Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

NIONAVYO: Hamasa ya mama darasa la walezi wa michezo

MAKALA za mwanzo za safu hii zilianza katika kipindi cha mwanzoni mwa msimu wa mashindano ya vilabu barani Afrika.Mtazamo wa mwandishi (bila shaka mtazamo wa Mwanaspoti) ilikuwa ni kuona Tanzania ikifanya vizuri na kila mwaka iwakilishwa na vilabu sita (inawezekana vikawa vinane iwapo klabu za Tanzania Zanzibar zitafanya vizuri pia).Hapa chini ni sehemu ya makala mojawapo:

Nafasi ya klabu zetu Afrika

“Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ina nafasi ya pekee katika mashindano ya klabu za mpira wa miguu Afrika. Kwamba tofauti na ilivyo kwenye timu za taifa ambako ni timu moja tu (Taifa Stars) ya muungano inayowakilisha nchi,kwenye ngazi za klabu Tanzania Bara inapewa nafasi kwenye mashindano ya ligi ya mabingwa na kombe la shirikisho na Tanzania visiwani ina nafasi kwenye mashindano hayo mawili ya klabu za Afrika.

Kwa bahati na zidi shukrani kwa mafanikio ya klabu ya Simba katika mashindano ya Afrika,timu zinazoshiriki ligi ya bara zina nafasi mbili zaidi hivyo kufanya nchi kuwakilishwa na timu 6 yaani 3 ligi ya mabingwa (Yanga,Simba na KMKM) na 3 kombe la shirikisho (Azam,Geita na Kipanga).

Kwa bahati mbaya tayari timu mbili za Geita Gold na KMKM zimekwishatolewa mashindanoni hivyo tumebaki na timu nne.
Mashindano niliyotaja hapo juu yana fedha nyingi sana hasa klabu inapofanya vizuri kama kucheza ngazi ya makundi,robo,fainali,nusu fainali,fainali na kuchukua ubingwa. Kuna pesa ambazo zimefanya klabu zinazoshiriki mashindano haya kuanzia ngazi ya makundi kurudi sura zilezile kila mwaka kwa sababu wanajua umuhimu na utamu wa kushiriki lakini pia kushiriki kwao kunawafanya kupata kipato kinachowawezesha kuwekeza na kugharimia ushiriki mzuri kwa kila mwaka unaofuata.
Kwa sasa mshindi wa Ligi ya Mabingwa Afrika inayodhaminiwa na kampuni ya nishati ya Total ya Ufaransa, anapata kiasi cha fedha kinachokaribia Sh 6 Bilioni wakati kuingia kwenye hatua ya makundi tu klabu inapata karibia Sh 1.3 bilioni.

Viwango kwa upande wa Kombe la Shirikisho Afrika ni takribani nusu ya vile vya ligi ya mabingwa. Mashindano haya ni fursa kwa klabu na kwa taifa kujitangaza, kuingiza watalii wa kimichezo na kujiingizia kipato.

Iwapo itakuwepo nia ya dhati ya kuviunga mkono vilabu na kutafuta wawekezaji kwenye klabu, hasa vinavyowakilisha nchi, vinaweza kufanya vizuri na kubaki na
nafasi hizi sita na hata kuongezeka kuwa nane iwapo klabu za Zanzibar zinaweza pia kufika mbele zaidi.


Zanzibar ndiyo inawezekana kama ilivyofika nusu fainali ya Kombe la Washindi Malindi FC iliyokuwa ikidhaminiwa na marehemu Nourshad Mohammed.
Tunaweza kufika mbali na kuwa washiriki wa kila mara kama ilivyokuwa kwa nchi kama Morocco.
Tanzania tunaweza kutumia ushiriki wa klabu zetu kama moja ya nyenzo za kuifungua nchi kwa dunia kwa lengo la kukuza uchumi na ustawi wa taifa.

Safu hii inampongeza kiongozi mkuu Rais Samia Suluhu Hassan kwa namna alivyoliunganisha taifa kwa hamasa alizotoa kwa klabu za Yanga na Simba katika ushiriki wao wa michuano ya Afrika na sasa kwa namna ya pekee alivyowaleta Watanzania pamoja katika kuhakikisha wanakuwa pamoja na klabu ya Yanga inapocheza fainali za kombe la Shirikisho Afrika dhidi ya USM Alger ya Algeria siku ya Jumapili.
Akiongea na watanzania kupitia kituo kimoja cha televisheni wiki iliyopita,Rais Samia aliwataka watanzania na hasa TFF kuwa karibuna hata kuwasemea vizuri ili waweze kufanya vizuri katika fainali yao.
Mara tu baada ya tamko la Rais tumeshuhudia Bodi ya Ligi na TFF wakishughulika na hata kuhakikisha kuwa ratiba ya michuano ya ndani haiingilii maandalizi ya Yanga kwa michezo ya fainali.
Rais Samia ametoa ndege kwa ajili ya kusafirisha timu na mashabiki kwenda kwenye fainali ya pili mjini Algiers. Sambamba na hilo ameongeza kiasi cha bonasi ya ushindi kwa timu na pia kununua tiketi 5000 za kuwezesha mashabiki kuingia uwanja wa Mkapa kuipa nguvu Yanga.
Baada ya ishara hiyo ya Rais kufanya juhudi hizo, kumejitokeza uungwaji mkono kutoka viongozi wa serikali , makampuni na watu binafsi.
Hekaheka zinazoendelea ni ishara ya namna michezo inavyoweza kuileta nchi pamoja na kuweza kufanikisha malengo ya kiuchumi,kisiasa na hata kijamii.Rais Samia ameonyesha njia katika uongozi na namna ya kufanikisha michezo.Juhudi za kuiwezesha Yanga kushinda iwe ni chachu kwa viongozi wa shirikisho la mpira wa miguu wa bara na visiwani na hata wa michezo mingine kwa ujumla wake kujifunza namna ya kufanikisha jambo la kuleta mafanikio kwa taifa hata katikati ya tofauti ya itikadi za Imani,siasa na maslahi mengine.
Nathubutu kusema tena kwamba chini ya Rais Samia,Tanzania ina mazingira bora kabisa ya kuendeleza michezo yakitumiwa vizuri. Kila la Kheri Young Africans,Kila la Kheri Tanzania.
Mwandishi wa makala hii ni Katibu Mkuu mstaafu wa Shirikisho la mpira wa miguu Tanzania (TFF). Unaweza kumtumia maoni yako kupitia simu yake hapo juu.