Prime
NOMA SANA! Wageni wafunika Bara misimu nane
KUTOKANA na rekodi za vinara wa mabao zinazoandikwa kila msimu, mastaa wa soka ndani na nje wamechambua zinavyoibua ushindani, wakisisitiza haijalishi zinazofikiwa ama kuvunjwa, kikubwa wanaona kila nyakati zina vitu vyake vya kukumbukwa.
Kauli za mastaa hao zilikuja baada ya Mwanaspoti kutaka kujua mitazamo yao wanaona ni mchezaji gani atakuwa mfungaji bora msimu huu na kama wanaona ni mzawa ama wa kigeni.
Staa wa zamani wa Yanga na Taifa Stars, Mohamed Hussein ‘Mmachinga’ aliyeweka rekodi ya kufunga mabao 26 mwaka 1999 amesema: “Kila msimu una utofauti na zipo rekodi mbalimbali zinazotakiwa kuvunjwa kwanza kabla ya kufikia mabao yangu na ya Abdallah Juma mchezaji wa zamani wa Mtibwa Sugar alifunga mabao 25 mwaka 2006.”
Anaongeza: “Katika msimu huu washambuliaji wana kazi ya kuvunja ama kufikia rekodi ya mabao 21 aliyoyafunga Stephane Aziz Ki akiwa Yanga 2023/24 kisha ya mshambuliaji wa zamani wa Simba, Meddie Kagere ya misimu miwili 2018/19 mabao 23 na 2019/20 mabao 22, watafuata ya Juma ya mabao 25 kisha ya kwangu ya mabao 26, naamini wanaweza wakaandika nyingine mpya itategemeana na ushindani na kujituma kwao.”
Mmachinga amesema mbali na kuvunja rekodi hizo, anaheshimu kila aliyewahi kuibuka kinara wa mabao anajua alifanya kazi ngumu, mtazamo wake kwa msimu huu anauona utakuwa wa mabao mengi, hivyo iwe wa kigeni ama mzawa anaweza akafunga mabao zaidi ya 20.
Kwa upande wa Kagere anasema: “Binafsi nikifanya kazi sijilinganishi na mwingine akili yangu inakuwa ni kuipambania timu, najivunia kuacha rekodi Ligi Kuu na klabu ya Simba, wachezaji waliyopo na wenyewe wana mchango wao na wana kitu cha kukumbukwa kwa nyakati zao.”
Kagere misimu iliyofuata (mabao 13, 2020-2021)
(2021-2022-mabao 7), Singida Black Stars (2022/23 mabao 8),(2023/24-mabao 2) na Namungo (2024/25-hakuna bao), amesema: “Panda shuka kwa mchezaji ni kawaida kikubwa ni kujitambua.”
Mshambuliaji George Mpole akiwa na Geita Gold msimu wa 2021/22 alifunga mabao 17 amesema:” Kila msimu unakuwa na ushindani wake, nilipoweka rekodi ya mabao 17 ikafikiwa na aliyekuwa mshambuliaji wa Yanga, Fiston Mayele msimu wa 2022/23 pia ikavunjwa ikaandikwa mpya msimu wa 2023/24 na Aziz Ki aliyefunga mabao 21, ingawa msimu uliyopita Charles Ahoua wa Simba alifunga mabao 16 alifanya kazi nzuri kwa nyakati zake.”
Staa wa zamani wa Simba, Mussa Mgosi anasema kwa sasa ni ngumu kujua nani ataibuka mfungaji bora kwani bado upande huo haujaanza kuchangamka.
“Naheshimu wachezaji wazawa wanaongoza kwa sasa Paul Peter mabao matano na Saleh Karabaka mabao manne wanaochezea JKT Tanzania, wanatakiwa kukaza buti na kujua inawezekana wakaibuka wafungaji bora, iliwahi kutokea hivyo kwetu zamani tulikuwa tunashindana na wageni vilevile,” amesema kocha msaidizi wa Simba Queens.
Kwa upande wa Karabaka anasema: “Japokuwa mabao manne ni rekodi mpya kwangu ila msimu huu naamini naweza nikafunga hata mabao 20.
Katika misimu minane wazawa wamechukua mara mbili na wageni mara sita, jambo ambalo kocha wa zamani wa Simba, Abdallah Kibadeni anasema: “Kwa afya ya timu ya taifa Stars, wazawa wanapaswa kupambana kuhakikisha hawabaki nyuma kuwania kiatu cha ufungaji bora.”
Winga wa zamani wa Simba na Taifa Stars, Emmanuel Gabriel anasema: “Kwa misimu hiyo nane wageni wamechukua mara nyingi tunahitaji wazawa wapambane kwani watasaidia katika timu ya taifa, ingawa haina maana kwamba hawafanyi kitu, wanapambana ila waongeze ushindani katika kuweka rekodi hizo.”