha Ten Hag na muda wote ananuna. Hata wenzake wakifunga bao ananuna. Ronaldo akianzishwa halafu akatolewa baadaye anatoka nje ya uwanja huku akitikisa kichwa kwa hasira.

Ronaldo akitaka kuingizwa uwanjani anakasirika na kugoma kama alivyofanya katika pambano dhidi ya Tottenham Hotspurs. Haya yote yanatokea kwa sababu anashindwa kuwa mkweli na mwili wake. Februari mwakani atatimiza miaka 38, lakini anajiona yuleyule wa miaka 10 iliyopita.

Tatizo ni kwamba hata anapopangwa huwa hana maajabu. Hili nalo halioni. Mwisho wa yote amehamishia hasira zake kwa kila mtu aliyepo katika klabu ya Manchester United. Wakati wenzake wakiwa katika juhudi kubwa za kujitafuta yeye anawavunja moyo.

Hii haikuwa namna sahihi ya kuondoka Manchester United. Wachezaji kama yeye wanatokea mara chache katika uso wa dunia. Na mara zote huwa wanaachana na klabu zao pendwa bila ya bifu la namna hii. Inajenga heshima kwa mashabiki.

Siamini kama Thierry Henry hakuona upungufu mkubwa wa Arsenal wakati anaondoka. Hata wakati ule aliporudi kucheza kwa mkopo akitokea Marekani nadhani alikuwa anaona upungufu mkubwa ndani ya Arsenal ikiwemo kikosi chenyewe cha Arsene Wenger ambacho kila siku kiliendelea kuwa dhaifu. Alichagua kukaa kimya.

Lionel Messi lazima aliona anguko kubwa la Barcelona katika siku zake za mwisho pale Catalunya, lakini aliondoka akilia kwa hisia baada ya klabu yake pendwa kuwa katika hali mbaya ya kifedha ambayo isingemuwezesha kubaki. Hata hivyo alichagua kukaa kimya.

Ronaldo ambaye ana hasira za kitoto ameamua kuzungumza. Ni mbinafsi kwa sababu amezungumza kutokana na kupoteza umuhimu mkubwa klabuni. Hapo ndipo anapoamini kwamba Manchester United imemsaliti, lakini pia ndipo anapoamini kwamba Ten Hag hamheshimu. Alikuwa anataka apangwe tu kwa sababu yeye ni Cristiano Ronaldo mmoja kati ya wachezaji bora kuwahi kutokea duniani.

Kitu kibaya kwake ni kwamba ameongea alichoongea huku watu wa Manchester United wakianza kuamini mradi mpya wa Ten Hag. Sawa kuna wakati timu inayumba, lakini wanahisi kwamba walau msimu huu kuna mwelekeo kuliko msimu uliopita.

Hapa ndio maana wengi wameamua kusimama nyuma ya Ten Hag na sio Ronaldo. Lakini kama Ronaldo angekuwa anaonyesha kiwango bora katika dakika anazopewa na Ten Hag, basi huenda angegawanya hisia za mashabiki na kuna kundi lingesimama nyuma yake.

Lakini kwa hiki kinachoendelea sasa hivi, tayari Ronaldo amepoteza heshima yake kwa mashabiki wa United. Angeweza kuziweka hisia zake kwa miaka kadhaa ijayo halafu akaandika katika kitabu chake, lakini kwa kuandaa mahojiano na rafiki yake Piers Morgan wanahisi kwamba anawavuruga.

Kumbuka kwamba walipopata ushindi mtamu dhidi ya Spurs, Ronaldo aliwahi kutoka uwanjani na vichwa vya habari vikabeba jina lake badala ya kushughulika na ushindi mnono wa United. Kumbuka kwamba wamewachapa Fulham ushindi mtamu wa dakika za mwisho Ronaldo akamwambia Morgan aachie mahojiano yao na yakavuruga utamu wa ushindi wao dhidi ya Fulham.

Sio tu mashabiki ambao wamemhama. Kuna watu wake ambao wamekuwa wakisimama nyuma yake kwa muda wote wa shida na raha zake. Kina Rio Ferdinand nao wamemhama. Nasubiri tu kusikia Roy Keane atasema nini, lakini zaidi nasubiri kusikia Sir Alex Ferguson naye atasema nini. Ni watu wake hawa lakini nahisi kwa utoto huu hawawezi kuwa nyuma yake. Tusubiri.